Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waandamanaji wakaidi amri ya Mkuu wa Majeshi Tanzania
Mamia ya watu wameuawa nchini Tanzania wakati wa maandamano ya siku tatu ya uchaguzi mkuu wa Jumatano, chama kikuu cha upinzani nchini humo kimesema.
Idadi ya vifo inatofautiana, huku hatua ya serikali kuzima mtandao wa intaneti kote nchini ikifanya kuwa vigumu kuthibitisha idadi halisi ya vifo au majeruhi.
Msemaji wa chama cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameliliambia shirika la habari la AFP kwamba "takriban watu 700" wameuawa katika mapambano na vikosi vya usalama, chanzo cha kidiplomasia nchini Tanzania kimeiambia BBC kwamba kuna ushahidi wa kuaminika kwamba watu wasiopungua 500 wamefariki.
Serikali inaonekana ''kudhibiti'' ukubwa wa ghasia hizo - na mamlaka zimeongeza muda wa amri ya kutotoka nje kwa nia ya kukomesha machafuko hayo.
Waandamanaji wengi wao vijana wamejitokeza barabarani ka kote Tanzania kupinga uchaguzi mkuu wa Jumatano Oktoba 29 ambao wanasema haukuwa wa haki.
Wanaishutumu Serikali kwa kukandamiza demokrasia kwa kuwazuia viongozi wakuu wa upinzani kushiriki – mmoja yuko jela na mwingine kuenguliwa kwa misingi ya kiufundi na hivyo kumuongezea Rais Samia Suluhu Hassan nafasi ya kushinda akiwa na chama chake tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Maandalamo yaliendelea siku ya Ijumaa, huku waandamanaji katika mji wa bandari wa Dar es Salaam wakikaidi amri iliyotolewa na Mkuu wa Majeshi ya kukomesha vitendo vya vurugu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Kombo Thabit ametaja ghasia hizo kuwa ni "matukio michache ya hapa na pale" na kusema "vikosi vya usalama vilichukua hatua haraka na madhubuti kushughulikia hali hiyo".
"Pia tunaendelea kupokea ripoti za mali zilizoharibiwa," waziri aliiambia BBC Focus on Africa, akiongeza kuwa kuzimwa kwa mtandao kulikuwa muhimu kukomesha uharibifu huo na kuokoa maisha.
''Wakati tulipowasha mtandao wa intaneti ilileta shida kwa watu wachache 'wahuni' ambao walikuwa wakitumia mtandao kuhamasisha vurugu. Sasa kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kusimamia mawasiliano Tanzania - kuna sheria ambazo zinatumiwa wakati kuna hofu ya usalama wa kitaifa kuhusu mtandao wa intaneti ndani ya nchi.''
Aliongeza kusema: ''Haya si mambo ya haki au ukosefu wa haki, tunazungumzia maisha ya watu, mali ya watu na usalama wa nchi yetu.''
Balozi Mahmoud Thabit pia alitetea jinsi serikali ilivyokabiliana na waandamanaji baada ya uchaguzi wa Jumatano wiki hii.
Imekuwa vigumu kwa waandishi wa habari na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuangalia ripoti za vifo, na hospitali zimekuwa zikikataa kutoa habari zinapoulizwa kuhusu majeruhi.
Chanzo cha habari katika hospitali moja jijini Dar es Salaam kiliiambia BBC kuwa imezidiwa na idadi ya majeruhi tangu Alhamisi, na kwamba hospitali nyingi za umma jijini humo zikikabiliwa na hali sawa na hiyo, huku makafani zikiripotiwa kujaa hadi pomoni,
Mwanasiasa mmoja wa Chadema alisema anahofia maisha yake kwani "mauaji yanafanyika nyakati za usiku wakati hakuna mtu anayeshuhudia".
"[Vikosi vya usalama] vinawasaka viongozi wetu na wengine wamelazimika kuondoka nchini. Watu hawa wanaua bila kuwajibishwa," John Kitoka, mkurugenzi wa Chadema wa mambo ya nje na diaspora, aliambia kipindi cha Newshour cha BBC.
"Tuna wasiwasi kwamba maandalizi ya uchaguzi yalikumbwa na visa unyanyasaji, utekaji nyara na vitisho kwa upinzani, waandishi wa habari na watendaji wa mashirika ya kiraia," aliongeza.
Umoja wa Mataifa imeoa wito kwa vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Visiwani Zanzibar - ambako watu huchagua serikali na kiongozi wake - Hussein Mwinyi wa CCM, ambaye ni rais aliyeko madarakani, alishinda kwa karibu asilimia 80 ya kura.
Upinzani huko Zanzibar umedai kuwa uchaguzi ulikumbwa na "udanganyifu mkubwa", shirika la habari la AP liliripoti.
Watalii katika kisiwa hicho wanaripotiwa kukwama katika uwanja wa ndege, huku maandamano ya Tanzania bara na kuzimwa kwa mtandao kukiathiri safari za ndege.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa Jumamosi, lakini Rais Samia anatarajiwa kushinda kupitia Chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeongoza nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1961.
Samia aliingia madarakani mwaka 2021 kama rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.
Hapo awali alisifiwa kwa kupunguza ukandamizaji wa kisiasa, lakini hali ya kisiasa tangu wakati huo imeendelea kuminywa, huku serikali yake ikishutumiwa kuwalenga wakosoaji kupitia wimbi la utekaji nyara.
Tundu Lissu ambaye ni kiongozi mkuu wa upinzani yuko jela baada ya kufunguliwa mshataka ya uhaini ambayo anayakanusha na chama chake kususia kura.
Mgombea mwingine, Luhaga Mpina wa Chama cha ACT-Wazalendo, alienguliwa kutokana na taratibu za kisheria.
Vyama vidogo 16 ambavyo havina uungwaji mkono mkubwa wa umma kihistoria, viliruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo.