Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Raila Vs Ruto: Mawakili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais Kenya
Na Dinah Gahamanyi
BBC Swahili
Makabiliano ya kisiasa nchini Kenya sasa yamehamia mahakamani kufuatia matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 9 Agosti, 2022. Hii ni baada ya mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio La Umoja wa Raila Odinga kupinga ushindi wa Bw William Ruto na hivyo kutangazwa kuwa Rais Mteule na Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC).
Tayari Bw Odinga kupitia mawakili wake amewasilisha kesi yake mahakamani kwa mujibu wa sheria ya katiba ya nchi hiyo.
Makabiliano haya ya kisheria katika mahakama ya juu zaidi nchini Kenya yatashuhudiwa baina ya mawakili maarufu wenye uzoefu kutoka upande wa wagombea Raila Odinga, William Ruto na mawaliki wa tume huru ya uchaguzi IEBC.
Baadhi ya mawakili hao walihusika katika kesi iliyopelekea kufutwa kwa matokeo ya kwanza ya uchaguzi ya mwaka 2017, ambapo hatimaye Bw Uhuru Kenyatta kuwa mshindi, huku Bw Odinga akishindwa.
Lakini je ni mawakili gani maarufu walitakaokabiliana katika kesi hii?
Mawakili wa Odinga
Pheroze Nowroje
Nowrojee amekuwa mwanasheria tangu mwaka 1965 mwaka mmoja baada ya Kenya ipate uhuru wake chini ya Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.
Nowroje alikuwa pia miongoni mwa mawakili waliouwakilisha Muungano wa NASA mnamo mwaka 2017 wakati huo kiongozi wa muungano juo Raila Odinga alipinga ushindi wa uchaguzi wa urais wa rais anayeondoka madarakani sasa Uhuru Kenyatta.
Wakili huyu mwenye umri wa miaka 82 amekuwa mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo kikuu cha Nairobi(UoN), na Chuo cha Sheria cha Kenya (KSL). Wakati mmoja alihudumu kama mhariri wa tathmini ya taarifa za kisheria katika kanda ya Afrika Mashariki.
James Orengo
James Aggrey Orengo ni miongoni mwa mawakili wachache nchini Kenya ambaye ameweza kufikia kiwango cha wakili mwandamizi ‘’Seniour Counsel’’, hadhi aliyoipata wakati wa utawala wa rais wa zamani hayati Mwai Kibaki.
Alifanya kazi muhimu wakati wa muhula wa kwanza na wa pili kama seneta wa serikali ya Uhuru alipokuwa akikosoa utawala uliopo mamlakani mara kwa mara.
Orengo anafahamika kwa msemo wake maarufu “Wakati mwingine mageuzi huwala watoto wake wenyewe …serikali huwala watu wake yenyewe. Serikali itakuadhibu wewe kuliko itakavyoniadhibu mimi, nakwambia "
Pamoja na kuwa wakili wa muda mrefu wa Raila, walishirikiana kupigania demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya wakati wa utawala wa Daniel Moi wa chama kimoja wa .
Kwa sasa ni Gavana mteule wa Kaunti ya Siaya.
Pia alimwakilisha Bw Raila katika uchaguzi wa mwaka 2017 ambapo Uhuru alishinda.
Alichaguliwa kama mbunge wa Ugenya kwa tiketi ya chama cha KANU mwaka 1980 na kuwa mbunge mwenye umri mdogo zaidi nchini wakati huo, akiwa na umri wa miaka 35.
Otiende Amollo
Amolo ni mbunge mteule wa jimbo la Rarienda magharibi mwa Kenya. Wakili huyo anayeongea kwa utaratibu wakati mmoja alihudumu kama Ombudsman.
Otiende alipata umaarufu mwaka 2017 wakati alipofanikiwa kutetea hoja katika kesi ya Raila dhidi ya Muungano wa Jubilee katika Mhakama ya juu zaidi iliyogeuza matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.
Mawakili wengine katika jopo la Odinga katika kesi hii ni Tom Ojienda, Philip Chirchir Murgor, na Paul Mwangi.
Mawakili wa Ruto
Wakili Fred Ngatia
Akiwa na uzoefu wa kisheria wa miaka zaidi ya 40, ni mojawapo ya sababu ambazo bila shaka, Ngatia yuko miongoni mwa mawakili wanaomuwakilisha Bw William Ruto katika kesi ya kupinga matokeo ya urais ambayo alitangazwa kuwa mshindi.
Bw Ngatia alikuwa wakili mtetezi wa Rais Uhuru Kenyatta wakati mgombea Raila Odinga alipowasilisha kesi Mahakama ya juu zaidi,mwaka 2017 ambapo Bw Kenyatta alishinda .
Kesi nyingine iliyompatia umaarufu ni ile alipomwakilisha Francis Karoki Muruatetu na Wilson Thirimbu, walipopinga uhalali wa kikatiba wa hukumu yak io nchini Kenya. Msingi wa hoja yao ilikuwa ni vipengele vya 203 na 204 vinavyoweka adhabu ya kifo kwa watu waliopatikana na hatia ya mauaji kwamba inavunja haki na kuwanyima waliopatikana na hatia haki ya haki ya kesi isiyo na upendeleo.
Mahakama ya juu iliafikiana na mteja wa Ngatia na kutangaza kuwa hukumu ya lazima ya kifo ni kinyume cha sheria. Bw Ngatia ni Wakili mwanadamizi.
Katwa Kigen
Wakili Katwa Kigen, sawa na Bw Orengo na Bw Otiende upande wa Raila, kwa upande wa Bw William Ruto, Wakili Katwa Kigen si mgeni hususan katika kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto mahakamani.
Mwaka 2020 ,Wakili Kigen ambaye anatoka katika kabila la Bw Ruto la Kalenjin alikuwa wakili mtetezi katika kesi ya uhalifu uliotekelezwa katika uchaguzi mkuu wa 2007 iliyomhusisha Bw Ruto katika mahakama ya kimataifa ya jinai -ICC. Hali kadhalika alimuwakilisha kisheria katika kesi ya madai ya upokonyaji wa ardhi ya mwaka 2004.
Katwa Kigen ambaye ni wakili aliyebobea katika sheria za kimataifa ni wakili anayefanya kazi hiyo nchini Kenya ya kampuni ya mawakili ya Katwa & Kemboy.
WakiliKindiki kithure
Wakili Kindiki kithure ni wakili wa muda mrefu ambaye pia alikuwa miongoni mwa jopo la mawakili waliomwakilisha Bw William Ruto katika kesi ya uhalifu iliyomuandama kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai ICC mjini The Heague.
Akiwa mwanachama wa Muungano wa Bw William Ruto, UDA ,Kindiki mwenye umri wa miaka 50 alifuzu katika Chuo kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini mwaka 2002 ambapo alitunukiwa shahada ya udaktari - PhD katika Sheria ya Kimataifa, mwaka 2002 alipata shahada ya uzamili katika sheria za kimataifa katika haki za binadamu na demokrasia katika shu kikuu cha Pretoria, na mwaka 1998, alitunukiwa shahada ya sheria kutoka chuo kikuu cha Moi nchini Kenya.
Aliwahi pia kuwa mhadhiri wa sheria katika Chuo kikuu cha Nairobi.
Mwaka 2013 alichaguliwa kama mbunge wa Kaunti ya Tharaka -Nithi katika seneti ya Kenya ambako baadaye aliteuliwa kuwa kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti kabla ya kuondolewa kwa kura.
Mawakili wa IEBC
Mwanasheria Mkuu wa zamani Profesa Githu Muigai
Tume huru ya uchaguzi na mipaka ( IEBC), imemteua Mwanasheria mkuu wa zaman nchini Kenya Profesa Githu Muigai kuongoza jopo la mawakili katika kesi ya kupinga amatokeo ya urais iliyowasilishwa na mgombea Raila Odinga dhidi yake. Bila shaka Bw Githu Muigai mwenye shahada ya uzamifu (PhD) katika sheria kutoka Chuo kikuu cha Nairobi na ile ya LLM kutoka Chuo Kikuu cha Colombia, ni mwanasheria mwenye uzoefu mkubwa katika kesi za utatuzi wa migogoro kama huu ambao IEBC imejipata katikati yake.
Alijiunga katika baraza la wanasheria katika mwaka 1985. Amebobea katika sheria ya manunuzi ya mali za umma, fedha za makampuni na biashara. Zaidi ya hayo Bw Muigai amekuwa akitekeleza kazi ya uwakili ikiwa ni pamoja na kuwa rafiki wa mahakama katika kesi sawa na ya sasa , iliyowasilishwa na Bw Odinga katika Mahakama ya juu zaidi kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyompatia ushindi Bw Kenyatta na baadaye mahakama hiyo kuidhinisha ushindi wake.
Bw Githu Muigai atashirikiana na mawakili Kamau Karori , Abdikadir Mohamed, Erick gumbo, Wambua Kilonzo, Peter Wanyama, George Murugu, Mahat Somane, Cypriane Wekesa na Edwin Mukele.
Katika mapambano haya ya kisheria IEBC inatarajiwa kuishawishi Mahakama ya juu zaidi ya Kenya kwamba uamuzi wake wa kumtangaza Bw William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais 2022, ulikuwa ni sahihi.
Kwa upande mwingine Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya , kama ilivyofanya katika mwaka 2017, ina mamlaka ya kubatisha uchaguzi wa urais, na kuitisha uchaguzi mpya katika kipindi cha siku 60. Je ni upande gani utakaoweza kuishawishi mahakama katika maamuzi yake? IEBC, upande wa William Ruto, au Raila?... Jibu litapatikana baada ya mahakama kusikiliza hoja za pande zote husika na kesi hii.