Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Amechaguliwa na Mungu': Wakristo wanaomwona Trump kama mwokozi wao
Aleem Maqbool
Mhariri wa Masuala ya dini
Akiwa amesimama kwenye jukwaa katika kituo cha mikutano cha Florida usiku wa uchaguzi, safu ya bendera za Marekani nyuma yake na umati wa watu wenye furaha wakitazama, Donald Trump alisema: "Watu wengi wameniambia kwamba Mungu aliokoa maisha yangu kwa sababu fulani, na sababu hiyo ilikuwa ni kuokoa nchi yetu na kuirejesha Marekani katika ukuu.”
Hii ilikuwa moja ya mada ya kuvutia zaidi ya kampeni yake ya uchaguzi - kwamba alikuwa amechaguliwa na Mungu. Hata kabla ya jaribio la kumuua mnamo Julai 13 huko Butler, Pennsylvania, mamilioni ya Wamarekani tayari walihisi kuongozwa na imani yao kumuunga mkono rais wa zamani, na sasa ajaye.
Wengine walifanya uchaguzi kwa njia isiyo ya kawaida na kumfananisha Trump na mtu anayetajwa katika Biblia.
Mwaka jana, kwenye kipindi cha Kikristo cha FlashPoint, mwinjilisti wa TV Hank Kunneman alielezea "vita kati ya wema na uovu", na kuongeza: "Kuna kitu juu ya Rais Trump ambacho adui anaogopa: kinaitwa upako."
Jim Caviezel, mwigizaji aliyeigiza kama Yesu katika filamu ya Mel Gibson ya 'The Passion of the Christ', alitangaza, ingawa kwa mzaha, kwamba Trump alikuwa "Musa mpya". Kisha, katika miezi kadhaa kabla ya uchaguzi, wengi wa wafuasi wake walimtaja kama "mwokozi".
Swali ni kwa nini. Ni nini kilichowafanya watu wengi wamwone mtu huyu, ambaye hajulikani kuwa na imani yenye nguvu sana, kama aliyetumwa na Mungu?
Na hilo linasema nini kuhusu Ukristo kwa upana zaidi katika nchi ambayo idadi ya waenda kanisani inapungua haraka?
'Sisi sote tumetenda dhambi'
Mchungaji Franklin Graham ni mmoja wa wainjilisti mashuhuri zaidi wa Marekani na mtoto wa Billy Graham, bila shaka mhubiri maarufu. Yeye ni mmoja wa waumini wa Trump, aliyesadiki hakuna shaka kwamba rais mteule alichaguliwa kwa misheni hii na Mungu.
"Risasi iliyopitia sikioni ilikosa ubongo wake kwa milimita moja, na kichwa chake kiligeuka sekunde ya mwisho wakati bunduki hiyo ilipofyatuliwa," anasema. "Ninaamini kwamba Mungu aligeuza kichwa chake na kuokoa maisha yake."
Maswali yaliyoulizwa kuhusu tabia ya Trump - ikiwa ni pamoja na mashtaka ya utovu wa maadili ,kashfa za ngono, na madai ya uhusiano wake na nyota wa filamu ya watu wazima Stormy Daniels na kesi inayohusiana na ulipaji wa fedha ili kuficha kilichotokea - hayafichi maoni ya Bw Graham.
“Unakumbuka Yesu alipouambia umati, ‘Yule asiye na dhambi na apige jiwe la kwanza’ na kwamba polepole, wasikilizaji wote walianza kutoweka? Sisi sote tumefanya dhambi.”
Sehemu ya sababu baadhi ya Wakristo wanaweza kuona ni rahisi kuangalia maswali ya zamani ya tabia ni kwamba wakati wa muhula wa kwanza wa Trump madarakani alitoa ahadi fulani: kuteua majaji wanaopinga uavyaji mimba katika Mahakama ya Juu ya Marekani.
Bw Graham anaashiria hili kama ushahidi kwamba rais mteule ni mtu mwadilifu.
"Huu ni ushindi mkubwa kwa Wakristo, kwa wainjilisti," anasema. "Tunaamini rais atatetea uhuru wa kidini pale ambapo wanachama wa Democrat hawataweza."
Kuchaguliwa kwa Mike Huckabee kama balozi wa Israeli tayari ni kidokezo kwamba imani inaweza kuunda sera fulani ya kigeni. Wainjilisti wa Marekani akiwemo Huckabee ni miongoni mwa wafuasi wa dhati wa nchi hiyo .
Wengi wao wanaamini kwamba Wayahudi wanapaswa kujaza eneo lote la Israeli ya kale, ikiwa ni pamoja na eneo ambalo sasa linakaliwa na Ukingo wa Magharibi na Gaza, ili kuharakisha matukio yanayoongoza kwenye Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.
Dini inayodorora kwa kasi
Hapo awali Donald Trump alizungumza juu ya kuwa na malezi ya Kipresbiteri. Lakini licha ya uungwaji mkono wake mkubwa kutoka kwa Wakristo katika uchaguzi wa wiki iliyopita, hakuwahi kujaribu kwa bidii kuwashawishi katika kampeni yake ya hivi majuzi kwamba alikuwa mmoja wao.
"Nadhani alitambua kuwa itakuwa rahisi kubishana kwamba yeye mwenyewe ni mtu wa kidini, lakini badala yake alichukua kama jambo la 'nifae kwa hili nikufae kwa jingine' anasema Robert Jones, mwanzilishi na rais wa Taasisi ya Umma ya Utafiti wa Dini ( PRRI), ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifuatilia mienendo ya kidini nchini Marekani.
Mtazamo huo ulikazia mabadiliko katika idadi ya watu na idadi inayopungua ya wanaoenda kanisani.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, karibu 90% ya watu wazima wa Marekani walitambuliwa kama Wakristo - takwimu ambayo ilikuwa imeshuka hadi 64% mapema muongo huu, na ongezeko kubwa la idadi ya wale wasio na imani yoyote, kulingana na data kutoka Kituo cha Utafiti cha Pew.
Hili, anasema Dk Jones, lilikuwa jambo ambalo Trump aliweza kutumia.
"Ujumbe wa Trump ulikuwa: 'Najua mnapungua kwa idadi, Najua watoto na wajukuu zenu hawashirikiani na Makanisa yenu tena, lakini mkinichagua, nitarejesha mamlaka kwa Makanisa ya Kikristo.'
Sio Wakristo wote nchini Marekani walishawishika, hata hivyo Kwa wengine, imani yao imewaongoza kwa maoni tofauti na ya Trump.
'Trump amedhalilisha na kukebehi'
Katika miezi ya hivi majuzi, kutoka kwenye mimbari ya Bible Ways Ministries huko Atlanta, Georgia, Mchungaji Monte Norwood amekuwa akishiriki ujumbe tofauti sana na ule wa Franklin Graham.
Yeye, kwanza,alisikitishwa na matokeo ya uchaguzi wa wiki jana.
"Trump amedhalilisha na kuwakebehi karibu kila mtu anayeweza, kutoka kwa wahamiaji hadi walio wachache hadi wanawake hadi wale ambao ni walemavu," anasema.
"Wakristo wazungu wenye misimamo ya kihafidhina wa Republican ambao wanapuuza tabia ni wanafiki tu."
Kwa muda mrefu amekuwa akipinga wazo la muhula wa pili wa Trump, na amezungumza haya kwenye mitandao ya kijamii na kupitia harakati za kuhimiza wapiga kura kujitokeza - kama vile kuwasaidia wapiga kura wengine weusi kujiandikisha kupiga kura na kupata safari za bure kwenda kupiga kura.
“Mimi ni Mkristo wa aina ya Mathayo sura ya 25 – ambapo Yesu alisema: ‘Nilipokuwa na njaa ulinilisha, nilipokuwa na kiu, ulininywesha.’”
Katika historia: Mifumo ya upigaji kura wa Kikristo
Utafiti wa PRRI umeangalia rekodi za upigaji kura katika historia, sio tu kwa mazoea ya kidini na imani lakini pia kwa rangi, na kugundua kuwa linapokuja suala la maoni ya kisiasa, kumekuwa na mwelekeo wazi kwa miongo kadhaa.
"Karibu bila ubaguzi, vikundi vya Wakristo wazungu wameelekea kupiga kura ya Republican katika mashindano ya urais," anasema Dk Jones. "Makundi ya Wakristo wasio wazungu, makundi yasiyo ya Kikristo na wapiga kura wasio na uhusiano wa kidini wameelekea kupiga kura ya Democrat."
Mtindo huu ulianza miaka ya 1960, anaongeza, wakati chama cha Democratic kilihusishwa na vuguvugu la haki za kiraia na vikundi vya Wakristo wazungu vilianza kuhamia Chama cha Republican.
Upigaji kura kabla ya uchaguzi wa 2024 unaozingatia nia ya wapigakura ulipendekeza kuwa kwa sehemu kubwa mtindo huu ulifanyika. "Kutokana na upigaji kura wetu, tuna chama cha Republican ambacho kina asilimia 70 ya wazungu na Wakristo, na chama cha Democratic ambacho ni robo tu ya wazungu na Wakristo."
Kulingana na uchunguzi wa PPRI wa watu wazima 5,027, wapiga kura wa kiinjili wa wa Kiprotestanti walikuwa wafuasi wakubwa wa Trump dhidi ya Harris kwa 72% hadi 13%. Wapiga kura Wakatoliki Wazungu pia walimuunga mkono Trump, huku 55% wakimuunga mkono na 34% wakiambatana na Harris. Waprotestanti weupe "wakubwa" wasio wainjilisti walionyesha mgawanyiko sawa.
Kwa kulinganisha, 78% Waprotestanti weusi walimuunga mkono Harris huku 9% tu walimuunga mkono Trump, kulingana na utafiti huo. Wafuasi wa Harris pia walijumuisha Wayahudi-Wamarekani, wasio na uhusiano wa kidini na Wamarekani wengine wasio Wakristo, kulingana na PPRI.
Ilipofikia kura halisi, kulikuwa na dalili za kuondoka kutoka kwa mifumo inayojulikana.
Matokeo kutoka Michigan yalionyesha mwelekeo wa wazi kuelekea Chama cha Republican na wapiga kura Waislamu katika jimbo hilo, huenda ikawa ni matokeo ya jukumu la utawala wa Biden katika kuisaidia Israel katika vita vyake huko Gaza.
Uchambuzi pia unaonyesha kuwa Wakatoliki wengi wa Latino walimpigia kura Trump kuliko ilivyotarajiwa, wakati hapo awali walikuwa na mwelekeo wa kuegemea chama cha Democratic.
Matatizo ya kiuchumi yanayoletwa na mfumuko wa bei unaoongezeka, miongoni mwa mambo mengine, huenda yalisababisha wapiga kura "wasio wa kawaida" wa Republican kujitokeza kumpigia kura Trump.
Kuhusu wito wake kwa Wakristo wa mapokeo, Dk Jones anahoji kwamba kumekuwa na kipengele cha imani katika wazo la "Kuifanya Amerika kuwa Kubwa Tena", kwa ahadi ya kurejesha tabia ya Kikristo ya nchi.
"Yake imekuwa kampeni ya manung'uniko na hasara na kutamani," anabisha Dk Jones, "na hiyo inajumuisha kutamani kutoka kwa mtazamo wa imani."
Mustakabali wa dini Marekani
Pamoja na nguvu zake zote za kisiasa, jambo moja ambalo Trump hawezi kufanya ni kuzuia wimbi la mabadiliko ya idadi ya watu nchini Marekani - ikiwa ni pamoja na kuondoka kwa imani.
Ingawa idadi ya wanaojitambulisha kama "wasioamini Mungu" inasalia kuwa chini nchini Marekani kuliko katika nchi nyingi za Magharibi, wale wanaosema "hawana uhusiano wa kidini" inaongezeka.
Kuna kipengele cha kizazi kwa hilo, pamoja na mielekeo iliyozoeleka ya uchumi wa kibinafsi ikimaanisha kuwa watu wana uhuru mkubwa wa kujitenga na kanuni zinazokubalika katika jamii zao. Lakini kuna sababu zingine pia.
Theluthi moja ya Wamarekani wasioamini kuwa kuna Mungu au wanaoamini kwamba Mungu hayuko wanasema walijitenga na dini yao ya utotoni kwa sababu ya kashfa za unyanyasaji wa Kanisa, kulingana na utafiti wa PPRI.
Mnamo mwaka wa 2020, Kanisa Katoliki lilitoa orodha ya makasisi walio hai nchini Marekani waliopatikana na tuhuma za unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na wengine wanaohusishwa na ponografia ya watoto na ubakaji. Kulikuwa na majina karibu 2,000.
Miaka miwili baadaye, mkutano wa Southern Baptist Conference wa Makanisa ya Kiprotestanti ya Marekani ilitoa orodha ya mamia ya viongozi wa Kanisa walioshutumiwa kwa unyanyasaji wa watoto kati ya 2000 na 2019.
Inaonyesha ukubwa wa suala ambalo Trump analikabili. Walakini, Franklin Graham ana matumaini.
"Mahudhurio ya kanisa hayataongezeka wiki ijayo kwa sababu Rais Trump amechaguliwa - lakini ninachofikiri inamaanisha ni kwamba sheria ambayo tunaweza kuwa tumeona ikija kwa njia ambayo ingeifanya iwe vigumu sana kwa watu wa imani,waje sasa,” anasema, akirejelea wazo la sheria inayoendelea zaidi, kwa mfano, uavyaji mimba na haki za watu wa mapenzi ya jinsia moja na mabadiliko kama hayo.
“Atalinda watu wa imani, atalinda uhuru wa kidini katika nchi hii. Sizungumzii tu kuhusu uhuru wa kidini wa Kikristo… [lakini] watu wote wa imani.”
Kuhusu kama yuko sahihi, Wamarekani wanaweza tu kutazama na kusubiri. Lakini kama vile wengine wanavyofurahia ahadi ya utawala unaoongozwa na Ukristo, wengine bila shaka wana wasiwasi.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah