Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kuunguzwa na kemikali na kuchomwa moto- Wagaza waiambia BBC kuhusu mateso katika kizuizi cha Israel
Wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na kurudi Gaza wameiambia BBC kwamba walitendewa vibaya na kuteswa mikononi mwa wanajeshi wa Israel na wafanyakazi wa magereza, na kuongeza ripoti za utovu wa nidhamu ndani ya kambi na jela za Israel.
Mtu mmoja alisema alishambuliwa kwa kemikali na kuchomwa moto. "Nilijibwaga kama mnyama katika jaribio la kuzima moto [mwilini mwangu]," alisema Mohammad Abu Tawileh, mwenye umri wa miaka 36.
Tumefanya mahojiano ya kina na wafungwa watano walioachiwa huru, ambao wote walikamatwa huko Gaza katika miezi kadhaa baada ya Hamas na vikundi vingine kuua takribani watu 1,200 huko Israeli na kuwachukua mateka 251.
Wanaume hao walizuiwa chini ya Sheria ya Wapiganaji Haramu ya Israeli, hatua ambayo watu wanaoshukiwa kuhatarisha usalama wanaweza kuzuiliwa kwa muda usiojulikana bila kufunguliwa mashtaka, huku Israeli ikipanga kuwaokoa mateka na kusambaratisha kundi la kigaidi lililopigwa marufuku.
Watu hao wanasema walishutumiwa kuwa na uhusiano na Hamas na walihojiwa kuhusu eneo la mateka na vichuguu, lakini hawakubainika kuhusika na mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023, hali ambayo Israel ilikuwa imeweka kwa yeyote aliyeachiliwa chini ya makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano.
Baadhi ya walioachiliwa chini ya mkataba huo walikuwa wakitumikia vifungo kwa makosa mengine makubwa, ikiwa ni pamoja na mauaji ya Waisraeli, lakini haikuwa hivyo kwa waliohojiwa. Pia tuliuliza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) na Jeshi la Magereza la Israel (IPS) kama kulikuwa na hatia yoyote au shutuma dhidi ya wanaume hao lakini hawakujibu swali hilo.
Katika ushuhuda wao:
- Kila mmoja anaelezea jinsi alivyovuliwa nguo, kufungwa macho, kufungwa mikono na kupigwa.
- Wengine wanasema walipigwa na mshtuko wa umeme, walitishiwa mbwa, na kukataliwa huduma za matibabu.
- Wengine wanasema walishuhudia vifo vya mahabusu wengine.
- Mmoja anasema alishuhudia unyanyasaji wa kingono.
- Mwingine anasema kichwa chake kilitumbukizwa kwenye kemikali na mgongo wake ukawashwa kwa moto.
Tumekutana na ripoti za wakili aliyemtembelea mmoja wa wanaume hawa jela, na tumezungumza na wafanyakazi wa kitababu waliowatibu baadhi yao waliporejea.
BBC ilituma barua ndefu kwa IDF ambayo ilielezea kwa kina madai ya wanaume hao na majina yao.
Katika taarifa yake, IDF haikujibu madai yoyote, lakini ilisema "inakanusha kabisa madai ya unyanyasaji wa kimfumo dhidi ya mahabusu".
Ilisema baadhi ya kesi zilizotolewa na BBC zitachunguzwa na mamlaka husika. Iliongeza kwamba nyingine "zililetwa bila maelezo ya kutosha, bila maelezo yoyote kuhusu majina ya mahabusu, na kuifanya iwe vigumu kuchunguza."
Iliongeza: "IDF inachukulia kwa uzito hatua yoyote inayoenda kinyume na maadili yake... Malalamiko maalum kuhusu tabia isiyofaa ya wafanyakazi wa kituo cha mahabusu au hali zisizoridhisha, hupelekwa kwa ajili ya uchunguzi na mamlaka husika na kushughulikiwa ipasavyo.
IPS ilisema haikuwa na habari kuhusu madai yoyote ya unyanyasaji yaliyotajwa katika uchunguzi wetu, katika magereza yake. "Hakuna matukio kama hayo yaliyotokea chini ya jukumu la IPS," iliongeza.
Dr. Lawrence Hill-Cawthorne, mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bristol, alisema matibabu ambayo wanaume walielezea "hayana ulinganifu na sheria za kimataifa na sheria za Israeli."
"Chini ya sheria za kimataifa, sheria ya migogoro ya silaha inakuhitaji kuwatendea wafungwa wote kwa utu," alisema. "Majukumu yanayohusiana na mahitaji ya msingi ya wafungwa hayaathiriwi na madai yoyote ya makosa."
Wapalestina watano walihojiwa kwa undani walirejeshwa mapema mwaka huu chini ya makubaliano ya usitishaji vita na Hamas, kundi lililohusika na mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.
Walikuwa miongoni mwa takribani wafungwa na mahabusu 1,900 wa Kipalestina waliobadilishana na mateka 33 wa Kiebrania, wanane wakiwa wamekufa na 25 wakiwa hai, baadhi yao wakiwa wameelezea kunyanyaswa, kukosa chakula na kutishiwa na watekaji.
Mateka wa kike waliorejeshwa awali wameelezea mashambulizi ya kimwili na kingono wakiwa katika kizuizi.
Israel inasema uchunguzi unaonesha baadhi ya mateka waliokufa waliorudishwa, wakiwemo watoto, waliuawa na Hamas, ingawa kundi hilo linakanusha hili.
Wote watano kati ya waliorejeshwa waliokuwa mahabusu wa Kipalestina walielezea maelezo ya kufanana kuwa walikamatwa Gaza, kisha kupelekwa Israel kupekuliwa katika kambi za kijeshi kabla ya kuhamishiwa jela, na hatimaye kurudi Gaza miezi kadhaa baadaye.
Walisema walinyanyaswa katika kila hatua ya mchakato huu.
Zaidi ya wafungwa kumi waliorejeshwa, ambao BBC iliwasiliana nao kwa muda mfupi walipofika nyumbani Gaza, pia walielezea mateso, njaa na magonjwa.
Haya, kwa upande mwingine, yanaendana na ushuhuda uliotolewa na wengine kwa shirika la haki za binadamu la Israeli B'Tselem na Umoja wa Mataifa, ambalo mnamo Julai lilielezea ripoti kutoka kwa waachiwa waliorejea wakielezea kwamba walivuliwa nguo, kunyimwa chakula, usingizi na maji, walipigwa na umeme na kuchomwa na sigara, na mbwa waliwekwa dhidi yao.
Ripoti zaidi kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita ilirekodi kesi za ubakaji na unyanyasaji wa kingono, na kusema kuwa kutumia hili kama tishio ilikuwa "taratibu za kawaida" kwa IDF. Israel ilijibu kusema inakanusha vikali madai yasiyo na msingi.
Kwa kuwa Israel haikubali kuwaruhusu waandishi wa habari wa kimataifa kufikia Gaza kwa uhuru kwa sasa, mahojiano yetu yalifanywa kwa simu na ujumbe wa maandishi, na pia kwa ana kwa ana na waandishi wetu wa kujitegemea walioko katika eneo hilo.
Wanaume watano walitufahamisha kwamba mateso yao yalianza wakati wa kukamatwa kwao, walisema walivuliwa nguo, kufungwa macho na kupigwa.
Mhudumu wa magari, Mohammad Abu Tawileh, alituambia kwamba aliteswa kwa siku kadhaa.
Alieleza kwamba alichukuliwa na wanajeshi hadi jengo lisilokuwa mbali na mahali alikokamatwa mnamo Machi 2024, na kushikiliwa katika chumba, akiwa ndiye mahabusu pekee hapo, kwa siku tatu za uchunguzi na wanajeshi.
Onyo: Picha hapa chini ni za kuogofya
Askari walichanganya kemikali zinazotumika kusafishia kwenye sufuria, alituambia, na kuingiza kichwa chake ndani yake. Kisha waliomhoji walimpiga ngumi, alisema, na akaanguka kwenye sakafu iliyojaa vifusi, na kumjeruhi jicho. Alisema kisha walimfunika jicho kwa kitambaa, ambacho alisema "kilichozidisha jeraha lake".
Pia walimuunguza moto, alituambia.
"Walitumia ' Air freshner' na kibiriti kuuwasha moto mgongo wangu. Nilijibwaga mithili ya mnyama nikijaribu kuzima moto huo.
Ulienea kutoka shingoni hadi miguuni. Kisha, walinipiga mara kwa mara na sehemu za vitako vya bunduki zao, na walikuwa na fimbo, ambazo walizitumia kunipiga na kunichoma ubavu," alisema.
"Walinimwagia kichwani, na kunidondokea mwilini mwangu nikiwa nimekaa kwenye kiti."
Hatimaye, alisema askari walimmwagia maji mwilini, na kumfukuza hadi Israel ambako alipatiwa matibabu hospitalini, ikiwa ni pamoja na kupandikizwa ngozi.
Wakati BBC ilipomhoji Bw Abu Tawileh muda mfupi baada ya kuachiliwa, mgongo wake ulikuwa umefunikwa na madoa mekundu. Maumivu ya mabaki ya kuungua kwake bado yalimuamsha, alisema, na uoni wake ulikuwa umeathiriwa.
BBC haikuweza kuzungumza na mtu yeyote aliyeshuhudia kushambuliwa kwa Bw Abu Tawileh, lakini daktari bingwa wa macho ambaye alimtibu aliporejea Gaza alithibitisha kuwa alichomwa na kemikali jichoni, na kuharibu ngozi karibu na jicho hilo.
Tulionyesha picha za majeraha yake na kutoa maelezo ya ushuhuda wake kwa madaktari kadhaa wa Uingereza, ambao walibaini kuwa kulikuwa na mapungufu kwa kile waliweza kutathmini kwa kutazama picha.
BBC ilitoa maelezo ya kina ya maelezo hayo kwa kwa IDF, na kuipa siku tano kufanya uchunguzi.
Haikujibu madai ya Bw Abu Tawileh moja kwa moja lakini ilisema itachukua hatua.
Ilisema "itachunguza" baadhi ya kesi, lakini haikujibu maswali ya kufuatilia kama hii iliyomjumuisha Bw Abu Tawileh.
Wanaume watatu kati ya tuliozungumza nao walidai kuwa mbwa walitumiwa kuwatisha wafungwa huko Sde Teiman na vituo vingine.
"Tulikuwa tukipigwa walipokuwa wakituchukua kutoka kwenye kambi hadi kwenye zahanati ya matibabu au chumba cha kuhojiwa , walituwekea mbwa, wakatufunga kamba," alisema Bw Abu Tawileh ambaye alizuiliwa katika ngome hiyo, na pia kutibiwa humo.
BBC iliitaka IDF kujibu madai kuwa ilitumia mbwa mara kwa mara kuwatisha na kuwashambulia wafungwa. Ilisema: "Matumizi ya mbwa kuwadhuru wafungwa ni marufuku."
Pia ilisema kuna "magaidi wenye uzoefu wanaochukuliwa kuwa hatari sana kati ya wafungwa wanaozuiliwa katika vituo vya kizuizini vya IDF" na kwamba "katika kesi za kipekee kuna wafungwa wa muda mrefu wa kufungwa kwa pingu wakati wakiwa kizuizini".
Shirika la Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), ambalo linafanya mahojiano na wafungwa wanaorejea, lilisema haliwezi kuzungumzia hali za watu binafsi kutokana na wasiwasi wa faragha.
Iliongeza kuwa ilikuwa na hamu ya kupewa fursa ya kuwafikia wale ambao bado wanazuiliwa, jambo ambalo halijaruhusiwa tangu mashambulizi ya Oktoba 7.
"ICRC inasalia na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya wafungwa na inasisitiza haja ya dharura ya kuanza tena kutembelea maeneo yote ya kizuizini. Tunaendelea kuomba ufikiaji katika mazungumzo ya pande mbili na ya siri na wahusika," iliiambia BBC.
Mateka 59 bado wanazuiliwa huko Gaza, 24 kati yao wanaaminika kuwa hai. ICRC haijawahi kupewa idhini ya kuwafikia katika miezi 18 wakiwa utumwani, na wapendwa wao wana wasiwasi mkubwa juu ya ustawi wao.
Kwa wengi wa wafungwa wa Kipalestina walioachiwa huru, kurejea Gaza ilikuwa ni wakati wa kusherehekea.
Bw Abu Tawileh alisema familia yake ilishtushwa na mwonekano wake alipoachiliwa, na kuongeza kuwa bado aliathiriwa na yale aliyoyapitia.
"Siwezi kufanya chochote kwa sababu ya jeraha langu, kwa sababu jicho langu linauma, na linatoka machozi na kuhisi kuwashwa, na vidonda vya kuchomwa kwenye mwili wangu. Hii inanisumbua sana," alisema.
Kijana Ahmed alisema sasa anataka kuondoka Gaza.
"Nataka kuhama kwa sababu ya mambo tuliyoyaona kizuizini, na kwa sababu ya mateso ya kiakili ya kuogopa mabomu yakianguka kwenye vichwa vyetu. Tulitamani kifo lakini hatukuweza kukipata."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga