Je, simu yako inaweza kulipuka ukiichaji usiku kucha?

    • Author, Muhammad Sahib
    • Nafasi, BBC

Wakili Usman Khan Yousafzai alikuwepo katika mahakama ya Islamabad siku ya Jumatatu wakati moshi ulipoanza kupanda ghafla kutoka kwenye koti lake.

Kwa kuona hatari hiyo, akalitupa koti na papo hapo simu iliyokuwa ndani ikateketea kwa moto.

Katika video iliyorekodiwa nje ya mahakama, wakili Usman Khan alielezea sababu ya kulipuka kwa betri ya simu yake kuwa ni kutokana na kuiweka chaji usiku kucha.

Anasema, ''niliweka simu yangu kwenye chaji usiku kabla ya kulala na kisha kuiondoa asubuhi, labda ndiyo sababu ya kulipuka.''

Usman alikuwa na simu ya kampuni ya simu za Samsung na kumekuwa na matukio ya milipuko ya betri kwa simu hizi siku za nyuma.

Aina ya simu aliyoitaja hutumia betri za lithiamu-polymer ambayo ni salama zaidi kuliko betri zenye utata za lithiamu-ioni zilizokuwa zikitumiwa hapo awali katika simu hizi.

Hii ndiyo sababu makampuni ya simu duniani kote yalianza kutumia betri za lithiamu polymer.

Mapema mwaka 2020, akizungumza na gazeti la The Daily Mail, mkazi wa California alidai betri ya simu yake ililipuka ghafla na simu ya Samsung iliteketea kabisa.

Baada ya video ya kulipuka kwa simu ya mwanasheria wa Islamabad kusambaa, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wanauliza swali: Je, ni hatari kuacha simu katika chaji usiku kucha?

Pia unaweza kusoma

Je, simu hazipaswi kuachwa katika chaji usiku kucha?

Kwa mujibu wa jarida la sayansi na teknolojia la 'The Conversation' simu nyingi za sasa hujaa chaji chini ya dakika 30.

Muda unaohitajika kuchaji pia unategemea na uwezo wa betri ya simu na ni kiasi gani cha nishati inayotolewa na chaja yako.

Kuiacha simu kwenye chaji usiku kucha si jambo la lazima na pia husababisha uwezo wa betri ya simu yako kupungua kwa kasi, hivyo hudhoofisha betri ya simu.

Wataalamu wanashauri kuepuka kuchaji simu kutoka sifuri hadi asilimia 100 (yaani kuchaji betri ya simu hadi asilimia 100 kwa mara moja). Mwongozo wa Samsung unasema kuchaji simu hadi asilimia 100 mara nyingi kunaweza kudhuru afya ya betri ya simu yako.

Kwa mujibu wa wataalamu, ni bora kuchaji simu kati ya asilimia 20 na 80 kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuna uwezekano mdogo wa simu kulipuka kwa kuichaji muda mrefu. Bali hulipuka kutokana na kasoro nyingine katika betri.

Kwa kawaida, kebo yenye hitilafu wakati wa kuchaji au betri kutoweza kumudu joto kunaweza kusababisha kulipuka.

Profesa Clare Gray, mtaalamu wa nishati katika Chuo Kikuu cha Cambridge, aliambia BBC kuwa makosa madogo yanaweza kusababisha betri kulipuka, kama vile chuma kilichoachwa kwa bahati mbaya kwenye betri.

Pia unaweza kusoma

Tahadhari za Kuchukua

Baadhi ya hatua zinaweza kuifanya betri ya simu yako kufanya kazi kwa muda mrefu na pia inaweza kusaidia kukulinda kutokana na ajali inayoweza kutokea.

Hakikisha programu za simu yako hazijapitiwa na wakati.

Tumia chaja ya asili au zilizoidhinishwa za simu kwani chaja zingine zinaweza kuwa na namna tofauti ya kupeleka moto.

Weka simu mbali na joto kali na baridi kali sana. Digrii sifuri hadi digrii 35 ni hali joto inayofaa. Weka simu yako chaji ifike kati ya asilimia 20 hadi 80 na usichaji simu hadi asilimia 100.

Usiache simu yako ikichaji usiku kucha na ikiwa betri imejaa iondoe kwenye chaji mara moja. Fuatilia betri yako ili kuona kama inaisha chaji haraka.

Iwapo unahisi simu yako inapata joto au betri imevimba, ipeleke kwenye duka lenye beteri za kampuni ya simu yako kwa ajili ya kununua betri mpya.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga