Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wasyria wanaotaka Syria mpya bila Urusi
- Author, Grigor Atanesian
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kwa miaka mingi Urusi na Syria zilikuwa washirika wakubwa - Moscow iliweka kambi za kijeshi za anga na baharini huko Mediterania huku Damascus ikipata msaada wa kijeshi kwa mapambano yake dhidi ya vikosi vya waasi.
Baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad, Wasyria wengi wanataka kuona majeshi ya Urusi yakiondoka lakini serikali yao ya mpito inasema iko tayari kwa ushirikiano zaidi.
"Uhalifu wa Urusi hapa ulikuwa hauelezeki," anasema Ahmed Taha, kamanda wa waasi huko Douma, maili sita kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Damascus.
Mji huo hapo zamani ulikuwa mahali penye mafanikio na Ahmed Taha aliwahi kuwa raia wa kawaida, akifanya kazi kama mfanyabiashara, kabla ya kuchukua silaha dhidi ya utawala wa Assad, kufuatia ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya mwaka 2011.
Wilaya nzima ya Douma sasa ni magofu baada ya mapigano makali katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14 nchini Syria.
Moscow iliingia katika mzozo huu mwaka 2015 ili kuunga mkono serikali. Na Moscow inadai ilifanya majaribio ya silaha 320 tofauti nchini Syria.
Pia ilikodi kwa miaka 49 kambi mbili za kijeshi kwenye pwani ya Mediterania - kambi ya wanamaji ya Tartus na kambi ya anga ya Hmeimim. Hii iliiruhusu Kremlin kupanua ushawishi wake barani Afrika, na kufanya operesheni Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, na Burkina Faso.
Licha ya kuungwa mkono na Urusi na Iran, Assad hakuweza kuzuia utawala wake kutoporomoka. Na Moscow imetoa hifadhi kwake na familia yake.
"Warusi walikuja katika nchi hii na kuwasaidia wadhalimu na wavamizi," anasema Abu Hisham, alipokuwa akisherehekea kuanguka kwa utawala wa Assad huko Damascus.
Kremlin daima imekuwa ikikanusha kufanya uhalifu, ikisema ililenga tu makundi ya wanajihadi kama IS au al-Qaeda. Lakini Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yanaishutumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita.
Mwaka 2016, wakati wa shambulio katika eneo lenye wakazi wengi Mashariki mwa Aleppo, vikosi vya Syria na Urusi vilifanya mashambulizi ya anga, "yakigharimu mamia ya maisha na kushambulia hospitali, shule na masoko," kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Huko Aleppo, Douma na kwingineko, vikosi vya serikali vilizingira maeneo yanayodhibitiwa na waasi, na kuzuia chakula na vifaa vya dawa, na kuendelea kushambulia kwa mabomu hadi makundi yenye silaha yalipojisalimisha.
Urusi pia iliingia katika makubaliano ya kusitisha mapigano na mikataba ya kujisalimisha katika miji inayoshikiliwa na waasi, kama vile Douma mwaka 2018.
Ahmed Taha alikuwa miongoni mwa waasi waliokubali kujisalimisha ili kupata njia salama ya kutoka nje ya mji huo kufuatia mzingiro wa miaka mitano wa jeshi la Syria.
Alirejea Douma mwezi Desemba kama sehemu ya waasi wanaoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) na kiongozi wake Ahmed al-Sharaa.
"Tumerejea nyumbani." Hana shaka kwamba vikosi vya Urusi vinapaswa kuondoka: "Kwetu, Urusi ni adui."
Ni hisia inayoungwa mkono na watu wengi tunliozungumza nao.
Hata viongozi wa jumuiya za Kikristo nchini Syria, ambao Urusi iliapa kuwalinda, wanasema hawakupata usaidizi kutoka Moscow.
Katika mji wa Bab Touma, mji wa kale wa Kikristo huko Damascus, Patriaki wa Kanisa la Kiorthodoksi la Kisiria anasema: "Hatukuona Urusi au mtu mwingine yeyote kutoka ulimwengu wa nje kutulinda."
"Warusi walikuwa hapa kwa manufaa na malengo yao," anasema Ignatius Aphrem II. "Walipokuja mwanzoni, walisema: 'Tulikuja hapa kutoa msaada,'" anasema mtu anayeitwa Assad. "Lakini badala ya kutusaidia, waliiangamiza Syria zaidi."
Urusi itaondoka au itabaki?
Sharaa, ndiye kiongozi wa sasa wa Syria, alisema katika mahojiano na BBC mwezi uliopita kwamba haondoi uwezekano wa kuwaruhusu Warusi kusalia, na alielezea uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuwa wa "kimkakati."
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Lavrov kwa upande wake alisema, Urusi "ina mambo mengi ya kufanana na marafiki zetu wa Syria."
Uhusiano wa Syria na Urusi
Kujenga upya jeshi la Syria kutahitaji mwanzo mpya au kuendelea kutegemea vifaa vya Urusi, jambo ambalo litamaanisha kuwepo aina fulani ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili, anasema Turki al-Hassan, mchambuzi wa masuala ya ulinzi na jenerali mstaafu wa jeshi la Syria.
Ushirikiano wa kijeshi wa Syria na Moscow ulikuwepo kabla ya utawala wa Assad, Hassan anasema. Karibu vifaa vyote vilivyopo vilitengenezwa na Muungano wa Sovieti au Urusi, anaeleza.
"Tangu kuanzishwa kwake, jeshi la Syria limekuwa na silaha za Kambi ya Mashariki."
Kati ya 1956 na 1991 Syria ilipokea vifaru 5,000, ndege za kivita 1,200, meli 70 na mifumo mingine mingi na silaha kutoka Moscow zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 26, kulingana na makadirio ya Urusi.
Ilikuwa ni kuunga mkono vita vya Syria dhidi ya Israel, ambayo kwa kiasi kikubwa ni sera ya mambo ya nje ya taifa hilo tangu lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1946.
Zaidi ya nusu ya kiasi hicho kiliachwa bila kulipwa wakati Muungano wa Kisovieti ulipoanguka lakini mwaka 2005 rais Putin alifuta 73% ya deni hilo.
Vassily Nebenzia, mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Moscow, amesema matukio ya hivi karibuni yanaashiria awamu mpya katika historia ya "watu wa Syria."
Amesema Urusi itatoa misaada ya kibinadamu na msaada kwa ajili ya ujenzi upya ili kuruhusu wakimbizi wa Syria kurejea nyumbani.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah