Daktari, fundi cherehani, na Bi harusi mtarajiwa: Simulizi za waliouawa huko Gaza

- Author, Ethar Shalaby
- Nafasi, BBC Arabic
Idadi ya watu waliofariki Gaza inaongezeka huku Israel ikiendelea na vita vyake dhidi ya Hamas, kufuatia mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba ambapo watu 1,400 waliuawa nchini Israel.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza inasema zaidi ya watu 9,000 wameuawa tangu vita kuanza.
Kwa sababu ya hofu ya usalama, kuna waandishi wa habari wachache huko Gaza kuangazia athari ya kibinadamu ya mapigano.
Lakini BBC imekuwa ikizungumza na familia kadhaa na watu walioshuhudia tukio hilo ambao wametusimulia hadithi za wapendwa wao ambao wameuawa katika siku za hivi karibuni.
Yusof Abu Mousa

Pamoja na matatizo makubwa ya usambazaji wa umeme katika Ukanda wa Gaza, Yusof na kaka zake wawili wakubwa - dada Jury, 13, na kaka wa miaka tisa Hamed - walihisi kuwa na bahati sana.
Baba yao, Mohamed Abu Musa, mtaalamu wa matibabu katika hospitali ya Nasser katika jiji la Khan Younis, alikuwa ameweka sola nyumbani kwao, ili watoto waweze kutazama katuni wanazozipenda zaidi kwenye TV.
Walikuwa wakitulia mbele ya televisheni tarehe 15 Oktoba wakati, baba yao anasema, nyumba yao ilikumbwa na shambulio la anga la Israel.
Jury na Hamed walinusurika kimiujiza, lakini Yusof aliuawa wakati paa la nyumba yao lilipoporomoka.
Alikuwa na umri wa miaka saba.
Mohamed alikuwa akifanya zamu ya saa 24 hospitalini wakati mke wake, Rawan, alipoingia, akipiga kelele kumtafuta mwana wao mdogo.
Alikuwa amempata Hamed, wakati waokoaji waliposaidia kumtoa Jury kwenye vifusi. Jury alikuwa amepata majeraha ya kichwa lakini wazazi wake wanasema "hali yake inaimarika".
Video inayoonyesha Rawan akimuulizia hospitalini "mwanawe mrembo na mwenye nywele zilizopinda" ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii. Lakini baadaye Mohamed angepata mwili wa mwanawe katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
"Mara ya mwisho nilipomuona Yusof akiwa hai ni wakati alipokimbia kunikumbatia kwenye mlango wa nyumba yetu, muda mfupi kabla nitoke kwenda kazini," Mohamed anakumbuka.
"Alinibusu na kuniaga baada ya kumpa biskuti na ndizi, alitaka kuwa daktari labda kwa sababu alikuwa akiniona nikienda hospitali kwa ajili ya kazi."
Dkt Midhat Saidam

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jioni ya Oktoba 15, Dk Saidam alihitaji kupumzika. Daktari huyo wa upasuaji mwenye umri wa miaka 47 hakuwa ameondoka katika hospitali ya al-Shifa, katika Jiji la Gaza kwa zaidi ya wiki.
Aliwaambia wenzake kuwa anaenda nyumbani kwa usiku huo. Lakini saa chache baadaye aliuawa katika shambuli la Israel nyumbani kwake.
"Mtu huyu mtulivu, mcheshi na mwenye moyo mkunjufu alirejea hospitalini asubuhi iliyofuata, lakini akiwa hana uhai," mwenzake Dkt Adnan Albursh alieleza.
Dk Albursh, ambaye alikuwa amemfahamu daktari huyo wa upasuaji kwa zaidi ya miaka 20, aliongeza kuwa marehemu alipewa jina la utani la "mpasuaji asiyechoka" na wenzake kutokana na jinsi alivyojitolea katika kazi hiyo.
Dk Saidam pia alijulikana kama mshauri mkubwa kwa madaktari wadogo.
"Iwapo mmoja wa madaktari alikabiliwa na matatizo yoyote, walijua Dkt Saidam ndiye angesuluhisha," aliongeza Dkt Ahmed El Mokhallalati, mkuu wa idara ya upasuaji wa plastiki katika Hospitali ya al-Shifa.
"Kifo chake ni pigo kubwa sio tu kwa hospitali hii bali pia kwa taaluma ya matibabu," aliongeza.
Nour Yousef al-Kharma

Mwanafunzi Nour mwenye umri wa miaka 17 aliuawa tarehe 11 Oktoba wakati mashambulizi ya angani ya Israel yalipopiga nyumba ya familia yake katika mji wa Deir al-Balah, kilomita 14 kusini mwa mji wa Gaza, kulingana na mjomba wake.
Mohammed al-Kharma alisema mpwa wake alitaka kuhama kwa sababu ya kuhofia mashambulio hayo na kuishi na jamaa zake mahali pengine.
"Baba yake alimsihi baki katika nyumba yake, lakini ililipuliwa asubuhi iliyofuata. Ilikuwa hatima yake," alisema.
Nour aliuawa pamoja na mpwa wake Yazan. Wawili hao walikuwa wakicheza sebuleni. Dada zake wakubwa, Ola, na Huda, waliokuwa wakitayarisha kifungua kinywa pamoja na mama yao, Jamalat, waliokoka.
Nour alikuwa katika mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili na alitaka kuwa daktari. Mjombake alisema familia yake ilipata begi lake la shule chini ya vifusi. Ilikuwa na vitabu na shajara, na katika mojawapo wa kurasa alikuwa ameandika: "Nataka kuifanya familia yangu ijivunie na nitapata alama za juu kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu."
Lurin Azzam Abuhalima

Katika mawasiliano yake ya mwisho na mchumba wake Khaled al-Masry, Lurin alisema alikuwa amechoka kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta usalama. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwa amewasili tu katika kambi ya wakimbizi ya Nusairat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, kukaa na shangazi yake.
Lurin alikuwa amenusurika mashambulizi mawili, ikiwa ni pamoja na moja ya tarehe 16 Oktoba ambayo iligonga jengo aliyokuwa akiishi na wazazi wake katika Jiji la Gaza.
"Aliniambia anataka kuoga, asali na kupumzika," Khaled anakumbuka.
Kulingana na mchumba wake, anayeishi na kufanya kazi huko Cyprus, alikuwa akisali katika chumba wakati nyumba yao iliposhambuliwa.
"Aliuawa alipokuwa akisali," anasema.
Lurin na Khaled walikuwa wameahirisha harusi yao mara kadhaa kutokana na hali ya wasiwasi huko Gaza.
Hatimaye walikuwa wakipanga kufunga ndoa mwezi wa Disemba na kuhamia Cyprus.
Khaled aliyekuwaka na huzuni alisema: "Sasa amepumzika milele. Alikuwa akipenda kuvaa nguo nyeupe, lakini sasa amevaa sanda nyeupe."
Fekriya Hassan Abdul A'al

Wakazi wa Wilaya ya Radwan katika jiji la Gaza ambao walihitaji mavazi rasmi ya wanawake wangeelekea moja kwa moja hadi kwa Fekriya Hassan Abdul A'al.
"Nakumbuka na nyumba yetu ilivyojaa mabibi-harusi na mabibi harusi ambao walikuja nyumbani kwa mama yangu kupima gauni. Alikuwa na kipaji cha kipekee," binti ya Fekriya, Nevine anasema.
Fundi cherehani huyo mwenye umri wa miaka 65 aliuawa pamoja na ndugu zake wawili, watoto wake wawili na wajukuu zake wawili, baada ya nyumba walimokuwa wakijificha kulipuliwa katika shambulio la anga tarehe 23 Oktoba.
Nevine, ambaye alikuwa akijificha kwenye nyumba ya rafiki yake, anasema kwamba Fekriya alikuwa amejitolea kwa familia yake na alikuwa akiandaa tafrija ya kila wiki. Lakini Nevine anasema aliathiriwa sana na kuongezeka kwa mzozo huo: "Aliniambia katika mawasiliano yetu ya mwisho yasimu: 'Sina furaha moyoni na nimechoka kutokana na kile kinachoonekana kuwa vita visivyoisha'."
Mazen na Ahmed Abu Assi

Ndugu Mazen, 17 na Ahmed, 13 walikuwa miongoni mwa waliouawa kwenye mlipuko katika Hospitali ya al-Ahli tarehe 17 Oktoba.
Maafisa wa Palestina wanasema mlipuko huo ulisababishwa na shambulio la anga la Israel. Lakini jeshi la Israel linasema ulisababishwa na roketi iliyofeli iliyorushwa na kundi la Kipalestina la Islamic Jihad - tuhuma ambayo kundi hilo liliipinga.
Arafat Abu Massi, baba yake Mazen na Ahmed, alisema ndugu hao wawili "walikuwa karibu sana" lakini walikuwa na haiba tofauti.
Arafat na mke wake walikuwa wamepitia matibabu ya IVF kwa miaka minane ili kumpata Mazen, ambaye alikuwa katika shule ya upili alitaka kuwa daktari wa meno. "Alikuwa mkali zaidi ya watoto wangu wote," anasema. Wakati Ahmed alielezewa na baba yake kama "mwenye nguvu na shujaa zaidi katika familia" - na mjasiriamali.

"Alikuwa akiuza vinyago na vifaa vya shule katika kibanda kidogo karibu na nyumba yetu," Arafat alisema.
Mtoto pekee aliyebaki sasa ni Faraj mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye kwa mujibu wa Arafat, anaendelea kulia na kuuliza ndugu zake wako wapi. "Nilimwambia kwamba Mungu amewachagua wakae mbinguni. Hapo ni mahali pazuri zaidi kwa wanangu wangu wawili wenye akili."
Salam Mema

Salam Mema, mwandishi wa habari wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 32, aliuawa tarehe 10 Oktoba wakati nyumba yake huko Jabaliya, kaskazini mwa Gaza, ilipogongwa katika mashambulizi ya anga ya Israel, rafiki yake aliambia BBC.
Mumewe, binti yao Sham mwenye umri wa miaka miwili, mtoto wao Hadi mwenye umri wa miaka saba, na watu wengine wa familia hiyo, pia waliuawa, na kumwacha mtoto wao wa kiume Ali mwenye umri wa miaka mitano aliyenusurika.
Kufikia tarehe 31 Oktoba, Salam alikuwa mmoja wa waandishi wa habari 31 waliothibitishwa kuuawa pande zote mbili, tangu mzozo wa Israel na Hamas uanze.
Safaa Nezar Hassouna

Mfamasia huyo mwenye umri wa miaka 26 aliuawa katika shambulio la anga katika mji wa kusini wa Rafah, tarehe 17 Oktoba.
Alikuwa amelala kando ya mtoto wake wa kike wa miezi mitatu, Elyana, na mumewe.
Mjomba wa Safaa na daktari mstaafu anayeishi Uingereza, Omar Hassouna, alisema wazazi wake walinusurika shambulio hilo lakini wameshtushwa na kuhuzunishwa na kifo chake.
Omar alisema mara ya mwisho alimuona mpwa wake ilikuwa Januari, wakati alipoenda likizo yake huko Gaza. "Safaa ilikuwa na nidhamu, alipenda kusaidia, na alipendwa na kila mtu.
"Nimempoteza mpwa mzuri. Kifo chake hakikuwa cha haki, sawa na vifo vingine vyote vya raia huko Gaza ."
"Ningependelea kuwa pamoja nao Gaza, ninahisi kukosa matumaini hapa nilipo."












