Je, unaweza kununua eneo mwezini?

Chanzo cha picha, getty Image
Baada ya mafanikio ya chombo cha India cha Chandrayaan-3 kufika mwezini, macho yote yameelekezwa mwezini sasa. Je, binadamu anaweza kuishi mwezini? Oksijeni inapatikana huko? Watu wengi wanauliza maswali hayo katika mtandao.
Kuna ripoti kwamba baadhi ya watu tayari wamenunua maeneo katika mwezi. Ni nani anayeuza maeneo kwenye mwezi? Je, ni halali kununua ardhi kama hii? Wanunuzi wanasema nini? Sheria zinasemaje?
Wanunuzi ni Wengi

Chanzo cha picha, RAAJEEVVV
Mfanyabiashara anayeishi Hyderabad na mnajimu, Rajeev mwenye umri wa miaka 50 ni mmoja wa wale wanaodai kuwa wamenunua eneo kwenye mwezi.
Aliambia BBC - alinunua mahali hapo mwaka wa 2002 kutoka kwa 'The Lunar Registry' yenye makao yake New York. Anasema kuwa alinunua ekari tano za ardhi karibu na eneo la 'Mare Imbrium' mwezini kwa rupia za India 7,000. 'Mare Imbrium' ni eneo liko kaskazini wa Mwezi.
The Lunar Registry ni kikundi cha kimataifa cha wanasheria. Kwenye tovuti ya kampuni hiyo inaeleza kwamba inafanya kazi ya kutafuta makaazi, kufanya utafiti na ubinafsishaji kwenye mwezi.
Rajiv aliiambia BBC jinsi alivyopata wazo la kuinunua eneo. "Miaka 20 iliyopita nilipokuwa nikifanya kazi nilikutana na tangazo kwenye mtandao. Linataja kuuza sehemu kwenye mwezi. Mwanzoni sikuamini. Lakini, baada ya kupata taarifa, nilinunua shamba la ekari tano,'' alisema.
Ameeleza kwa nini aliinunua. "Nilinunua mahali hapo kwani ni pazuri kwa wanadamu. Najua siwezi kwenda huko. Lakini, baada ya miaka 50 au 100, makao ya binadamu yanaweza kuanzishwa. Kisha maeneo yetu yatakuwa na manufaa," alisema.

Chanzo cha picha, RAAJEEVVV
Vilevile Lalit Mohta mwenye umri wa miaka 46, mtaalamu wa kompyuta kutoka Bengaluru, pia alinunua ekari mbili za ardhi mwezini. 2006 alinunua ekari hizo kutoka kwa kampuni ya The Lunar Registry kwa rupia 3000.
Anauita ni uwekezaji wa muda mrefu. Naye aliiambia BBC kwa nini alinunua mahali hapo.
"Najua siwezi kuishi mwezini sasa. Lakini, kwa majaribio kama ya chombo cha Chandrayaan-3, kuna matumaini kwamba makazi yatawezekana katika siku zijazo. Ardhi yetu inaweza kutumika wakati makazi yanaundwa huko."
Naye Rupesh Mason, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 49 kutoka Jammu na Kashmir, hivi karibuni alifichua kwa vyombo vya habari kwamba amenunua mahali kwenye mwezi.
Hadi sasa kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa watu wengi wamenunua maeneo mwezini. Wengi wao wamenunua kutoka kwa The Lunar Registry.
Nani anauza?

Chanzo cha picha, LALIT MOHATA
Jina kamili la kampuni ya The Lunar Registry ni International Lunar Land Registry' (ILLR) - 'Masjala ya Kimataifa ya Ardhi ya Mwezi.' Ilianzishwa mwaka 1999.
ILLR inasema kufikia Julai 2019, watu 3,26,000 duniani kote wamejiandikisha kwa manunuzi ya ekari milioni 1.25 jumla za ardhi kwenye mwezi.
Hata hivyo, kampuni hiyo inaweka wazi kupitia tovuti yake kwamba wao sio wamiliki wa mwezi, bali wanasajili tu madai ya ardhi kwenye mwezi.
BBC iliwasiliana na shirika hilo ili kujua ni kwa msingi gani usajili huo unafanyika. Lakini hakukuwa na majibu kwa barua pepe wala simu hadi muda wa makala haya yanaandikwa.
Sheria zinasemaje?

Chanzo cha picha, getty image
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mataifa Wanachama wa Umoja wa Mataifa yameingia makubaliano juu ya vitu vya anga, ukiwemo Mwezi. Mkataba huo unaoitwa 'Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Kanuni za Anga za Juu' umetiwa saini na zaidi ya nchi 100 ikiwemo India.
“Maliasili zote angani, ukiwemo mwezi, ni mali ya binadamu kwa ujumla. Kifungu cha 2 cha mkataba huo kinasema kwamba, "hakuna nchi itamiliki rasilimali hizi kwa nguvu au kwa njia nyingine yoyote."
Lakini katika makubaliano haya ya 1967, haijasemwa popote kwamba watu binafsi hawana haki ya kumiliki eneo katika mwezi. Kuna ripoti katika vyombo vya habari kwamba mtu mmoja aitwaye Dennis Hope kutoka Amerika aliwahi kutangaza kuuza eneo kwenye mwezi na kupitia mauzo hayo alipata pesa nyingi .
N Raghunandan Kumar, mkurugenzi wa Planetary Society of India, anasema kwamba kununua eneo kwenye mwezi kutoka kwa watu binafsi au mashirika ni kupoteza pesa.
Umoja wa Mataifa unasema kwamba utajiri wa anga ni wa wanadamu wote. “Je, kampuni binafsi au watu binafsi wanawezaje kuuza eneo ambalo ni mali ya binadamu wote?” alihoji.
Manunuzi ya Nyota

Chanzo cha picha, FACEBOOK/MAHESH BABU
N Raghunandan anasema hivi karibuni kulikuwa na ripoti za mashabiki wa mwigizaji wa filamu Mahesh Babu kununua nyota kwa jina lake.
"Iliandikwa kwenye habari kwamba mashabiki wa Mahesh Babu walinunua nyota na kumpa kama zawadi siku yake ya kuzaliwa. Mashabiki wamewahi kutoa zawadi sawa na hiyo kwa Shah Rukh Khan,” anasema Raghunandan.
“Haijasemwa kuwa nchi zilizokanyaga kwanza mwezini zina haki ya umiliki. Kwa hiyo, usajili unaofanywa na mashirika binafsi na watu binafsi hauna uhalali wowote. Huku ni kupoteza pesa," anasema.
Profesa wa anga wa Chuo Kikuu cha Osmania Shanti Priya pia anakubaliana na hoja ya Raghunandan.
"Kulingana na Mkataba wa Kimataifa wa Anga, watu binafsi hawana haki juu ya utajiri wa anga. Ni sawa na nchi. Ni utajiri wa kila mtu,'' alisema.












