Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wayne Rooney azungumzia uraibu wake wa pombe
Nahodha wa zamani wa Uingereza Wayne Rooney ameeleza katika kipindi kipya cha mtandaoni cha Rob Burrow kuhusu uhusiano wake na pombe katika siku za mwanzo za maisha yake ya soka.
Rooney alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na umri wa miaka 16 akiwa na Everton na haraka tu akawa maarufu.
Rooney, ambaye sasa ana umri wa miaka 38, ndiye mgeni wa kwanza kwenye mfululizo wa kipindi kipya cha The Total Sport cha BBC kinachoendeshwa na Rob Burrow.
Alipoulizwa na Burrow kuhusu kukabiliana na changamoto katika maisha yake ya soka, Rooney, ambaye aliifungia England mara 53 na ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Manchester United, aliibua suala la pombe kuwa moja ya changamoto ngumu zaidi.
Alimwambia Burrow: "Changamoto yangu ilikuwa pombe nilipokuwa na umri wa miaka 20. Nilikua nikinywa karibu kuzimia. Sikujua jinsi ya kukabiliana nayo. Sikutaka kuwa karibu na watu, kwa sababu wakati mwingine najihisi aibu."
Rooney, ambaye sasa ni meneja wa Birmingham City, anasema: "Usipotaka msaada na mwongozo wa wengine, unaweza kuwa katika hali ya mbaya sana, na nilipitia hali hiyo kwa miaka michache.
"Nashukuru, sasa siogopi kwenda kuzungumza na watu kuhusu jambo hili."
Wageni wengine
Wageni watakao kuja kwenye kipindi hicho ni pamoja na mshindi wa kombe la dunia la chama cha raga cha Uingereza Jonny Wilkinson, Dame Kelly Holmes aliyeshinda medali ya dhahabu ya Olimpiki mara mbili na mshindi wa medali ya dhahabu ya Paralimpiki mara saba Hannah Cockroft.
Mada nyingine ambazo Rooney aliulizwa na Burrows ni pamoja na mchezaji anayempenda zaidi na wachezaji wenzake ambao hawakuwa na maelewano mazuri.
Burrow anasema "amependa" kufanya kazi kwenye kipindi kitakachotoa mahojiano mapya kila Jumatano na kuzungumza na magwiji wa michezo.
Mwendeshaji wa kipindi
Rob Burrow ni nyota wa mchezo wa raga ambaye anatumia teknolojia ya akili bandi kurikodi sauti yake na kuwasilina. Burrow mwenye ugonjwa MND, unaoathiri ubongo na mishipa ya fahamu.
"Kuwa na ugonjwa huu haimaanishi sina sauti. Ninaishi maisha kamili na kila siku niko tayari kujitolea. Nafurahi sana kuweza kuonyesha utu wangu katika kipindi hiki na kucheka."
Tanya Curry, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha MND alisema: "Kwa kutumia msaada wa teknolojia – Rob huzungumza na wageni na kufanya hivyo anaondosha kasumba kuhusu watu wanao ugua ugonjwa huo."