Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Raila Odinga awasilisha kesi ya kupinga uteuzi wa William Ruto mahakamani
Mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio Raila Odinga hatimaye amewasilisha rasmi ombi la kupinga uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule.
Kesi hiyo iliwasilishwa na mawakili wa Raila walioongozwa na wakili James Orengo katika mahakama ya upeo ya Milimani .
Sheria kuhusu kesi ya kupinga uchaguzi wa Urais 2017 inasema kwamba iwapo kesi itawasilishwa katika siku ya mwisho ya muda uliowekwa kuwasilisha kesi hiyo basi lazima ifanyike kabla ya saa nane mchana katika siku hiyo.
Kulingana na wakili wa Muungano wa Azimio Daniel Maanzo , kikosi cha mawakili wa Muungano wa Azimio tayari kimewasilisha kesi hiyo mtandaoni na kwamba watawasilisha stakhabadhi zinazohitajika mahakamani wakati wowote kufikia sasa.
''Tumewasilisha kesi hiyo kupitia mtandao huku tukisubiri kuleta stakhabadhi ili mahakama hiyo iweze kuthibitisha ombi hilo''.
''Tuna hadi saa nane lakini naweza kuwahakikishia kwamba kila mtu yuko tayari. Kundi la mawakili linaendelea kukusanya nakala za kesi hiyo na zinatarajiwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa'', alisema Maanzo.
Na kufuatia hatua ya kuwasilisha kesi hiyo mahakamani, Muungano wa Azimio una hadi tarehe 23 Agosti , kukikabidhi chama cha UDA, rais Mteule na tume ya uchaguzi IEBC malalamishi hayo.
IEBC itakuwa na siku nne kuwasilisha majibu yao katika mahakama ya upeo. Hii itafungua njia ya kusikilizwa kwa ombi hilo na majaji wa Mahakama ya upeo siku saba baada ya kuwasilishwa - Jumatatu, Agosti 29.
Majaji wa mahakama ya upeo wakiongozwa na rais na Jaji Mkuu Martha Koome watakuwa na hadi Septemba 4, kutoa uamuzi wao kuhusu ombi hilo.
Kulingana na Kifungu cha 140 cha Katiba ya Kenya (2010), mahakama, kupitia kura ya majaji wengi, inaweza kuunga mkono au kubatilisha uchaguzi wa urais. Iwapo ushindi wa Ruto utaidhinishwa, ataapishwa siku saba baada ya uamuzi huo kutolewa - uamuzi unaopingana utasababisha kurudiwa kwa uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi yaliotangazwa na mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi IEBC yalisema kwamba Mgombea wa chama cha UDA ndiye aliyeshinda uchaguzi kwa asilimia 50.49 huku mpinzani wake wa karibu Raila Odinga akipata asilimia 48.85.
Hii ni mara ya tano kwa Raila Odinga kuwania wadhfa huona mara ya tatu kupinga matokeo ya uchaguzi ya urais kupitia mahakama ya upeo, baada ya kuwasilisha pingamizi katika uchaguzi wa 2-13 na 2017.
Mwaka 2017, mahakama ya upeo iliagiza marudio ya uchaguzi , uchaguzi ambao ulisusiwa na Odinga ambaye alipoteza tena kwa rais aliyepo madarakani Uhuru kenyatta.
Na hayo yakijiri wafuasi wa Muungano wa Azimio wamekongamana nje ya mahakama hiyo ya milimani ili kuunga mkono azma ya Muungano huo kuwasilisha kesi hiyo.
Wakati huohuo usalama umeimarishwa nje ya mahakama hiyo .
Tunaendelea kukupasha...