Waridi wa BBC: 'Mambo ni mawili, umrushe mtoto mtoni au niwauwe nyote wawili'

    • Author, Na Asha Juma
    • Nafasi, BBC Swahili Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kila anapokumbuka usiku ule wa kutisha, Marion Watswenje anajihisi kama mtu aliyefufuka kutoka kaburini. Alishtuliwa kutoka usingizini na maneno ambayo yangeweza kuwa ya utani, lakini hayakuwa hivyo.

"Aliniamsha usiku wa manane akaniambia, unaona ule mto unaoitwa Riverside, siku moja nitaamka na wewe hapa nikakutumbukize humo ndani."

Siku iliyofuata, saa sita za usiku, aliamshwa tena. Mara hii si kwa maneno ya kutisha tu, bali kwa kitendo kilichomuweka ukingoni mwa maisha na mauti.

"Nikambeba mtoto mgongoni. Akaniambia tunaenda hospitali. Tulipofika kwenye mto, alinigeukia na kusema, hapa ndipo maisha yenu yanaishia. Mambo ni miwili, umrushe mtoto mtoni au niwaue nyote wawili."

Kauli hii ya mume wake aliyosheheni maneno mazito ilibadili kabisa mtazamo wake wa maisha hadi leo.

Katika simulizi hii, Marion Watswenje anasimulia jinsi ndoa yake ilivyogeuka kuwa jinamizi na namna kifo kilivyomkabili usoni.

Tahadhari: Baadhi ya simulizi inaweza kukuumiza moyo

Karibu.

Safari ya maisha yake ni hadithi ya simanzi

Marion, alimpoteza mama yake mzazi mnamo mwaka 1997, na hivyo akalelewa na bibi yake.

Akiwa katika malezi ya bibi, alipata ujauzito na hilo likamlazimu kutafuta maisha kwingineko.

Kipindi hicho alikimbilia kwa mjomba wake kujistiri.

Huko alitafutiwa kazi ya ndani ili kujikimu kimaisha hadi alipojifungua.

Lakini kufikia mwaka mwaka 2010, alimpoteza bibi yake na muda mfupi baadaye, akakutana na mwanaume ambaye angemuita mume wake….nyonda mkalia ini.

Tofauti kidogo pengine na wengine ambao wanachukua muda kufahamiana, Marion na mwandani wake walikuwa wamejuana kwa siku tatu pekee.

Na hivyo ndivyo walivyoamua kuanza kuishi pamoja kama mke na mume hasa baada ya kumuarifu kuwa anatafua mtu wa kuishi naye.

Marion alikuwa na matumaini na ndoa yake, kama wanawake wengi, matarajio ya amani, upendo na maisha bora. Lakini haikuchukua muda kugundua kuwa aliingia kwenye shimo la mateso. Mume wake aligeuka mtu mwingine: mlevi, mwenye hasira, asiyejali familia, na hatimaye, mwenye mawazo ya mauaji.

Tangu mwanzo, maisha yalikuwa na panda shuka. Ujauzito wake wa kwanza ulifungua mlango wa mateso ya kimwili, kiakili na kihisia. Mtoto aliyezaliwa alikumbwa na matatizo ya kiafya, lakini mume wake hakuonekana kujali hata kidogo.

"Alianza kubadilika, akawa mara harudi nyumbani, anakuja akiwa mlevi, naenda kumtafuta baa, sio tena ile ndoa niliyotarajia," anasema Marion.

Pia unaweza kusoma:

Wakati huo, alifanikiwa kukutana na Meresa Achieng aliyegeuka kuwa rafiki yake wa dhati, aliyempa moyo na matumaini kwamba iko siku mambo yatakuwa mazuri.

Alipoanza kupata maumivu ya kujifungua alipokuwa mjamzito wa mtoto wake huyo wa kwanza, ambaye kwa mumewe ni wa pili, alimuarifu mume wake ambaye hakuwa karibu akaamua kujipeleka hospitali.

Alijifungua salama na mume wake alichofanya ni kumpa pesa za kupanda bodaboda wakati wa kurejea nyumbani lakini yeye mwenyewe akatokomea.

"Hivi ndio mtu akiolewa mumewe anafaa kumfanyia?" ni baadhi ya maswali ambayo Marion alikuwa anajiuliza, wakati anarudi nyumbani na mwanawe mchanga.

"Kwa neema za Mwenyezi Mungu, nilifika nyumbani lakini mambo hayakuwa rahisi. Kwa mila za Kijaluo, mwanamke ambaye amezaa haruhusiwi kupika, kwa hiyo, nikawa hata nikiwa na njaa siwezi kujipika, hadi nimsubiri mume wangu atakaporejea nyumbani".

Kadiri siku zilivyosonga mbele, Marion alikuwa na maswali mengi akilini mwake.

Masaibu aliyokumbana nayo

Mume wa Marion alianza kutojishughulisha nao lakini nguzo iliyomsimamisha imara ni imani yake kwamba iko siku mambo yatabadilika na kuwa sawa.

Marion anasema, changamoto ziliongezeka pale mtoto wao alipoanza kuumwa.

Sehemu yake ya kupata haja ndogo ilikuwa na uchungu sana wakati anajisaidia na kila alipomuarifu mume wake kwamba mtoto anaumwa, alikuwa mkali mno.

"Kuna wakati hali ya mtoto ilikuwa mbaya sana. Eneo la kupata haja ndogo iliziba kabisa, nilipofika hospitali walisema awekewe bomba au afanyiwe upasuaji, sikuwa na pesa."

Marion anaendelea kusema, "Wakati mtoto alikuwa mgonjwa, nilikuwa naenda tu hapo hospitali, ninakaa nje, nione kama kuna ambaye angeweza kunisaidia, na ikifika wakati anataka kujisaidia alikuwa akilia sana.

Mtu mmoja alipendekeza kuwa mtoto atahiriwe kwanza ili kuona kama eneo la kupata haja ndogo linaweza kufunguka, lakini Marion alihoji kuwa ngozi na eneo la haja ndogo ni sehemu mbili tofauti.

Marion alihisi kuchanganyikiwa wakati ambapo mtoto alizidiwa, akawa hana la kufanya, na mume wake aliyetarajia kuwa msaada wake, akakimbia familia yake.

"Yeye alitutoroka, hauna kazi, mtoto ni mgonjwa, kula ni shida, mwenye nyumba alikuja akanibomelea paa la nyumba upande mmoja wakati mvua inanyesha," Marion anasimulia.

"Ilifika wakati ikawa akilala, unasikia harufu ni kama mikojo inakuja na mdomo na kwenye pua," Marion anasema.

"Nilikuja nikapata msamaria mwema akaisaidia. Alilazwa hospitali wiki ya kwanza na kufikia ya pili, akawa yuko sawa. Tukaruhusiwa kurejea nyumbani."

Meresa, ambaye alisimama na Marion wakati anapitia changamoto za maisha, alikuwa akiwapa chakula cha mchana watoto wa Marion.

Wakati huo huo, Marion alikuwa anajitahidi kutafuta vibarua vya kufua ili watoto wake wasikose kupata riziki hata kama ni mara moja kwa siku.

Wakati alikuwa anafikiria changamoto zimepungua, ndio mwanzo zilikuwa zimeanza.

Mtoto wa Marion alianza tena kuumwa na viungo.

"Nilipomuomba pesa za matibabu, aliniambia, nimekuonyesha kwetu, nikakakwambia huyo mtoto siku atakufa, mpeleke aende azikwe."

Anasema, mume wake alikuwa amezidisha vitimbi.

"Anaenda anaoa, anarudi, anaoa anarudi". Unajaribu kulinda ndoa lakini haikaliki. Hiyo ndoa sio yako na umejilazimisha kabisa. Kuombea kitu ambacho si chako ni kitu kibaya sana," Marion anasema.

Siku moja wakati Marion alikuwa ameenda kanisani, alitumiwa ujumbe na mume wake kwamba akirejea nyumbani, atamuua.

Baada ya kuwashirikisha ujumbe ule, waliamua kwenda naye nyumbani ili kutathmini hali iko vipi.

Walipoingia, walimkuta mume wake akiwa ameweka nyundo juu ya kiti huku kisu kikiwa chini ya kitanda, Meresa aliyekuwa akimshika Marion mkono wakati anapitia changamoto za maisha, alithibitisha hilo.

'Alitaka nimtupe mtoto wetu mtoni'

Baada ya mume wa Marion kutoroka família yake kwa muda, alirejea tena huku akijifanya amebadiilika

"Alinunua TV kubwa, akatupeleka kwenye nyumba ya mawe, akanunua woofer, maisha yalibadilika. Hata kama nilikuwa nimeteseka lakini nilifikiria kurudi kwenye maisha ya zamani sio jambo zuri."

Alichosahau Marion ni kuwa tabia ni kama ngozi haibadiliki, alirudi tena kuwa mnyama. Mtoto alipoanza tena kuwa mgonjwa, shida zikarudi upya.

"Alikuwa anatoka vidonda mwili mzima na huyo mtoto akiwa mgonjwa siku mbili unaweza kufikiria ameumwa miezi minne."

Safari hii mume wa Marion alikuja kivyengine. Alianza kumtishia maisha, akimwambia "sio lazima tuishi na wewe, nitakuua."

"Ainiamsha usiku akaniambia, unaona ule mto wa Riverside, siku moja nitaamka na wewe hapa nikakutumbukize humo ndani."

Lakini Marion aliamua kutoshtuka kwa sababu tayari alikuwa amepitia mengi.

Asichokijua ni kwamba maneno hayo hayakuwa utani, bali alimaanisha.

Siku hiyo alirudi akiwa mkimya, akawa amelala kitandani. Wakala chakula cha jioni, Marion asijue kilichokuwa kinamsubiri.

"Ilipofika saa nane usiku aliniamsha akaniuliza, umefikiria nini kuhusu maneno niliyokwambia, Nikamuuliza yapi hayo, akaniambia, sinilikwambia sio lazima niishi na wewe na nitakuua."

Maneno hayo yalimtia Marion hofu kubwa. Yalikuwa maneno makali kiasi kwamba alikosa nguvu ya kumshirikisha yeyote.

Siku iliyofuata. Alimuamsha saa sita usiku. "Aliniambia beba huyu mtoto."

"Nikafunga mtoto mgongoni tukatoka. Akaniambia tunaenda hospitali. Tulipofika kwenye mto, akasema, hapa ndio maisha yenu yanaishia. Mambo ni miwili, umrushe mtoto au niwauwe nyote wawili."

Lakini wakiwa katika harakati hizo, polisi walijitokeza na akawauliza munafanya nini hapa?

Mume wa Marion alikimbilia kujibu kwa haraka kwamba wanaenda hospitali wasijue kuwa lengo na nia yake ilikuwa kumrusha mtoto aliyebebwa.

Hivyo ndivyo walivyoonusurika kifo kupitia tundu la sindano.

"Mimi nimeepuka kifo mara nyingi sana," Marion anasema aliwahi kuripoti polisi lakini hakupata usaidizi.

Tazama hapa

Mfadhaiko kwa mtoto

Cha kusikitisha zaidi, mtoto aliyekuwa anapangiwa uovu huo, alikuwa anazungumza, anasoma na alisikia yaliyotendeka.

Siku moja alimuuliza mama yake, "sasa baba akirudi si atamuua hadi yule yuko tumboni?" Kipindi hicho, Marion alikuwa amepata ujauzito wa mtoto mwingine.

Hapo ndipo akagundua kuwa mwanawe anajua kilichotokea.

Alivyosonga mbele

Marion anasema ilifika mahali akawa amechoka.

"Sioni utamu wa ndoa. Nimechoka." Na hapo ndipo alipopata ushauri kutoka kwa mchungaji wake kuwa atoke kwenye ndoa hiyo, ikawa kama ufunguo wa ukurasa mpya maishani mwake.

"Nilifika mahali, nikajiita mkutano, nikajiambia maisha yangu yataendelea bila yeye, nilifuta namba zake za simu, kila kitu, nikaamua kuanza upya."

Tofauti na wakati uliopita ambao alikuwa akijiambia hana pa kwenda kwa sababu hakuwa na wazazi.

Ushauri wa Marion

Marion anasema kuna nyumba nyingi ambazo zinateseka huko nje.

"Ukisikia unaishi na mtu na anakwambia atakuua, usikae ungoje. Mimi ningekuwa nilimtegemea huyo mwanaume, saa hivi ningekuwa nimeoza."

Usione mama ameketi ukamuita majina mabaya, au umchukulie vile unataka, tunapitia mambo mengi sana ndani ya ndoa, lakini afadhali unywe hata maji tu, au hata ulale njaa ila upate amani ya moyo wako.