Mzozo wa Elon Musk na Afrika Kusini juu ya Starlink

    • Author, Khanyisile Ngcobo
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mzozo kati ya bosi wa Starlink, Elon Musk na Afrika Kusini baada ya kushindwa kuzindua huduma za kampuni hiyo nchini humo, kutokana na sheria za taifa hilo za kuwawezesha watu weusi, huenda ni moja ya sababu ya mzozo wa kidiplomasia kati ya Marekani na taifa hilo lililoendelea kiviwanda barani Afrika.

Mbele ya wafuasi wake zaidi ya milioni 219 kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, Bw Musk alitoa tuhuma za ubaguzi wa rangi na kudai kuwa huduma yake ya intaneti kupitia satelaiti "haikuruhusiwa kufanya kazi nchini Afrika Kusini kwa sababu mimi si mweusi."

Lakini Mamlaka Huru ya Mawasiliano ya Afrika Kusini (Icasa) - inayoshughulikia sekta ya mawasiliano na utangazaji - imeiambia BBC kwamba Starlink haijawahi kuwasilisha maombi ya leseni.

Na Wizara ya mambo ya nje, ilisema kampuni hiyo inakaribishwa kufanya kazi Afrika Kusini "mradi tu inafuata sheria za nchi hiyo."

Ili kufanya kazi nchini Afrika Kusini, Starlink inahitaji kupata mtandao na leseni, ambazo zote zinapaswa umiliki wa 30% uende kwa watu weusi.

Hasa ni watu weusi wa Afrika Kusini, ambao walitengwa kiuchumi wakati wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na apataidi.

Utawala wa kibaguzi wa Wazungu walio wachache uliisha mwaka 1994 baada ya Nelson Mandela na chama chake cha African National Congress (ANC) kuingia madarakani.

Tangu wakati huo, ANC "imewawezesha watu weusi" na kulifanya hilo kuwa nguzo kuu katika sera yake ya kiuchumi, kama jaribio la kukabiliana na dhuluma za ubaguzi wa rangi wa hapo awali.

Kuna sheria inayowataka wawekezaji kuzipa makampuni ya ndani ya watu weusi hisa 30% katika biashara zao nchini Afrika Kusini.

Musk na Afrika Kusini

Musk - alizaliwa Afrika Kusini mwaka 1971 kabla ya kuhamia Canada mwishoni mwa miaka ya 1980 na kisha Marekani, ambako akawa mtu tajiri zaidi duniani. Anaonekana kuiona sheria hii kama kikwazo kwa Starlink kufanya kazi nchini humo.

Starlink inasema masharti ya kuwawezesha watu weusi katika sheria, inawatenga wamiliki "wengi" wa satelaiti kutoka nchi za kigeni kuingia katika soko la Afrika Kusini, kulingana na tovuti ya habari ya TechCentral.

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje Clayson Monyela alipinga maoni haya mwezi Machi, akisema zaidi ya kampuni 600 za Marekani, ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya kompyuta ya Microsoft, zinafanya kazi nchini Afrika Kusini kwa kufuata sheria zake - na "zinastawi."

Starlink ya Musk ina mshirika mkubwa ambaye ni Waziri wa Mawasiliano wa Afrika Kusini, Solly Malatsi.

Anatoka chama cha Democratic Alliance (DA) - chama cha pili kwa ukubwa nchini Afrika Kusini - ambacho kilijiunga na serikali ya mseto baada ya ANC kushindwa kupata wabunge wengi katika uchaguzi wa mwaka jana.

DA ni mkosoaji mkali wa sheria za sasa za kuwawezesha watu weusi, chama hicho kinadai zinachochea upendeleo na ufisadi huku wawekezaji wakilazimishwa kuunganishwa na kampuni zenye uhusiano na ANC ili kufanya kazi nchini Afrika Kusini au kushinda kandarasi za serikali.

Oktoba mwaka jana, Malatsi alidokeza kwamba anatafuta njia ya kukwepa sera ya asilimia 30 kwa watu weusi. Lakini Waziri huyo wa mawasiliano huenda anakabiliwa na upinzani wa kisiasa kutoka kwa wabunge wa ANC bungeni pale atakapojaribu kuibadilisha sera hiyo.

Khusela Diko, mwenyekiti wa kamati ya mawasiliano ya bunge, alimuonya Malatsi mapema mwezi huu kwamba "mabadiliko" katika sekta ya teknolojia hayawezi kujadiliwa, akionekana kupinga kuipa Starlink ya Musk upendeleo wowote maalum.

Msimamo huo mgumu wa Diko haujashangaza kwani uhusiano kati ya serikali ya Afrika Kusini na Marekani umeharibika katika muhula wa pili wa Rais wa Marekani Donald Tump.

Marekani na Afrika Kusini

Musk, ambaye ni miongoni mwa watu wa karibu wa Trump, amekosoa kile anachokiita "sheria za kibaguzi za umiliki" nchini Afrika Kusini, huku rais wa Marekani akitishia kususia mkutano wa viongozi wa dunia wa G20 utakaofanyika nchini humo baadaye mwaka huu.

"Wanachukua ardhi ya Wakulima wa Kizungu, na kisha kuwaua wao na familia zao," Trump alisema kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social .

Madai yake ya mauaji ya halaiki dhidi ya wakulima wa kizungu yamekanushwa na wengi kuwa ya uongo, lakini ndio madai hayo hayo ya bilionea wa teknolojia.

Mwezi uliopita, Musk alikishutumu chama cha kisiasa nchini Afrika Kusini - chama chenye itikadi kali cha Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho kilishika nafasi ya nne katika uchaguzi wa mwaka jana - kwa "kuhimiza mauaji ya wazungu."

"Mwezi mmoja uliopita, serikali ya Afrika Kusini ilipitisha sheria ya kuhalalisha kuchukua ardhi kutoka kwa watu weupe bila hiari yao na bila malipo," anasema Musk.

Afŕika Kusini ilipitisha sheŕia mapema mwaka huu ambayo inaruhusu seŕikali kutaifisha ardhi bila fidia, lakini katika baadhi ya kesi maalumu.

Lakini Musk anaunganisha maswala haya na kushindwa kwake kupata leseni ya Starlink.

"Starlink haiwezi kupata leseni ya kufanya kazi nchini Afrika Kusini kwa sababu mimi sio mtu mweusi." Alisema mwezi Machi.

Msimamo wake mkali unakuja licha ya kukutana na rais wa Afrika Kusini mjini New York mwaka jana. Musk aliutaja mkutano huo kuwa mzuri, huku Rais Cyril Ramaphosa akisema alijaribu kumshawishi bilionea huyo kuwekeza nchini Afrika Kusini.

Lesotho inaonekana kutii shinikizo kutoka kwa utawala wa Trump kwa kutangaza Jumatatu kwamba imetoa leseni ya miaka 10 kwa Starlink.

Inakuja baada ya Trump kuweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa kutoka Lesotho, na hilo linatishia ajira za maelfu ya watu nchini humo.

Baadaye Trump alisitisha ushuru huo kwa siku 90, lakini ushuru wa 10% umeanza kutumika tarehe 5 Aprili.

Baadhi ya ripoti zinaonyesha Mamlaka ya Mawasiliano ya Lesotho (LCA), iliondoa vikwazo ili kuepusha tishio la kupandishwa kwa ushuru zaidi kwa kuipa Starlink leseni.

Hata hivyo, hili lilikataliwa na Waziri wa Mambo ya Nje Lejone Mpotjoane: "Maombi ya leseni na mazungumzo ya ushuru hayapaswi kuunganishwa," alisema.

Uamuzi wa kutoa leseni ulilaaniwa na shirika la kiraia la Section Two, na kusema Starlink huko Lesotho inamilikiwa na wageni kwa 100% na haina umiliki wa ndani, iliripoti tovuti ya habari ya GroundUp ya Afrika Kusini.

Wakati wa mashauriano kuhusu ombi la Starlink, Vodacom Lesotho, ilisema kampuni ya Musk inapaswa kuanzisha umiliki wa ndani kabla ya kupokea leseni, imeripoti tovuti ya Space in Africa.

Kwengineko Namibia, koloni la zamani la Ujerumani, ilikuwa chini ya utawala wa Wazungu wachache wa Afrika Kusini hadi ilipopata uhuru mwaka 1990.

Ina masharti magumu zaidi kuliko jirani yake. Biashara zinazofanya kazi nchini Namibia zinahitaji kumilikiwa na watu wa ndani kwa 51%.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano ya Namibia (Cran) iliambia BBC, Starlink iliwasilisha ombi la leseni kwa ya Mawasiliano mawasiliano Juni 2024, lakini ombi hilo bado halijapitishwa.

Starlink sasa inafanya kazi katika zaidi ya nchi 20 Afrika. Somalia yenye mgogoro, imeipa leseni ya miaka 10, siku mbili kabla ya Lesotho kufanya kama hivyo.

Starlink inatoa huduma za intaneti za kasi kwa maeneo yote hata ya mbali, hata ambayo hayana huduma za simu, hadi katika maeneo ya vijijini.

Starlink haitegemei nyaya au minara, badala yake hutumia mtandao wa setilaiti katika obiti ya dunia. Kwa sababu satalaiti hizo ziko karibu na dunia, zina kasi kwa intaneti kuliko satelaiti za jadi.

Nigeria lilikuwa taifa la kwanza la Afrika kuruhusu Starlink kufanya kazi, mwaka 2023. Kampuni hiyo tangu wakati huo imekua mtoa huduma wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.