Kwa nini raia hawa wa Somalia wameamua kukabiliana na Al-Shabaab

Raia wa Somalia

Chanzo cha picha, SNTV

Vita dhidi ya Al-Shabaab bado vinaendelea nchini Somalia hasa eneo la Hiran, katika oparesheni ambayo inafanywa na wanamgambo wa kijamii wa eneo hilo ambao wanaungwa mkono na vikosi vya serikali.

Ingawa ni vigumu kupata habari huru kutoka katika maeneo ambayo vita hivyo vinaendelea, vyombo vya habari vya serikali vilisema kwamba jeshi lilichukua mamlaka kutoka kwa Al-Shabaab katika eneo liitwalo Booco, ambalo ni takriban kilomita 45 kusini mashariki mwa Beledweyne.

Televisheni ya Taifa, ikimnukuu Gavana wa eneo la Hiran, Ali Jeyte Osman, ilisema kwamba Al-Shabaab wameondoka eneo hilo na walikuwa na "kambi na mahakama yao".

Zaidi ya wanamgambo 100 wa wanamgambo wa Al-Shabaab waliripotiwa kuuawa katika mapigano hayo yaliyotokea katika muda wa siku tatu zilizopita.

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Somalia na kuchapishwa kwenye tovuti ya Televisheni ya Taifa, wanajeshi wa Marekani wanaunga mkono serikali.

"Msaada wa anga uliotolewa na Marekani umechangia katika operesheni zinazoongozwa na Wanajeshi," ilisema taarifa hiyo.

Mikoa jirani ya Hiraan na Galgaduud katika wiki za hivi karibuni imekuwa kitovu cha vita dhidi ya Al-Shabaab, ambayo ni maarufu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Katika ujumbe wa mwisho wa video, msemaji wa Al-Shabaab Ali Dheere aliwatishia wakaazi wa eneo hilo ambao wanapinga kundi hilo.

Ni nani anaongoza oparesheni?

Mpiganaji

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika mahojiano hapo awali mmoja wa viongozi wa Hiran, alimbia BBC Somali kwamba walijipanga kupigana na Al-Shabaab.

Alidokeza kwamba wamejitolea kulipiza kisasi kila mtu aliyeuawa na Al-Shabaab.

Kwa upande mwingine, taarifa zinazotolewa na serikali au kusambazwa katika vyombo vyake vya habari zinasema kuwa operesheni hiyo inaongozwa na Jeshi.

Hata hivyo, inasadikiwa kuwa baadhi viongozi wa eneo hilo wanaopinga mashambulizi ya Al-Shabaab, wameanza kuchukua silaha na kuwahimiza watu kupigana.

Kwa vyovyote vile, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ambaye amerudia mara kadhaa kwamba wanapigana dhidi ya Al-Shabaab, amewapongeza watu wanaokabiliana na kundi hilo na kuwaahidi uungwaji mkono wa serikali.

Abdisalam Guled, naibu kamanda wa zamani wa Shirika la Usalama wa Kitaifa na Ujasusi nchini Somalia, aliambia kipindi cha BBC Newsday kwamba vita vinavyoendelea vinaongozwa na wakaazi wa eneo hilo.

“Vita hivyo viko katika kiwango cha juu zaidi...na vinaendelea katika eneo ambalo naweza kukadiria kutoka kilomita 200 hadi 300,” alisema Abdisalaam.

Aliongeza: “Katika muda wa wiki mbili au tatu zijazo, inawezekana tutaona jeshi la ATMIS na vikosi vya serikali vikishiriki kikamilifu katika vita hivyo, kutoka pande tofauti.

“Pia alibainisha kuwa kuna makabila mengine yanajipanga pamoja.

Sababu zilizosababisha watu kupigana

Abdisalaam Guled anaamini kwamba Al-Shabaab, ambayo katika miaka mitano iliyopita "ilivuka mipaka ya shinikizo lake kwa watu", hali ambayo ilichangia uasi dhidi yao.

Anatoa mfano wa "kodi na mizigo kwa kundi hilo" ambayo imekuwa ngumu kwa watu kumudu.

Mbali na hayo, pesa na wanyama hai huchukuliwa kutoka kwa watu na kwamba familia zilidai watoto wao wa kiume kujiunga na wanamgambo wa Al-Shabaab, hali ambayo kulingana na Abdisalam ilifanya watu kufanya auasi dhidi yake.

Tangu Rais wa Somalia aingie madarakani, ameonyesha kwamba serikali yake imejitolea kusaidia wananchi katika kukomboa maeneo yao kutoka kwa Al-Shabaab, jambo ambalo Abdisalam anaona kuwa ni jambo jingine ambalo limewatia moyo wanamgambo wa kikabila.

"Hii ndiyo sababu iliyowapa ujasiri wananchi na kuwafanya waamini kuwa wana uwezo wa kupigana na Al-Shabaab," alisema Mbunge Abdimalik Abdalla, ambaye yuko katika wilaya ya Buulo-burde mkoani Hiran, moja ya maeneo ambapo vita vinaandaliwa.

Wanamgambo wa Al-shabab

Chanzo cha picha, AFP

Katika mahojiano na BBC alielezea sababu kwa nini watu sasa wanachukua silaha kupigana dhidi ya Al-Shabaab.

“Kwa kuwa wilaya hizi zimetengwa kwa muda wa miaka 13, wananchi wamechoka, wananchi wanataka maisha, watoto wao wameuawa, wameibiwa mifugo yao na inasemekana ‘ng’ombe’zao zilichukuliwa maasi yalipotokea.

Kilichotokea hapa ni uasi wa wenyewe kwa wenyewe unaoongozwa na serikali.

Alisema kuwa wana matumaini mazuri na wamefurahishwa na msaada wa serikali.

“Tumefurahishwa sana na uungwaji mkono wa serikali, na tunaamini kwamba wataongeza mengi,” alisema Mbunge Abdimaalik.

Aliondoa hofu kwa silaha zinazotumiwa na raia zinaweza kusababisha matatizo hata kama watashinda harakati hizo.

“Watu hawa walikuwa tayari wamejihami, na hakuna aliyekuwa tishio kwao, na hii haimaanishi kwamba serikali inawapa silaha wanamgambo au jamii fulani. Sio jamii moja inayopigana hapa, ni watu wa eneo hilo ambao wako tayari kujikomboa, na sidhani kama serikali itateseka ikiwa itasimama upande wao," alisema.

Akitaja oparesheni hizo kuwa ni nadra, Abdisalam alisema kuwa watu wana wasiwasi jinsi makabiliano hayo yatakavyoisha, huku wanahoji operesheni zinazoongozwa na wanamgambo wa kikabila zitaendelea hadi lini na iwapo wataendelea kutoa ulinzi.

"Watu wanajiuliza ikiwa hatua kama hii ingeweza kufanyika, kwa nini ilichukua muda wote huo?" alijiuliza.