Kwa nini unapaswa kulala wakati huo huo kwa wiki nzima?

Chanzo cha picha, Getty Images
Tofauti ndogo ya mazoea ya kulala kati ya siku za kazi na siku za kupumzika kunaweza kusababisha mabadiliko yasiyofaa kwa bakteria kwenye matumbo yetu, utafiti unaeleza.
Kwa mujibu wa utafiti wa karibu watu wazima 1,000 uliofanywa na wanasayansi wa Chuo cha King London, unasema ratiba za kulała zilizovurugika, haswa kutokana na kazi, zinaleta athari kwa afya.
Kuweka nyakati za kulala na nyakati za kuamka zifanane na kula mlo kamili kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa.
Kuna aina mbalimbali za bakteria katika mfumo wa usagaji chakula. Baadhi ni bora zaidi kuliko wengine, lakini kupata mchanganyiko sahihi ni muhimu ili kuzuia magonjwa.
"Mabadiliko ya nyakati za kulała yanaweza kuzusha viumbe vidogo vidogo ambavyo vina uhusiano usiofaa na afya yako," anasema Kate Bermingham, mwandishi wa utafiti na mtaalamu wa lishe katika kampuni ya sayansi ya afya ya Zoe.
Kulala na kuamka nyakati tofauti wakati wa wiki, ikilinganishwa na wikendi, kunadhaniwa kuathiri zaidi ya 40% ya idadi ya watu wa Uingereza, utafiti unasema, na ni kawaida kwa vijana na kisha hupungua kadri tunavyozeeka.
Washiriki wa Utafiti
Washiriki wa utafiti huu, uliochapishwa na Jarida la European Journal of Nutrition, walichunguza usingizi na damu. Sampuli za kinyesi zilikusanywa na kurekodi kila kitu walichokula katika dodoso la chakula.
Wale ambao hubadilisha nyakati za kulala kwa 16% wana uwezekano wa kula chakula kilichojaa viazi, ikiwa ni pamoja na makwaru na chips, pamoja na vinywaji vya sukari, na matunda na karanga.
Utafiti wa awali ulionyesha watu wanaobadilisha nyakati za kulała hula vyakula kidogo vya nyuzinyuzi kuliko wale ambao nyakati zao za kulała hazibadiliki. Tafiti nyigine ziligundua watu wanaobadili muda wa kulala hupata uzito, magonjwa na uchovu wa akili.
Watafiti waligundua spishi tatu kati ya sita za viumbe vidogo vidogo zilikuwa nyingi zaidi kwenye matumbo ya watu wanaobadili nyakati za kulała. Vilevile wanahusishwa na lishe duni, kunenepa, viwango vya juu vya maambukizi na hatari ya kiharusi.
"Kudumisha utamaduni wa kulała wakati huo huo na kuamka, ni tabia inayoweza kufuatwa kwa urahisi," anasema Dk Sarah Berry, wa Chuo cha Kikuu cha King London.
Lishe yenye afya ni ipi?
Tovuti ya NHS inapendekeza:
• Kula angalau aina tano za matunda na mboga kila siku
• Weka matunda na mbogamboga kwenye vyakula vyenye wanga nyingi kama vile viazi, mkate, wali au tambi
• Kula vyakula mbadala vya maziwa au kunywa maziwa yenyewe, na kula vyakula vyenye sukari au mafuta kidog inapowezekana
• Kula maharagwe, kunde, samaki, mayai, nyama na protini nyingine
• Kunywa maji mengi (angalau glasi sita hadi nane kwa siku).












