Somalia na al-Shabab: Mapambano ya kuwashinda wanamgambo
Na Mary Harper
Mhariri wa Afrika, BBC World Service News

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika uteuzi wa kijasiri, serikali mpya ya Somalia imemjumuisha mwanamgambo wa zamani wa al-Shabab, ambaye wakati fulani alipigana dhidi ya mamlaka, katika baraza la mawaziri, lakini shambulio baya la hoteli mwishoni mwa juma ni ukumbusho wa kazi ngumu iliyo mbele ya wale walio madarakani.
Wakati Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alipoingia madarakani mwezi Mei alitangaza kipaumbele cha kwanza kuwa ni kukomesha uasi wa miaka 15 wa Kiislamu nchini humo.
Miezi mitatu baadaye al-Shabab walifanya moja ya mashambulizi yake ya kustaajabisha kuwahi kutokea, na kuvamia hoteli iliyokuwa umbali mfupi wa gari kutoka ikulu ya rais katika mji mkuu, Mogadishu.
Walishikilia mateka hoteli hiyo kwa saa 30. Maafisa walisema zaidi ya watu 20 walikufa katika shambulio hilo dhidi ya hoteli ya Hayat na 117 walijeruhiwa.
Chini ya mwezi mmoja mapema, kundi hilo lilianzisha uvamizi ambao haujawahi kushuhudiwa katika nchi jirani ya Ethiopia.
Ilikuwa ni kana kwamba walikuwa wakimzomea rais mpya.
Wanadiplomasia wa kimataifa wameelezea shambulio hilo tata, lililoratibiwa kama "badiliko la hali" ambalo lilichukua angalau miezi 18 kupanga na kuhusisha takriban wapiganaji 1,200.
Kamanda wa wakati huo wa Kamandi ya Marekani ya Afrika, Jenerali Stephen Townsend, alisema wanamgambo hao walipenya kilomita 150 (maili 93) ndani ya Ethiopia.
Sababu moja kwa nini kikundi kiliweza kufanya shambulio hili la kinyama ilikuwa kuongezeka kwa vita nchini Ethiopia baada ya miaka ya utulivu .
Muda mfupi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka katika eneo la kaskazini la Tigray mnamo Novemba 2020, mwanachama wa al-Shabab aliniita.
"Tunafurahia tamasha la Ethiopia ikijiangamiza," alifurahi. "Wakati wa kumpiga adui yetu mkuu hatimaye unakaribia."
Ethiopia ni mojawapo ya nchi katika eneo hilo ambayo imetuma wanajeshi wake nchini Somalia kusaidia serikali.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii ni mara ya pili kwa Rais Mohamud kuwa madarakani. Nilipomhoji muda mfupi baada ya kuanza kwa muhula wake wa kwanza mwaka wa 2012, alisema atawashinda wanamgambo ndani ya miaka miwili.
Miaka kumi baadaye, bado wanaendelea kuwa na nguvu.
Mwenyekiti wa kituo cha sera na fikra kuhusu usalama cha Hiraal chenye makao yake mjini Mogadishu, Mohamed Mubarak, anasema "wana nguvu zaidi na za kisasa kuliko walivyokuwa mwaka 2012".
Al-Shabab imeunda serikali sambamba na kudhibiti maeneo makubwa ya ardhi.
Inatoza ushuru kwa watu wa ndani na nje ya maeneo inayodhibiti. Hata wakazi wa Mogadishu wanapendelea kutumia mfumo wake wa utoaji haki, ambao wanauona kuwa wenye ufanisi zaidi na usio na rushwa kuliko mahakama rasmi.
Kundi hilo linaendelea kushambulia wapendavyo, likirusha kombora bungeni na katika uwanja wa ndege wa kimataifa wenye ngome nyingi ambao una makao ya balozi, Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa kigeni.
Si ajabu kwamba al-Shabab imeelezewa kuwa mshirika wa al-Qaeda wenye mafanikio zaidi.
Rais Mohamud anakubali kwamba al-Shabab haiwezi kushindwa kwa nguvu za kijeshi pekee.
Mnamo tarehe 2 Agosti, serikali ilichukua hatua inayoweza kuchukuliwa kama kamari ya ujasiri ya kuleta mmoja wa maadui wake wa zamani kama sehemu ya mkakati mpya wa kumaliza mzozo huo.
Nilikuwa Mogadishu wakati huo, kwenye gari na marafiki waliokuwa wamekwama kwenye kizuizi cha barabarani.
Kwa mara moja, hakuna mtu ambaye alikuwa na wasiwasi hata kidogo kuhusu kuamriwa kutoka kwenye gari au watu kupekuliwa.
Tulipokuwa tukingoja kwenye sehemu ndogo tu ya kivuli tuliyoweza kupata, tuliingia katika hali ya mawazo, macho yakiwa yamebaki kwenye simu zetu za mkononi huku tukimtazama msemaji wa waziri mkuu akitangaza baraza jipya la mawaziri.
Jina tulilokuwa tukingojea lilikuwa la mwanachama mwanzilishi wa al-Shabab, aliyefunzwa nchini Afghanistan.
Uvumi huo uligeuka kuwa kweli.

Chanzo cha picha, AFP
Aliyekuwa naibu kiongozi na msemaji wa Al-Shabab, Mukhtar Robow, aliteuliwa kuwa waziri wa masuala ya kidini.
Huku wengine wakichukizwa na hatua hiyo, Wasomali wengi wamepokea kwa shauku kuingia serikalini kwa mwanamume ambaye aliwahi kuwa kwenye orodha ya Marekani ya magaidi wanaosakwa zaidi na zawadi ya $5m (£4.2m) kichwani mwake.
Wanajumuisha mbunge na mwandishi wa zamani wa BBC Moalimuu Mohamed ambaye ana makovu ya kunaswa katika mashambulizi matano ya al-Shabab. Shambulio lililolengwa la kujitoa mhanga mapema mwaka huu lilimwacha akipigania maisha yake.
"Nakaribisha uteuzi wa Bw Robow," asema Bw Mohamed.
"Kama kiongozi wa zamani wa kijihadi atachangia sana katika vita dhidi ya al-Shabab. Anaweza kufanya kazi na jumuiya ya kidini kupinga itikadi kali na kuwashawishi wapiganaji kwamba imani zao hazifuati njia ya kweli ya Uislamu."
Bw Robow alitofautiana na al-Shabab mwaka wa 2013. Alikashifu kundi hilo hadharani, hata kuchangia damu kwa ajili ya wahasiriwa wa shambulio kubwa la bomu la lori mjini Mogadishu Oktoba 2017 ambalo liliua karibu watu 600.
Alizuiliwa mnamo Desemba 2018 na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani hadi alipotajwa kama waziri wa serikali. Alisema alipokea simu akiwa kizuizini.
Mtaalamu wa usalama, Bw Mubarak, anaelezea uteuzi wa Bw Robow kama "wazo zuri kutoka kwa mtazamo wa kukabiliana na ugaidi".

Chanzo cha picha, Reuters
"Yeye ni chombo chenye nguvu, hasa katika suala la itikadi, kwani atatoa msukumo mkali wa kimafundisho dhidi ya al-Shabab. Kama mwanachama mwanzilishi wa kikundi hicho anawajua kwa ndani. Anajua jinsi wanavyofikiri na jinsi wanavyotenda."
Wengine wameitikia kwa hofu kuteuliwa kwa Bw Robow na kuiona kama ishara nyingine ya kutokujali ambayo imeashiria mgogoro wa zaidi ya miongo mitatu nchini Somalia.
Mitandao ya kijamii imepamba moto na ukosoaji. Matamshi mengi kwenye Twitter yalikuwa ya chuki:
"Kama Somalia ingekuwa jumuiya inayofanya kazi, Robow angenyongwa hadharani."
"Kuteuliwa kwa muuaji huyu katili kunamaanisha jambo moja tu: Al-Shabab wamejipenyeza rasmi katika serikali ya Somalia."

Al-Shabab inaamini kwamba kukubali kwa naibu kiongozi wake wa zamani kazi ya serikali ni uhalifu wa kutisha, unaostahili adhabu ya mwisho.
Katika taarifa iliyorekodiwa ya dakika 10 msemaji wa kundi hilo, Ali Dheere, alisema "Robow ni muasi dini . Kumwaga damu yake kunaruhusiwa."
Rais Mohamud anaamini kuteuliwa kwake pamoja na mashambulizi mapya ya kijeshi kutaidhoofisha al-Shabab vya kutosha kuilazimisha kufanya mazungumzo.
"Yote inategemea nia ya kisiasa," anasema Bw Mubarak.
"Kuanguka kwa al-Shabab kutakuja tu ikiwa Umoja wa Afrika na vikosi vingine vya kigeni, wanajeshi wa shirikisho na wa kikanda, na wanamgambo wa ndani wote wataungana. Hapo ndipo watakapojadiliana na kufanya maafikiano."
Mwanamgambo aliyegeuka kuwa waziri Bw Robow sasa anazungumza kuhusu amani na msamaha. Anasema atashirikiana na wanazuoni wa Kiislamu kuwashawishi watu kuachana na al-Shabab kwa kuwaaminisha kwamba wanachofanya si Uislamu.
Lakini haijulikani kama kamari ya serikali italipa, au itaimarisha tu azimio la al-Shabab kupigana zaidi kuliko hapo awali.
Matukio ya hivi majuzi yanapendekeza kuwa watachugua la mwisho















