Kipi kinatishia 'kufeli' kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani

Muda wa kusoma: Dakika 5

Iran na Marekani zimefanya duru ya pili ya mazungumzo ya hali ya juu ya nyuklia mjini Roma - na kukubaliana kukutana tena wiki ijayo - hata kama matumaini ya kumaliza tofauti zao yanaendelea kudidimia kutokana na vitisho vya kijeshi vinavyoongezeka na ujumbe mchanganyiko.

Rais wa Marekani Donald Trump anaikumbusha Iran karibu kila siku machaguo yaliyopo: kufikia makubaliano au vita.

Hapo awali alisema Israel itaongoza hatua ya kijeshi ikiwa mazungumzo hayo yatashindwa.

Siku ya Jumatano, gazeti la New York Times liliripoti kwamba Trump "amepuuza" mpango wa Israel wa kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran mapema mwezi ujao.

"Singesema kuwa ni kutupiliwa mbali hatua hiyo. Sina haraka ya kufanya hivyo," Trump aliwaambia waandishi wa habari akijibu makala ya siku ya Alhamisi, akiongeza kuwa alipendelea kutoa fursa ya diplomasia kufuatwa.

"Nadhani Iran ina nafasi ya kuwa nchi bora na kuishi kwa furaha bila vifo... Hilo ni chaguo langu la kwanza. Ikiwa kuna chaguo la pili, nadhani hali itakuwa mbaya zaidi kwa Iran."

Baada ya pande zote mbili kuelezea duru ya kwanza ya mazungumzo ya Oman wikendi iliyopita kuwa yenye tija, Trump alisema "atafanya uamuzi juu ya Iran haraka sana".

Kwa nini Iran ilirudi kwenye meza ya mazungumzo

Mnamo mwaka wa 2018, Trump aliiondoa Marekani kutoka kwa makubaliano ya mwaka 2015 ambayo yaliifanya Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia na kuruhusu ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ili iweze kuondolewa vikwazo.

Alisema hatua hiyo ilichangia padogo mno katika kuzuia Iran kujikita kwenye silaha ya nyuklia na akarejesha vikwazo vya Marekani kama sehemu ya kampeni ya "shinikizo la juu" ili kuilazimisha Iran kujadili makubaliano mapya.

Hata hivyo, Iran ilikataa na kuzidi kukiuka vikwazo ilivyowekewa kama njia ya kulipiza kisasi. Sasa imekusanya madini ya uranium iliyorutubishwa vya kutosha kutengeneza mabomu kadhaa ikiwa itachagua kufanya hivyo - jambo ambalo inasema haitafanya kamwe.

Soma zaidi:

Tishio la kutekeleza hatua ya kijeshi inaonekana kuchangia katika kuirejesha Iran kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo inasisitiza kwamba sio sababu.

Tovuti ya Kiongozi Muadhamu, Ayatollah Ali Khamenei, ilisema Iran imekubali kufanya mazungumzo kwa sababu tu Marekani iliwekea mipaka matakwa yake katika masuala ya nyuklia - si kwa kuhofia mashambulizi ya Marekani na Israel.

Hata hivyo, kufikia makubaliano ni hatua ambayo bado iko mbali isio na uhakika.

Mjumbe Maalum wa Trump katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff, ambaye anaongoza timu ya mazungumzo ya Marekani, aliweka ujumbe kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne: "Mpango wowote wa mwisho lazima utengeneze mfumo utakaolenga kuleta amani, utulivu na ustawi katika Mashariki ya Kati - ikimaanisha kuwa Iran lazima isitishe na kuachana kabisa na mpango wake wa kurutubisha nyuklia na silaha."

Hili lilijitokeza siku moja tu baada ya kupendekeza katika mahojiano na Fox News kwamba Iran itaruhusiwa kuendelea kurutubisha madini ya uranium.

"Haihitajiki kurutubisha zaidi ya 3.67%," alisema, akimaanisha ukomo uliowekwa na makubaliano ya nyuklia ya 2015.

"Hii itahusu zaidi uthibitishaji kwenye mpango wa urutubishaji na hatimaye uthibitisho wa utumiaji silaha."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mkuu wa ujumbe wa Iran, alijibu kwa kuashiria "kauli zinazokinzana" za Witkoff na kusisitiza kwamba "misimamo halisi itawekwa wazi katika meza ya mazungumzo".

"Tuko tayari kujenga imani kuhusu wasiwasi unaowezekana kuwepo juu ya mpango wa urutubishaji wa Iran, lakini kanuni ya kurutubisha sio suala la kujadiliwa," alisema.

Mfululizo wa shughuli za kidiplomasia

Mazungumzo ya Jumamosi mjini Roma yalifanyika huku kukiwa na msururu wa shughuli nyingi za kidiplomasia.

Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Prince Khalid bin Salman, alitembelea Tehran siku ya Alhamisi, na kutoa ujumbe wa kibinafsi kutoka kwa baba yake Mfalme Salman kwa Ayatollah Khamenei. Pia alikutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Iran imeonya kwamba hatua zozote za kijeshi za Marekani zitakabiliwa na ulipizaji kisasi dhidi ya kambi za Wamarekani katika eneo hilo - nyingi zikiwa zimeandaliwa na majirani wa Kiarabu wa Iran.

Wakati huo huo, Araghchi alitembelea Moscow na kukabidhi barua kutoka kwa Khamenei kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Iran na Urusi zimeimarisha uhusiano wao wa kijeshi tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, huku Tehran ikishutumiwa kusambaza ndege zisizo na rubani kusaidia juhudi za vita vya Moscow.

Bunge la Urusi liliidhinisha ushirikiano wa kimkakati wa miaka 20 kati ya Iran na Urusi siku 10 zilizopita. Hata hivyo, mpango huo haujumuishi kifungu cha ulinzi wa pande zote.

Wakati huo huo, mkuu wa IAEA Rafael Grossi alikamilisha ziara ya siku mbili mjini Tehran wiki hii, kukutana na maafisa wa nyuklia wa Iran na waziri wa mambo ya nje katika jitihada za kupunguza mvutano na kurejesha itifaki za ukaguzi.

Mazingira ya kutoaminiana

Tangu Trump arudi ofisini mwaka huu, Ayatollah Khamenei amekuwa akikashifu mazungumzo na Washington.

"Kujadiliana na utawala huu si jambo la kimantiki, si jambo la busara, wala si jambo la heshima," alisema katika hotuba yake ya Februari, miezi miwili tu kabla ya kukubaliana kuingia kwenye duru ya sasa ya mazungumzo.

Kutokuwa na imani kwa kiongozi huyo mkuu kunatokana na Trump kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia, kampeni ya "shinikizo la juu" iliyofuata, na mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani katika shambulizi la Marekani nchini Iraq mwaka 2020.

Ayatullah Khamenei ameeleza kuridhishwa na duru ya kwanza ya mazungumzo hayo akisema "imetekelezwa vyema".

Lakini alitahadharisha kwamba "hakuwa na matumaini makubwa wala mwenye kukata tamaa sana".

Pia ameonya hapo awali kuwa Iran italipiza kisasi endapompango wake wa nyuklia utashambuliwa.

Baadhi ya maafisa, akiwemo mshauri wake Ali Larijani, wamesema hata Iran inaweza "kulazimishwa" kuwa na silaha za nyuklia ikiwa itashambuliwa.

"Hatutengenezi silaha, na hatuna tatizo na uangalizi wa IAEA - hata ikiwa utaendelea kwa muda usiojulikana. Lakini ikiwa utaamua kushambulia, Iran haitakuwa na budi ila kufikiria upya jibu lake. Na sio kwa maslahi yako," Larijani aliiambia TV ya taifa mapema mwezi huu.

Kila upande unashinikiza msimamo wake kuhusu jinsi mazungumzo hayo yanavyoendeshwa.

Marekani wanasema wanataka mazungumzo ya moja kwa moja. Iran inasema haitaki mazungumzo ya moja kwa moja, na kwamba Oman inapatanisha kwa kubadilishana maandishi.

Baada ya duru ya kwanza mjini Muscat, Araghchi alikiri kuwa na mazungumzo mafupi na Witkoff "kutokana na uungwana wa kidiplomasia" baada ya kukutana.

Tovuti ya habari ya Marekani ya Axios, ikinukuu vyanzo, iliripoti wapatanishi wakuu wawili walizungumza kwa hadi dakika 45.

Tehran inapendelea usiri. Washington inatafuta kuweka mambo wazi kwa umma.

Baada ya pande zote mbili kutoa kauli chanya kuhusu duru ya kwanza, sarafu ya Iran ilipanda kwa asilimia 20%.

Uongozi wa Iran unafahamu vyema kutoridhika kwa umma juu ya hali mbaya ya kiuchumi ya nchi - na uwezekano wa maandamano ambayo yanaweza kutokea

Kwa Jamhuri ya Kiislamu, hofu sio tu juu ya mashambulizi - ni maandamano pia.

Pia unaweza kusoma:

Imefasiriwa na Asha Juma