Syria ina uhuru baada ya Assad, je utadumu?

    • Author, Lina Sinjab
    • Nafasi, Middle East Correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Asubuhi ya tarehe 8 mwezi Disemba mwaka jana 2024, nilisubiri kwa hamu na hamumu mpakani Lebanon nikitumai kuingia Syria pindi lango la mpaka litakapofunguliwa nisichojua ni kipi nitakutana nacho.

Bashar al Assad ambaye alikuwa Rais wa Syria kwa miaka 24 alikuwa ameng'atuliwa madarakani.

Wapiganaji wa upinzani walikuwa wameteka miji mikuu kama vile Aleppo.

Sikutarajia kukiona nilichokishuhudia, Syria ilikuwa huru.

Kama vile raia wengi wa Syria walikuwa wamezoea nchi yao chini ya utawala wa Assad pamoja na babake Hafez aliyekuwa madarakani tangu 1971 hadi 2000.

Maisha chini ya utawala wa familia ya Assad ilimaanisha ni miaka 50 ya watu kupotea katika hali tatanishi na uhalifu wa kivita ulioanza mwaka 2011 uliosababisha hasara na mamia ya maelfu ya watu kupoteza maisha.

Niliwahi kukamatwa na kuzuiliwa mapema wakati vita vilipoanza na kushuhudia wanaume wakipigwa na vilio vya kudhulumiwa.

Hata baada ya kuondoka nchini humo mwaka 2013 niliarifiwa kuwa maafisa wa usalama walivamia nyumba yangu iliyoko Damascus na kuharibu mali yangu.

Nilijua kuwa nimepoteza nchi yangu mara ghafla mwaka jana serikali iliyojaa udikteta iliondolewa madarakani.

Nikirejea nchini sikuwa na hofu ya kukamatwa wala kufuatiliwa nilichokishuhudiwa ni wapiganaji wa upinzani wakisherehekea mitaani huku wenyeji wakiwalaki kwa mbwembwe nilitamani kucheka lakini machozi ya furaha yalinitiririka.

Kwa wiki kadhaa, katika uwanja wa Ummayad ulioko Damascu uligeuka kuwa eneo la sherehe.

Si wazee si watoto walizungumzia siasa bila uoga na mustakabali wa Syria haukukosekana kwenye vikao vya mazungumzo huku watu wakiendelea na shughuli za kawaida.

Haya yote hayangejitokeza katika kipindi cha Assad, Wasyria hawangeandamana kwa hofu ya kupotezwa au kudhibitiwa vikali.

Hata hivyo imekuwa mwamko mpya kwa nchi hii hasa uhuru wa umma kumeanza kuibuka wasiwasi kuhusu demokrasia itakavyotekelezwa na pia jukumu la dini ya kiislamu katika kusuka utawala mpya.

Je uhuru wa umma utaendelea au kama baadhi wanavyohofia uhuru huo utafutiliwa mbali nakuzikwa kwa kaburi la sahau.?

Pia unaweza kusoma:

Raia waliokuwa uhamishoni warejea

Katika mkahawa wa Rawda ulioko katikati mwa mji wa Damascus mkabala na bunge la taifa wasomi hukutana wakipiga soga huku wakivuta shisha na kujadili kuhusu utamaduni.

Wakati wa Assad wanaharakati wa siasa walikuwa wakibebwa hobela hobela na kukamatwa wakati wa mazungumzo.

Ilidaiwa kulikuwa na vibaraka wa utawala ambao walikuwa wakifanya kazi katika mkahawa huo wakiwatonya serikali kilichokuwa kikijadiliwa.

Leo hii mambo yamebadilika.

Mkahawa huo ni wa burudani na vikao vya kijamii.

Watu mashuhuri ambao walikuwa wamekimbia nchi sasa wamerejea huku baadhi wakikaribishwa kwa muziki usioisha.

Mwanahabari wa Syria Mohammad Ghannam ni mmoja wao.

Ananieleza kuwa aliwahi kuzuiliwa katika gereza wakati wa utawala wa Assad na alipoachiliwa aliondoka na kuelekea Ufaransa: na kwasasa anafurahia kurejea nchini kwao.

"Nadhani kila mtu anayeweza kurejea, anapaswa kurejea kuijenga upya nchi," anatangaza. "Kuna dirisha la kufanya chochote unachotaka sasa ikilinganishwa na kabla ya tarehe 8 Desemba 2024."

Akitafakari yaliyopita, anaongeza: "Hata viongozi wa kidini misikitini walihitaji kupata kibali na kujua watakachohubiri. [Sasa] ni bure kabisa. [Kwenye] Swala ya Ijumaa Imam alikuwa anazungumzia jinsi uhuru wako wa kibinafsi haupaswi kukanyaga uhuru wa watu wengine."

Odai al-Zobi pia amerejea nchini Syria hivi karibuni baada ya miaka 14 - aliondoka kwenda kusoma lakini anasema hakuweza kurejea hapo awali kwa sababu alikuwa mwanaharakati na kuikosoa serikali.

"Vitabu vyangu vilipigwa marufuku hapa," ananiambia. "Sasa hakuna udhibiti, unaweza kusoma chochote unachotaka. Nilishangaa sana kwamba watu wengi wanataka kusoma na kutaka kujua zaidi."

"Haya ni mabadiliko makubwa," anakubali Ali al-Atassi, mtayarishaji filamu wa Syria na mtoto wa Rais wa zamani wa Syria Noureddine al-Atassi. (Baba yake aliondolewa madarakani katika mapinduzi na Hafez al-Assad.)

"Ilibadilisha sheria za mchezo, na kufungua mitazamo mingi kwa nchi."

Kulinda sanaa na usanii

Mandhari ya sanaa na utamaduni ya Syria kwa muda mrefu imekuwa chanzo cha fahari ya nchi hiyo: Assads waliiunga mkono, wakitaka kuwasilisha utamaduni tajiri kwa ulimwengu lakini baadhi ya wasanii na waandishi waliuawa kwa maoni yao kuhusu utawala huo.

Hata kubeba vitabu fulani kuliwahi kuwa sababu ya kukamatwa.

Leo, hata hivyo, kila aina ya vitabu vinaonyeshwa kwenye maduka karibu na mji mkuu - hata majina ya kisiasa.

Vilabu vya sinema huonyesha filamu ambazo hapo awali zilipigwa marufuku pia.

Kwa wiki baada ya kuanguka kwa Assad, serikali iliyochukua usukani haikuteua Waziri wa Utamaduni lakini wasanii na wataalam wa sanaa walijikusanya na kulinda sekta hiyo.

Japokuwa hakuna pingamizi ya sanaa inayochezwa majukwaani kuna wasiwasi huenda viongozi wa kidini wakabadilisha mkondo nakutaka kuzuia baadhi ya maudhui ambayo wanayataja hayalingani na misingi ya dini.

Hakuna ushahidi wa wazi wa hili.

Dk Maher Al Sharaa, kaka wa Rais wa mpito, ameonekana kwenye Jumba la sanaa la jiji hilo akiwa na familia yake; Vivaldi ilichezwa na wanamuziki wa Syria.

"Ni vyema kupata fursa hii kuzungumza miongoni mwetu kuhusu jinsi ya kulinda na kuunga mkono eneo la sanaa nchini Syria," anasema Noura Murad, mwandishi wa chore.

Bw al-Atassi pia anachagua kuwa na matumaini. "Ninaamini Wasyria hawataruhusu utawala huu kuingia katika maisha yao ya kibinafsi, kuunda sheria za jinsi ya kuishi katika nafasi ya umma."

Nguvu ya mamlaka

Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, ambaye aliongoza mashambulizi ya waasi yaliyomwondoa madarakani Bashar al-Assad, aliteuliwa rasmi na Baraza la Kijeshi mnamo tarehe 29 Januari.

Katika hotuba yake ya kuapishwa, alisisitiza kwamba kipaumbele cha taifa ni "kujaza pengo la uongozi kwa njia halali na ya kisheria."

Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye, wasiwasi umeanza kuibuka miongoni mwa baadhi ya wananchi na wadau wa kisiasa kuhusu uwezekano wa kuanzishwa kwa demokrasia endelevu nchini humo.

Kwa sasa, hakuna mfumo rasmi wa kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi, wakiwemo wale wa juu kama Rais, hadi katiba ya kudumu itakapopitishwa na uchaguzi wa kidemokrasia kufanyika.

"Hadi sasa, utawala haujaonesha utayari wa kushirikiana madaraka na kuruhusu vikundi vingine vya kisiasa na kijamii kushiriki katika ujenzi wa taifa," anadai Bw. Al-Atassi.

"Bila kufungua uwanja wa kisiasa kwa wadau mbalimbali, sidhani kama Rais Sharaa ataweza kuirejesha Syria katika hadhi yake ya kimataifa."

Mnamo mwezi Februari, mamia ya raia walikusanyika katika Jumba la Umma mjini Damascus kushiriki mdahalo wa kitaifa wa siku mbili uliohusu mustakabali wa Syria.

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji walieleza kuwa kikao hicho kilipangwa kwa haraka na kilikuwa kifupi mno kuweza kushughulikia kwa kina masuala muhimu ya taifa.

Kwa mujibu wa Abdulhay Sayed, mtaalamu wa sheria kutoka Syria na mshirika mkuu katika kampuni ya uwakili ya Sayed and Sayed, mdahalo huo haukuwa wa uwakilishi mpana, wala haukuakisi maoni ya pamoja ya taifa.

Rais Ahmed al-Sharaa, ambaye awali alikuwa kiongozi wa Hayat Tahrir al-Sham (HTS) – kundi lililokuwa mshirika wa zamani wa al-Qaeda na lililotawala muungano wa waasi – ametangaza waziwazi dhamira yake ya kujenga taifa lenye "uchaguzi huru na wa haki."

Ingawa kuna juhudi za kuonyesha uwakilishi mpana katika serikali mpya ya Syria, baadhi ya uteuzi bado umeacha maswali mengi.

Miongoni mwa walioteuliwa ni mwanamke wa dini ya kikristo aliyekabidhiwa wizara ya masuala ya kijamii, pamoja na mkuu wa kikundi cha uokoaji cha White Helmets, ambaye sasa anasimamia wizara ya dharura na majanga.

Lakini si wote walioona uteuzi huu kama hatua ya kweli ya mabadiliko.

Uamuzi wa kumteua kaka wa Rais Sharaa kuwa mkuu wa masuala ya urais umeibua hisia juu ya dhana ya upendeleo wa kifamilia.

"Viongozi wa zamani wa ngazi za juu kutoka kundi la HTS sasa wanashikilia nyadhifa nyeti za kiserikali," anaeleza Bw. Sayed kwa tahadhari.

Naye Bw. Al-Atassi anazidi kutoa changamoto kwa serikali mpya, akisema, "Wataalamu wa sheria za kimataifa wenye sifa za kipekee hawakushirikishwa katika Baraza la Mawaziri – walipuuzwa kana kwamba ujuzi wao hauna nafasi katika taifa jipya."

Uteuzi mwingine unaozua maswali ni ule wa Waziri wa Sheria, ambaye ana shahada katika sheria ya Sharia, lakini hana ujuzi katika Kanuni ya Kiraia ya Syria mfumo wa sheria unaotegemea sana misingi ya Kifaransa na ya Milki ya Kiosmani.

Hii imechochea mjadala: je, Syria inajiandaa kuhamia kwenye mfumo wa sheria za kidini badala ya sheria za kiraia?

"Hadi sasa, hakuna dalili za wazi kwamba serikali mpya inataka kubadili sheria zilizopo na kuanzisha sheria zinazoongozwa na Sharia," anabainisha Bw. Sayed. "Lakini bado ni eneo tunalolifuatilia kwa karibu."

Hofu kubwa kwa sasa, anasema, si tu aina ya sheria zitakazotumika, bali ni iwapo uhuru wa mahakama ambao umekuwa ukikandamizwa kwa miaka mingi utaweza kurejeshwa, na zaidi ya yote, kulindwa kwa dhati.

Uhuru wa wanawake na dini

Wizara ya Sheria imeanza kutekeleza utaratibu wa kutenganisha wanaume na wanawake katika maeneo ya kuingilia, na kumekuwa na ripoti kuhusu wanaume wanaogawa vijikaratasi katika mabasi na katika Msikiti wa Umayyad jijini Damascus, wakihimiza wanawake kuvaa vazi la hijabu ya uso mzima (nikabu).

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya Uislamu wameeleza wasiwasi wao. Damascus imejulikana kwa kuvumiliana kidini, lakini kuna hofu inayozidi kuongezeka kwamba mamlaka mpya zinatoka katika msingi wa ushawishi wa kisalafi — mtazamo wa Uislamu unaojikita katika usafi wa itikadi na ufuasi mkali wa mafundisho ya awali ya Sunni.

"Kuna wito unaozidi kushika kasi wa kurejea kwenye maadili ya kidini," anasema Bw. Sayed. "Hili ni changamoto kubwa kwa wale wanaoamini katika demokrasia, utawala wa sheria, na usawa wa uraia."

Hata hivyo, Husam Jazmati, msomi wa Syria ambaye anafanya utafiti kuhusu harakati za Kiislamu katika taasisi ya utafiti wa jamii ya kiraia iitwayo Impact, anadai kuwa Sharaa "anapinga harakati zote — za Kiislamu na zisizo za Kiislamu — na wala hana nia ya kuanzisha dola ya Kiislamu, wala haamini jambo hilo linawezekana."

Na Qur'ani inasema wazi: ''Hakuna kulazimisha katika dini."

Mvutano kuhusu mustakabali Syria

Hivi sasa, ghasia katika ukanda wa Syria umesababisha zaidi ya watu 1,400 kufariki wengi wao wakiwa ni jamii ya Waalawite jamii ambayo Rais Assad aliyotoka.

Vurugu hizi zinasemekana kuwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya Syria.

Swali kuu sasa linahusu jinsi WaSyria wanavyotazama mustakabali wao.

Migongano imeibuka kati ya viongozi wa sasa na kundi la HTS, kulingana na Bw. Jazmati.

Anasema kuwa viongozi wa serikali ya Sharaa wanataka kujenga taifa la "kiadili na lenye uchumi huria," lakini hawawezi kuzuiya wanachama wao wengi kutoka kujaribu kulazimisha maisha ya Kiislamu katika jamii ya Syria.

Taasisi ya International Crisis Group pia ina wasiwasi kuhusu hali ya Syria, ikisema kuwa nchi inaishi kwa "muda wa mkopo''.

Serikali ya mpito inakutana na changamoto za kifedha, vyombo vya usalama vimelemewa, umasikini unazidi, na uasi unazidi kuibuka.

Vikwazo vya Magharibi vinawanyima viongozi rasilimali muhimu za kujenga upya nchi.

Kwa Bw. Al-Atassi, suluhu ni rahisi: Anaamini kuwa Sharaa anapaswa kufungua nafasi ya kisiasa kwa wote. "Hakuna uchaguzi nchini Syria leo; kilichopo ni uteuzi tu," anasema. "Hii ni hatari kubwa."

Kuhusu demokrasia ya kudumu, Al-Atassi anasema, "Tunahitaji kusubiri kuona, lakini sina matumaini."