Ramadhani: Athari za kufunga unapokuwa na kisukari

Chanzo cha picha, Getty Images
'Insulini ni nini?'
Insulini ni homoni muhimu inayozalishwa kwenye kongosho inayosaidia kudhibiti sukari ya kwenye damu.
Ikiwa kongosho hutoa insulini kidogo sana au mwili hautumii insulini ipasavyo, matatizo mengi ya kiafya yanaweza kutokea.
Insulini inafanya kazi vipi mwilini?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Mwili hubadilisha chakula tunachokula kuwa sukari. Sukari hii ndio chanzo cha msingi cha nishati kwa mwili wetu.
- Sukari hii kisha inaingia kwenye damu yetu na kuashiria kongosho kutoa insulini.
- Insulini husaidia kusafirisha sukari kutoka kwa damu kwenda kwenye misuli, mafuta, na seli za ini, kwa hivyo mwili unaweza kutumia sukari hii kwa nishati au kuihifadhi kwa matumizi ya baadaye.
- Wakati sukari inapoingia kwenye seli, kiwango chake katika damu kinapungua, ambacho kinaashiria kongosho kuacha kutoa insulini.
Seli kushindwa kuchukua sukari kutoka kwenye damu?
Huu ni mchakato mgumu unaotokea wakati seli za misuli, mafuta na ini hazitoi ushirikiano ipasavyo kwa insulini.
Kwa sababu ya hili, seli huacha kunyonya au kuhifadhi sukari kwa ufanisi kutoka kwa damu.
Hii haipunguzi viwango vya sukari kwenye damu. Kongosho hutoa insulini zaidi ili kupunguza viwango vya sukari kwenye damu. Hali hii inaitwa 'hyperinsulinemia'.
Maadamu kongosho inatoa insulini ya kutosha kukabiliana na mwitikio wa seli dhaifu, viwango vya sukari ya kwenye damu hubaki kuwa katika viwango vinavyotakikana, yaani sio juu wala chini.
Wakati huo huo, ikiwa seli zitashindwa kuchukua sukari kwenye damu, kiwango cha sukari kitaongezeka.
Kuongezeka kwa sukari kwenye damu huongeza hatari ya magonjwa mengine mengi, pamoja na kisukari cha aina ya 2.
Sababu nane kwa nini seli kushindwa kuchukua sukari kwenye damu huongezeka

Chanzo cha picha, Franklin Joseph
Franklin Joseph ambaye pia ni mwanzilishi wa Kliniki ya kupunguza uzito anaangazia sababu zinazoweza kuchangia seli kushindwa kuchukua sukari kwenye damu:
- Unene: Hasa mafuta ya tumbo, inasemekana kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na tatizo hili
- Kupungua kwa shughuli za kimwili: Kutofanya mazoezi mara kwa mara kunaweza pia kuongeza hatari ya kupata tatizo hili
- Jenetiki: Baadhi ya watu wanapata tatizo hili kutokana na urithi wa jeni
- Lishe duni: Kula vyakula vilivyochakatwa, wanga iliyosafishwa, na ulaji wa chakula chenye sukari nyingi pia kunaweza kusababisha tatizo hili
- Lishe kama hiyo inaweza kusababisha viwango vya sukari kwenye damu kuongezeka haraka, ambayo pia inaweza kuongeza uzalishaji wa insulini.
- Msongo wa mawazo wa kila mara: Homoni hizi kama vile 'cortisol' zinaweza kutatiza uwezo wa insulini kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu
- Matatizo ya kupata usingizi: Ukosefu wa usingizi yanaweza kuathiri jinsi seli za mwili zinavyotumia sukari inayopatikana kwenye damu.
- Ukosefu wa usingizi unaweza kuharibu viwango vya homoni katika mwili
- Kuongezeka kwa umri kunaweza kupunguza mwitikio wa seli katika mwili wa binadamu. Hii huongeza hatari ya kupata tatizo hili
Mfungo wa Ramadhani
Wakati wa mwezi wa Ramadhani, jumuiya nyingi za Kiislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi jioni. Shirika la misaada la Ugonjwa wa Kisukari Uingereza linawashauri watu wanaokabiliwa na matatizo ya kiafya kuwa waangalifu.
Profesa Wasim Hanif, Profesa na Mkurugenzi wa Kliniki ya Kisukari katika Hospitali ya Chuo Kikuu Birmingham, anasema, "Kufunga wakati una kisukari kunaweza kuwa hatari."
Hii inaweza kusababisha matatizo mengi yanayohusiana na afya. "Ni muhimu sana kwa watu kama hao kufunga tu baada ya kushauriana na mtaalamu wa ugonjwa wa kisukari."
Dk. Franklin Joseph anasema, kulingana na tafiti zingine, kufunga kunaweza kuboresha mwitikio wa insulini kwa watu walio na tatizo la seli kushindwa kuchukua sukari kwenye damu na kisukari cha aina ya 2.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wengine wanaweza kupoteza uzito au kupata mabadiliko katika mafuta ya mwili wakati wa kufunga. Yote hii inaweza kuathiri mwitikio wa insulini na kimetaboliki. Watu wanene hasa wanakabiliwa na tatizo hili.
Franklin Joseph alisema kuwa kufunga kunaweza kuwa na athari tofauti kwa kila mtu. Athari za kufunga kwenye mwitikio wa insulini na kimetaboliki hutegemea mambo kama vile umri wa mtu, jinsia, afya, chakula, na shughuli za kimwili.
Anasema, "Ni muhimu kwa watu wenye kisukari na matatizo mengine ya kimetaboliki kuwa waangalifu na afya zao wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani. Wafunge kulingana na ushauri wa daktari wao."
"Iwe unafunga mara kwa mara au unafunga wakati wa Ramadhani, kufuata mtindo mzuri wa kula ni muhimu sana kwa afya bora," anasema Reem Al-Abdalat, mtaalamu wa lishe huko Amman.
Kipimo cha glycemic ni nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hiki ni kipimo cha ulinganisho wa jinsi sukari inavyoongezeka haraka au polepole baada ya kula chakula.
Tunaweza kutumia kipimo hiki kujua jinsi sukari yetu inavyopanda haraka, wastani, au polepole baada ya kula chakula chochote.
Wanga, ambayo humengenywa polepole, inachukuliwa kuwa na kiwango cha chini cha glycemic. Hii ni pamoja na mboga mboga, matunda, maziwa yasiyotiwa sukari, kunde na nafaka.
Sukari, vyakula vitamu na vinywaji, viazi vyeupe, na mchele mweupe huchukuliwa kuwa na kiwango cha juu. Vyakula hivi husababisha viwango vya sukari kwenye damu kuongezeka haraka.
Hata hivyo, kipimo hiki pekee hakiwezi kubaini kama chakula ni kizuri kwa afya au la. Kwa mfano, chokoleti nyingi zina kiwango cha chini ya glycemic lakini ina kalori nyingi.
Vile vile, vyakula vilivyo na kiwango cha juu cha glycemic sio lazima viwe vibaya. Matunda mengi, kama tikiti maji, yana kiwango cha juu cha glycemic. Lakini matunda haya yana faida nyingi mwilini.
Je, tatizo la seli kushindwa kuchukua sukari kwenye damu linaweza kupata tiba?
Profesa Joseph anasema, "Tatizo hili linaweza kutibiwa kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha na, wakati mwingine, dawa."
Mtaalamu wa lishe Reem Al-Abdalat anasema, "Unahitaji kuzingatia sana mlo wako. Unapaswa kuepuka kula peremende. Unapaswa kupunguza ulaji wako wa vyakula vya wanga."
Mazoezi ya mara kwa mara husaidia kupunguza uzito hasa, karibu na tumbo ambako kunaweza kuimarisha mwitikio wa insulini.
Hii pia ni pamoja na kuondokana na tatizo la msongo wa mawazo. Profesa Joseph anasema kwamba unaweza kukabiliana na msongo wa mawazo kwa tiba vile ya kutafakari, yoga, mazoezi ya kupumua sana na kadhalika.
Kupata usingizi mzuri ni muhimu sana.
Hatimaye, dawa kama vile metformin husaidia kupunguza tatizo hili pamoja na kisukari cha aina ya 2.
Hata hivyo, ni muhimu kushauriana na daktari ili kujua ni kiasi gani matibabu yatasaidia.
Imetafsiriwa na Asha Juma












