Jinsi ndoto mbaya za mara kwa mara zinavyoweza kufupisha maisha yako

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuamka baada ya ndoto mbaya kunaweza kufanya moyo wako uende mbio, lakini madhara yanaweza kwenda mbali zaidi ya usiku usio na utulivu.
Watu wazima ambao huota ndoto mbaya kila wiki wana uwezekano wa karibu mara tatu wa kufa kabla ya umri wa miaka 75 kuliko wale ambao huota mara chache.
Hitimisho hili la kutisha, ambalo bado halijapitiwa upya, linatokana na watafiti waliochanganya data kutoka kwa tafiti nne kubwa za muda mrefu zilizofanywa nchini Marekani, wakiwafuatilia zaidi ya watu 4,000 wenye umri wa miaka 26 hadi 74.
Hapo awali, washiriki waliripoti ni mara ngapi ndoto mbaya zilikatiza usingizi wao.
Katika miaka 18 iliyofuata, watafiti walirekodi idadi ya washiriki waliokufa kabla ya wakati, 227 kwa jumla.
Hata baada ya sababu za hatari za kawaida kama vile umri, jinsia, afya ya akili, sigara na uzito, waligundua kuwa watu ambao walikuwa na ndoto mbaya kila wiki walikuwa na uwezekano wa karibu mara tatu wa kufa kabla ya wakati, hatari sawa na ile ya kuvuta sigara nyingi.
Ndoto hutokea wakati wa kulala, wakati ubongo unafanya kazi sana lakini misuli imepooza. Kuongezeka kwa ghafla kwa adrenaline, cortisol, na homoni nyingine za mafadhaiko kunaweza kuwa kali kama kitu chochote kinachotokea wakati wa kuamka.
Msongo wa mawazo wa mara kwa mara huathiri mwili. unachochea kuvimba, huongeza shinikizo la damu, na kuharakisha mchakato wa kuzeeka kwa kuondoa kinga za chromosomes zetu.
Zaidi ya hayo, kuamshwa ghafla na ndoto mbaya huvuruga usingizi mzito, kipindi muhimu ambacho mwili hujirekebisha na kuondoa uchafu kwenye kiwango cha seli. Kwa pamoja, athari hizi mbili, msongo wa kila wakati na ukosefu wa usingizi, vinaweza kuwa sababu kuu za mwili kuzeeka mapema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa watu wazima walio na ndoto za kila wiki wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa shida ya akili na ugonjwa wa Parkinson, miaka kabla ya dalili kuonekana.
Ushahidi unaoongezeka unaonesha kwamba maeneo ya ubongo yanayohusika katika ndoto pia huathiriwa na magonjwa ya ubongo. Kwa hiyo, ndoto mbaya za mara kwa mara zinaweza kuwa onyo la matatizo ya neva.
Ndoto za kutisha pia ni za kawaida. Takribani 5% ya watu wazima wanaripoti kuwa na takribani ndoto moja kwa wiki, na 12.5% wana ndoto moja kwa mwezi.
Tiba ya utambuzi wa tabia (CBT) ya kukosa usingizi, tiba ya mazoezi ya pich, ambapo wagonjwa huandika upya mwisho wa ndoto mbaya inayojirudia wakiwa macho na hatua rahisi kama vile kuweka chumba cha kulala kikiwa na baridi, giza, na bila skrini, zote zimeonesha kupunguza wingi wa ndoto mbaya.
Kabla ya kufikia hitimisho, ni muhimu kukumbuka mambo machache muhimu. Utafiti ulitegemea ripoti za ndoto za washiriki, ambazo zinaweza kufanya iwe vigumu kutofautisha kati ya ndoto mbaya ya kawaida na ile halisi. Zaidi ya hayo, washiriki wengi walikuwa Wamarekani weupe, hivyo huenda matokeo yasitumike kwa kila mtu.
Licha ya mapungufu, utafiti una nguvu muhimu zinazostahili kuzingatiwa. Watafiti walitumia vikundi vingi vya washiriki, waliwafuata kwa miaka mingi, na walitegemea rekodi rasmi za kifo badala ya data iliyoripotiwa. Hii inamaanisha kuwa hatuwezi kutupilia mbali matokeo haya kama mabadiliko tu ya takwimu.
Ikiwa timu nyingine za utafiti zinaweza kuiga matokeo haya, madaktari wanaweza kuanza kuwauliza wagonjwa kuhusu ndoto mbaya wakati wa ukaguzi wa kawaida, pamoja na kupima shinikizo la damu na kuangalia viwango vyao vya mafuta.
Matibabu ya kudhibiti ndoto za kutisha ni nafuu, si ya kuvamia, na yanapatikana kwa urahisi. Kupitishwa kwao kwa wingi kunaweza kutoa fursa adimu ya kuongeza muda wa kuishi huku tukiboresha ubora wa usingizi wetu.















