Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mauaji ya mtoto Samantha Pendo: Ukatili wa polisi na muda mrefu wa kusubiri haki nchini Kenya
- Author, Anne Soy
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Miaka saba baada ya mtoto wao wa kike kuuawa wakati wa operesheni ya kikatili ya usiku wa manane iliyofanywa na polisi nchini Kenya, wakati wa vurugu wa baada ya uchaguzi, Joseph Oloo Abanja na Lensa Achieng bado wana uchungu huku kesi dhidi ya maafisa wanaodaiwa kuhusika ikicheleweshwa.
"Ni kovu ambalo halitaisha," anasema Bi Achieng, mfanyakazi wa hoteli, kuhusu kifo cha Samantha Pendo akiwa na miezi sita ambaye alikufa kwa kuvunjika fuvu la kichwa na kuvuja damu ndani.
Familia hiyo inaishi katika mji wa magharibi wa Kisumu - ngome ya upinzani ambako ghasia zilizuka Agosti 2017 kuhusu matokeo ya uchaguzi ambao hatimaye ulirudiwa kwa sababu ya dosari.
Siku ya tukio
Nyumba yao ndogo ilikuwa kando ya barabara katika makazi yasiyo rasmi ya Nyalenda, maandamano yalitokea tarehe 11 Agosti na polisi wa kupambana na ghasia walitawanywa.
Usiku huo wana ndoa hao walifunga mlango wao wa mbao na kuuwekea vitu vya samani. Majira ya saa sita usiku, walisikia milango ya majirani zao ikivunjwa na baadhi ya watu waliokuwa ndani wakipigwa.
Haikupita muda maafisa wa polisi wakafika mlangoni kwao.
"Waligonga na kuupiga teke mara kadhaa [lakini] nilikataa kufungua," anasema Abanja, akiongeza kuwa aliwasihi waiache iishi familia yake ya watu wanne.
Lakini mapigo hayo yaliendelea hadi maofisa hao wakapata nafasi ndogo ambayo waliitumia kurusha gesi ya kutoa machozi ndani ya nyumba hiyo yenye chumba kimoja, na kuwalazimisha wana familia kutoka nje.
Abanja anasema aliamriwa alale chini nje ya mlango na kisha kipigo kikaanza.
"Walikuwa wakipiga kichwa changu hivyo niliweka mikono juu ya kichwa, na wakapiga mikono yangu hadi haikuweza kushikilia tena."
Mkewe alitoka nje ya nyumba akiwa amemshika Samantha ambaye alikuwa akipumua kwa shida kutokana na mabomu ya machozi, naye hawakumuacha.
"Walinipiga [kwa virungu] nikiwa nimemshika binti yangu," anaema Bi Achieng.
Kitu cha pili alichohisi ni bintiye kumshika kwa nguvu "kama yuko kwenye maumivu."
"Nilimgeuza na kuona kilichokuwa kinatoka mdomoni mwake, ni povu."
Alipiga kelele kuwa wamemuua bintiye na hapo ndipo wakasimamisha vipigo na Bwana Abanja akaamriwa amtazame mtoto.
Mtoto alikuwa amejeruhiwa vibaya.
Wanandoa hao wanasema maafisa hao waliondoka haraka na majirani wakawasaidia kumkimbiza Samantha hospitalini. Alikufa baada ya siku tatu akiwa katika uangalizi mahututi.
Jitihada za kutafuta haki
Jitihada zao za kutafuta haki ni za muda mrefu na za kukatisha tamaa, kama zile za makumi ya wengine waliojikuta katika ghasia za baada ya uchaguzi.
Maafisa 12 wa polisi wanatarajiwa kushtakiwa kwa mauaji, ubakaji na utesaji - lakini usikilizwaji wa kesi hizo bado haujafanyika.
Mmoja wa mawakili wa waathiriwa, Willys Otieno, anaamini kuwa kucheleweshwa huko kunatokana na ukosefu wa nia ya kisiasa ya kutoa haki kwa waathiriwa wa ghasia za uchaguzi.
Uhuru Kenyatta alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2017 – mgombea wa upinzani alijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho. Naibu wake William Ruto, alishinda urais katika uchaguzi uliofuata – na kuingia madarakani Septemba 2022.
Otieno anamtuhumu mkurugenzi wa sasa wa mashtaka ya umma (DPP) kwa "kujifanya kama wakili wa washtakiwa."
"Hata sio washtakiwa waliowasilisha ombi la kesi kuahirishwa katika mahakama - ni DPP ndiye aliwasilisha ombi mahakamani kuahirisha kesi hiyo," anasema wakili huyo kuhusu majaribio mawili yaliyoshindwa ya kuwasilisha kesi mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana.
Jaribio la tatu lilikusudiwa lifanyike siku mbili zilizopita lakini limeahirishwa kwa sababu ya kuhamishwa jaji mkuu - na limepangwa kufanyika tena mwishoni mwa mwezi huu.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imeiambia BBC kuwa haiwezi kujibu maswali yake, lakini ilichapisha taarifa kwenye X ikisema, "kesi hiyo inasalia kuwa moja ya kesi kubwa katika historia ya karibuni, huku kifo cha mtoto (Samantha) Pendo kikiashiria msiba kutokana na ukatili wa polisi wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2017."
Uchunguzi wa kesi
"Ofisi ya DPP ndiyo iliyoanzisha kesi hii, na wao ndio waliokuja kwetu miaka kadhaa iliyopita," anasema Irungu Houghton, mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International Kenya.
Baada ya uchunguzi wa awali, DPP wa wakati huo, Nurdin' Hajji, alianzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mtoto Samantha. Hakimu aliwakuta polisi wana kesi ya kujibu.
Baadaye, mwendesha mashtaka wa umma aliamuru uchunguzi zaidi wa kesi nyingine zilizotokana na operesheni ya polisi ya Agosti 2017, na kuvileta vyombo huru vya uchunguzi, mashirika ya kiraia na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.
Uchunguzi ulifichua ushahidi ambao DPP alisema unaonyesha "ukatili, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono, dhidi ya raia, ambayo yote yanajumuisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu dhidi ya ubinadamu."
Oktoba 2022, mwendesha mashtaka alitaka washukiwa hao kushtakiwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya chini ya Sheria ya Kimataifa ya Uhalifu.
Watakaoshtakiwa ni pamoja na makamanda waliokuwa maafisa wakuu wakati huo – na itakuwa kesi ya kwanza ya aina hiyo nchini Kenya.
Septemba 2023 DDP mpya alichukua ofisi, Renson M Ingonga, lakini kumekuwa na mwendelezo mdogo wa kesi hiyo tangu wakati huo.
Inaonekana kuna "kutokuwepo kwa utayari wa kuanzisha kesi hii," anasema Houghton.
Kuna njia mbadala?
Otieno anasema mawakili wa waathiriwa wanafikiria kufungua kesi binafsi au kwenda katika Mahakama ya Afrika Mashariki au Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ikiwa ucheleweshaji utaendelea.
Wazazi wa Samantha wanaunga mkono wazo hili kwani bila haki wanasema hawawezi kupona - kila kuahirishwa kunafungua tena majeraha yao.
"Haijalishi nitatumia njia gani, ila nitahakikisha haki inapatikana," anasema Abanja, ambaye sasa ana umri wa miaka 40 na anajikimu kimaisha kwa kuendesha teksi ya bajaji.
"Walininyang'anya kitu ambacho ni cha thamani sana kwangu - alikuwa kila kitu kwangu, msichana mdogo niliyempa jina la mama yangu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah