Urusi-Ukraine: Nani ameitungua ndege ya Urusi iliyokuwa na wafungwa wa kivita?

Chanzo cha picha, Reuters
Kuna vita vya kurushiana risasi na kuna vita vya taarifa. Nchi zinazopigana zinapigana vita vyote viwili. Hilo linaweza kupelekea kuupata ukweli likawa jambo gumu.
Ripoti juu ya ndege aina ya Il-76 kuanguka zilionekana kwanza kwenye mashirika ya habari ya serikali ya Urusi.
Waliinukuu Wizara ya Ulinzi ya Moscow ikidai makumi ya wafungwa wa kivita wa Ukraine walikuwa kwenye ndege, wakielekea kwenye eneo la kubadilishana wafungwa.
Kyiv haikuthibitisha hilo na hakukuwa na ushahidi kutoka Urusi.
Mbunge wa Urusi, Andrei Kartapolov, alianza kuipanua taarifa hiyo na kudai Ukraine inaweza kuwa ilitumia kombora la Patriot kuipiga ndege ya Ilyushin.
Hiyo ingemaanisha silaha inayotolewa na nchi za Magharibi imetumika kupiga ndege. Haya ni madai makubwa, ambayo bado hakuna ushahidi wa kuyaunga mkono.
Huko Kyiv, tulianza kusikia uvumi kwamba ubadilishaji wa wafungwa umepangwa kufanyika leo. Lakini hakuna mtu wa Kyiv alisema hilo rasmi.
Kila tuliyempigia simu atupe maelezo alituambia, "bado" au "tunafuatilia taarifa" au "subiri." Kwa saa nane, hapakuwa na taarifa rasmi.
Ukraine ilihusika?

Tovuti ya habari ya Ukrainska Pravda ilinukuu chanzo cha kijeshi kikisema ni "kazi yao," na ndege hiyo ilikuwa imebeba makombora ya S300 ya Urusi.
Baadaye taarifa hilo ilirekebishwa na kusema chanzo hicho kilikuwa hakijathibitishwa.
Hatimaye jioni tulipata taarifa mbili rasmi. Ya Jenerali wa Jeshi na kutoka Idara ya Ujasusi ya Kijeshi ya Ukraine, kwa pamoja wanakubali kwamba huenda Ukraine imeidungua ndege hiyo - ingawa hakuna aliyesema hivyo moja kwa moja.
Ukraine inasisitiza haina taarifa za kuaminika kuhusu nani aliyekuwa kwenye ndege. Lakini ilithibitisha ubadilishaji wa wafungwa ulipangwa Jumatano na haukufanyika.
Pia, ilisema kwa kawaida Urusi hutoa maelezo kuhusu njia na usafiri utakaotumika kubadilishana wafungwa, ili kuhakikisha kuwa ni salama.
Wakati huu, Ukraine inasema, maelezo ya aina hiyo hayakutolewa.
Zelensky ailaumu Urusi

Chanzo cha picha, 77
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameishutumu Moscow kwa "kuchezea maisha ya wafungwa wa Ukraine", baada ya ajali hiyo iliyotokea magharibi mwa Urusi.
Ametaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike baada ya ajali ya Jumatano katika eneo la Belgorod karibu na mpaka wa Ukraine.
Urusi ilisema hakuna mtu aliyenusurika baada ya Kyiv kuangusha ndege ya Il-76 iliyokuwa na wafungwa 65 wa vita wa Ukraine, wafanyakazi sita wa Urusi na wasindikizaji watatu.
Idara ya kijasusi ya kijeshi ya Ukraine ilisema haijaambiwa ili kuhakikisha kuna usalama wa anga kama ilivyokuwa katika matukio yaliyopita.
Katika hotuba yake ya video siku ya Jumatano, Rais Zelensky alisema "ni dhahiri kwamba Warusi wanacheza na maisha ya wafungwa wa Ukraine."
Zelensky – ambaye amesitisha safari ya kikanda inayokwenda sanjari na siku yake ya kuzaliwa siku ya Alhamisi - alisisitiza "ukweli wote wazi lazima ubainishwe."
Maoni ya idara ya kijasusi ya kijeshi ya Ukraine mapema siku hiyo yalionekana kama kukiri kimyakimya kwamba iliidungua ndege hiyo ya kijeshi, ingawa ilisisitiza haikuwa na taarifa za kuaminika kuhusu nani alikuwa ndani ya ndege hiyo.
Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha ndege ikianguka na kufuatiwa na mlipuko na moto karibu na kijiji cha Yablonovo, kilomita 70 kaskazini-mashariki mwa jiji la Belgorod, saa 11:00 kwa saa za huko (08:00 GMT).
Gavana wa mkoa wa Belgorod Vyacheslav Gladkov alisema ndege hiyo ilianguka kwenye uwanja karibu na makazi ya watu na skila mtu aliyekuwemo alikufa.
Kabla ya mpango wa kubadilishana wafungwa, maafisa wa Ukraine walisema wanajeshi wa Urusi waliokamatwa "walifikishwa eneo lililokubaliwa kwa wakati ili kubadilishwa, na walikuwa salama."
Wizara ya Ulinzi ya Urusi, ilisema ndege hiyo ilipaa kutoka kambi ya anga ya Chkalovsky kaskazini-mashariki mwa Moscow ikielekea Belgorod, ikidai jeshi la anga la Ukraine lilirusha makombora mawili ya kutungulia ndege kutoka eneo la Lyptsi kusini mwa mpaka wa Ukraine.
Mabadilishano makubwa zaidi ya wafungwa tangu kuanza kwa vita yalifanyika mapema mwezi huu, wakati Ukraine ilipowaachia huru wafungwa 248 wa kivita wa Urusi na Urusi kuwaachilia huru watu 230 katika makubaliano yaliyopatanishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu .
Zaidi ya Waukraine 8,000, raia na wanajeshi, bado wanashikiliwa na Urusi, kulingana na Ukraine inasema makumi ya maelfu ya wengine bado hawajulikani walipo.
Mashambulizi yaongezeka

Mji wa Belgorod uko takriban maili 25 (40km) kaskazini mwa mpaka na Ukraine, umekumbwa na maelfu ya majeruhi kutokana na mashambulizi ya anga na ndege zisizo na rubani tangu vita vya Ukraine kuanza.
Vita vya Urusi nchini Ukraine vinaendelea huku vikikaribia mwaka wake wa tatu.
Wiki iliyopita, Urusi ilidai kuteka kijiji kilicho karibu na mji ulioharibiwa wa Bakhmut, katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine. Kyiv haijathibitisha madai hayo.
Wakati huo huo, mashambulizi ya anga ya Urusi yameongezeka katika wiki za hivi karibuni. Siku ya Jumanne, watu 18 waliuawa na 130 walijeruhiwa katika mashambulizi ya makombora katika miji ya Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov ameonya kuwa wakati wanajeshi wa Ukraine wakikabiliwa na uhaba wa silaha, Urusi imetumia zaidi ya makombora 600 na ndege zisizo na rubani zaidi ya 1,000 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Kwa upande wake, Ukraine inapigana zaidi kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Mwishoni mwa juma, shambulio la ndege zisizo na rubani lilisababisha mlipuko katika kituo kikuu cha usafirishaji wa gesi karibu na jiji la St Petersburg.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












