Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, kuna vyakula vinavyoweza kukufanya unukie vizuri?
Tunajua kwamba tunapokuwa na joto, tunatoka jasho zaidi. Ni njia ya miili yetu ya kutunza baridi: kila tone la jasho ambalo hutoka kwenye ngozi yetu husaidia kupunguza joto letu .
Lakini hata ikiwa ni lazima, mchakato huu wakati mwingine huja na athari zisizofurahisha.
Ndio, tunazungumza juu ya harufu.
Kila mtu ana harufu tofauti anapotoka jasho: baadhi ya watu huwa hawatoi harufu, wakati kwa wengine inaweza kuwa harufu kubwa, na inayokera sana.
Profesa Johan Lundström wa Taasisi ya Karolinska huko Stockholm amefanya utafiti mkubwa kuhusu uvundo au harufu na manukato.
Anasema kwamba harufu ya jasho letu inategemea vigezo vingi tofauti.
"Harufu ya mwili wetu hutokana na a mchanganyiko wa vitu mbalimbali vinavyotolewa na tezi tofauti, ambayo pia inategemea kwa kiasi kukibwa na jeni zetu, idadi ya bakteria katika mwili wetu (kutokana na mambo kama usafi), na mazingira ( unyevu, joto, hewa na mengine).
"Na hatimaye, kile tunachokula kinaweza pia kuwa na mchango muhimu katika hili."
Kwa hivyo pamoja na mambo haya dhahiri zaidi kama vile chembe za urithi na jinsi tunavyoshughulika na usafi wa mwili, chakula tunachokuwa na kuingia ndani ya miili yetu kinaweza kuwa na mchango muhimu kwenye jasho letu na namna harufu yake itakavyokuwa.
Chakula ambacho hubadilisha harufu ya mwili wetu
Hatujui ni kwa kiwango gani chakula huathiri harufu tunayotoa tunapotoka jasho.
"Kwa ufahamu wangu wote, hili halijatathminiwa rasmi," anasema Lundström.
Lakini tunajua ni vyakula gani vina uwezekano mkubwa wa kuathiri harufu.
"Watu wanaokula nyama nyingi kwa ujumla wana harufu 'mbaya zaidi' kuliko wale walio na lishe inayotokana na mimea.
"Pia, kama inavyoonekana kwa wengi, mtu anayependa kula kitunguu saumu pengine atakuwa na harufu kali katika jasho lake," anasema.
"Vitu vingi vinavyoingia kwenye damu hutolewa kwa namna moja au nyingine kupitia harufu ya mwili wetu."
Kwa hiyo, kwa mfano, vitunguu na nyama vina salfa ambayo, mara moja hutumiwa, hutoka kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jasho.
Na kwa harufu ya kuvutia zaidi?
Ingawa kuna utafiti mdogo juu ya vyakula maalum ambavyo vinaweza kufanya jasho lako liwe na harufu nzuri, tafiti zingine zinaonyesha ni lishe gani ina uwezekano mkubwa wa kusababisha harufu ya jasho lako kuwa "ya kuvutia".
Jaribio moja kama hilo lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Macquarie huko Australia.
Washiriki wa kiume 43 walioga kwa maji tu kabla ya kuvaa fulana zilizotengenezwa kwa pamba (manukato hayakuruhusiwa).
Walivaa mashati kwa saa 48, ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi kwa saa moja ili kuchochea tezi za jasho, kabla ya kuwapeleka mtaani kwa uchunguzi wa harufu.
Matokeo?
Wanaume ambao walikuwa na ulaji wa juu wa matunda na mboga "walihusishwa kwa kiasi kikubwa na jasho la harufu ya kupendeza zaidi (yenye sifa nyingi za maua, matunda, na dawa), bila kujali kiwango cha jasho."
Wale ambao walikuwa wamekula vyakula vya mafuta mafuta, nyama, mayai, pia walikuwa na harufu nzuri vizuri.
Hata hivyo, wale walio na ulaji mwingi wa vyakula vya wanga (mfano wali,ugali,viazi, mihogo) walisemekana kuwa na 'jasho zito na lisilo la kupendeza' , kwa ufupi harufu mbaya.
Katika utafiti mwingine kuhusu mvuto wa jasho la wanaume, wanaume 17 walikula ama chakula chenye nyama nyekundu au ambacho hakikuwa na nyama kabisa. Sampuli za jasho zilikusanywa baada ya wiki mbili.
Mwezi mmoja baadaye, walirudia jaribio hilo, na washiriki wote walibadilisha lishe.
Hatimaye, kundi la wanawake 30 lilikadiria jasho hilo kulingana na jinsi lilivyokuwa zuri, la kuvutia, na la kiume.
Jasho la wanaume mara kwa mara lilionekana kuwa la kupendeza zaidi walipokuwa wakifuata lishe ambayo haina nyama.
Kama ilivyo kawaida katika tafiti za kisayansi, kuna utafiti mdogo sana unaohusisha washiriki wa kike.
Hata hivyo, uchunguzi mmoja mdogo ulibainisha kuwa wakati jasho la wanawake watatu lilipochambuliwa kabla, wakati, na baada ya "kuzuiwa ulaji wa vyakula vyenye kalori," wanaume waligundua kuwa jasho la wanawake lilikuwa nzuri zaidi mara tu walipoanza kula tena vyakula hivyo na harufu isiyo ya kupendeza wakati wamezuiwa kula kalori.
Kwa hivyo ni jambo la thamani ya kubadilisha mlo wako ili kuboresha harufu ya mwili wako?
Badala ya kula vyakula maalum ili kujaribu kuboresha, Lundström anasema kimantiki, ni "rahisi zaidi kutumia manukato."
Zaidi ya hayo, yuko tayari kusema kwamba hata kama wewe ni "mtu mwenye harufu mbaya," huenda sio daima kuonekana hilo ni kama jambo baya.
"Kuna tofauti kati ya nchi ambazo harufu za mwili zinakubaliwa au la. Na hata tofauti zaidi hutokana na mazingira ambayo harufu ya mwili inasikika.
"Kwa mfano, harufu ya mwili ukiwa kwneye maeneo ya mazoezi (gym) au kitandani na mtu unayempenda inaonekana tofauti sana kuliko harufu kama hiyo katika hali ambapo usafi unathaminiwa sana, kama vile unapoketi karibu na mtu asiyemjua kwenye basi. .
"Pamoja na hayo, mwenzi anayetarajiwa atapenda harufu yako ya asili ya mwili!"
Kwa kweli, hiyo ni njia moja ya kupima utangamano wako na mtu.