Tunachokifahamu kuhusu wanajeshi 200 wa Marekani waliotumwa Nigeria

Muda wa kusoma: Dakika 4

Marekani inapania kuwatuma wanajeshi 200 zaidi nchini Nigeria, ili kuwapa mafunzo ya kijeshi wanajeshi wa taifa hilo kuhusu jinsi ya kupambana wapiganaji wenye itikadi kali.

Marekani imesema kuwatuma wanajeshi zaidi nchini Nigeria ni mwendelezo wa jitahada zao za kuisaidia Nigeria kukabiliana na utovu wa usalama

Nigeria yadhibitisha uwepo wa wanajeshi wa Marekani

Mamlaka za Nigeria zimedhibitisha ujio wa wanajeshi wa Marekani. Msemaji wa jeshi la Nigeria Meja Jenerali Samuel Uba, aliiambia BBC kuwa;

"Kutokana na maombi yaliyotolewa na serikali ya Nigeria katika kamati ya pamoja ya Nigeria na Marekani, Marekani imetuma kikosi ambacho kitatusaidia kutoa mafunzo na kurekebisha vifaa tulivyonavyo na kutupa ushauri kuhusu maeneo tofauti."

"Wanajeshi hao hawataingia nyanjani kupigana moja kwa moja" Alisema Jenerali Uba.

Wanajeshi hao 200 watakuwa wanajiunga na wanajeshi wengine wa Marekani ambao tayari wako nchini humo.

Nigeria imekuwa ikipokea shinikizo katika siku za hivi karibuni kutoka Washington kwa kushindwa kuwalinda waumini wa kikristo kutoka kwa wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali kaskazini Magharibi mwa taifa hilo.

Taifa la Nigeria limekanusha kuwauwa na kuwatesa waumini wa kikristo, na kusema mashambulio yanayotekelezwa na makundi yenye itikadi kali yanawalenga wakristo na waislamu.

Kundi la Boko Haram, wapiganaji wa Islamic State West Africa Province (ISWAP) na makundi mengine, yameongeza mashambulizi yao kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Taifa la Nigeria lina idadi ya watu zaidi ya millioni 230, na limegawanyika mara mbili, waumini wengi wakikristo wakiwa kusini mwa taifa hilo, huku waumini wengi wa kiislamu wakiwa kaskazini mwa taifa hilo.

Licha ya Nigeria kuwa na tofauti zao na Marekani, mataifa hayo mawili yamekubaliana kushirikiana kiusalama.

Shambulio la Marekani nchini Nigeria

Disemba mwaka uliopita, Marekani ilitekeleza shambulizi katika kambi moja la Islamic State katika jimbo la Sokoto, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Trump alisema "Chini ya utawala wake,taifa lake halitakubali itikadi kali za dini ya kiislamu kuenea."

Tangu shambulio hilo la Marekani, Nigeria na Washington wamekuwa wakiimarisha uhusiano wao wa kiusalama.

Mwezi Januari, Marekani ilituma silaha za kijeshi nchini Nigeria kama njia ya kuimarisha ushirikiano wao wa kiusalama pamoja na kuendelea kuwapa taarifa za kijasusi.

Mbona Trump anajali hali ya usalama Nigeria?

Mwaka jana, Seneta wa Marekani Ted Cruz, aliishtumu Nigeria kwa kuruhusu 'mauaji ya kimbari' dhidi ya wakristo.

Cruz aliwasilisha azimio katika bunge la Seneti mwezi Septemba mwaka uliopita, ambapo alitaka Marekani kuingilia kati usalama wa Nigeria.

Mwezi Oktoba tarehe 8, Ted Cruz, alichapisha kwenye mtandao wa X kuwa makundi yenye itikadi kali yamewauwa waumini wa kikristo zaidi ya elfu hamsini, kuharibu vyule 2,000 na makanisa 18,000.

Cruz aliitaka bunge la Congress kuwawekea vikwazo maafisa wakuu katika serikali ya Nigeria ambao aliwatuhumu kwa "kuwaondoa na wakati mwingine kuwasaidia watu wafisadi ikiwemo magaidi."

Serikali ya Nigeria ilikanusha madai ya Ted Cruz, na kusema makundi yanayotekeleza mashamabulizi hayo yanawalenga raia wote wa Nigeria bila kubagua, na kuongeza kuwa wanajitahidi kuimarisha hali ya usalama .

Trump baadaye alisema kuwa iwapo Nigeria haitawajibika basi ataingilia kati na kuchukua wajibu huo.

Hatua zilizochukuliwa na Nigeria

Kufuatia mashambulizi kadhaa kaskazini mwa taifa hilo, Nigeria ilitangaza hali ya dharura kutokana na utovu wa usalama.

Visa vya wanafunzi kutekwa wakiwa shuleni na waumini wakikristo kutekwa kanisani vimeripotiwa.

Watu waliojihami waliwateka wanafunzi 300 mwezi Novemba 21 pamoja na walimu katika shule ya St. Marys katika jimbo la Niger.

Wengi waliotekwa tayari wameachiliwa na kurejea kwa familia zao.

Nigeria ilituma kikosi chake maalum chini ya mshauri wa usalama wa kitaifa Nuhu Ribadu, nchini Marekani kuzungumzia hali ya usalama nchini humo.

Na baadaye Marekani ilituma kikosi chake nchini Nigeria ambapo walikubaliana kushirikiana.

Hii ina maanisha nini?

Kufuatia kutumwa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Nigeria, mchambuzi wa masuala ya usalama nchini Nigeria Abdullahi Bakoji Adamu, anasema hatua hii inaweza kulisaidia taifa hilo kukabiliana na changamoto walionayo ya kudorora kwa usalama.

"Kwa njia moja au nyingine itakuwa hatua kubwa, ila si suluhisho kamili."

Aliongezea kuwa ushirikiano na Marekani itawapa mafunzo ya kisasa maafisa wa kijasusi wa Nigeria, kutokana na teknoljia ya kisasa na makombora wanayomiliki Marekani.

Aidha aliongezea kuwa changamoto bado ni kubwa "Wanajeshi wa kigeni hawajui taifa hili vizuri,na watu walivyo. Tatizo la usalama Nigeria ni zaidi ya bunduki, inahusisha utamaduni wa watu, kabila, umaskini na siasa."

Mchambuzi huyo alisema kuwa kutokana na hali ya Nigeria ilivyo, kutegemea vikosi vya kigeni kikamilifu haitakuwa jambo la busara.

Bakoji Adamu anasema njia sahihi ya kutatua changamoto za kiusalama ni kuimarisha vikosi vya usalama nchini Nigeria, kuboresha silaha wanazotumia na kuboresha maslahi yao.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula