Nchi za Afrika zimechukua hatua gani kuwalinda wananchi dhidi ya gharama ya juu ya maisha?

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili

Gharama ya juu ya maisha imeendelea kuwaathiri watu kote duniani huku raia wa nchi nyingi hasa barani Afrika wakizitarajia serikali zao kuchukua hatua kuwapa afueni .

Licha ya hali hiyo ngumu kusababishwa na vichochezi vilivyo nje ya uwezo wa serikali zao kama vile vita vya Urusi nchini Ukraine ,bei ya juu ya mafuta duniani na kiangazi kilichosababisha uhaba wa chakula ,wananchi wamekuwa na matarajio kwamba nchi zao zitachukua hatua ama kuweka mikakati ya kuwapa afueni wakati huu mgumu .

Hata hivyo mataifa mengi hayajafanikisha mipango ya kuleta afueni hiyo kwa wengi kwa sababu baadhi ya mipango hiyo imekuwa ya muda mfupi .

Nchini Kenya kwa mfano serikali ilianzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa unga wa mahindi ulidumu kwa mwezi mmoja tu kisha bei ya juu ya bidhaa hiyo ikarejea ambayo watu wengi hawawezi kuimudu .

Kununua bidhaa kwa Pamoja

Mnamo Mei mwaka huu nchi za Kiafrika ziliweka makubaliano ya kuiweza kununua kwa pamoja bidhaa za kimsingi, ambazo usambazaji wake umeathiriwa na mzozo wa Ukraine, kufuatia kuzinduliwa kwa Soko la Biashara la Afrika (ATEX), jukwaa lililoundwa ili kuepusha madhara ya vita vya Ulaya mashariki barani Afrika.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Benki ya Uagizaji wa Bidhaa za Kiafrika (Afreximbank) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa ushirikiano na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika (UNECA).

Ilitafuta kuzisaidia chumi ambazo tayari zimedorora kukabiliana na uhaba wa usambazaji uliosababishwa na vita vya Ukraine, UNECA ilisema katika taarifa wakati huo.

"Mgogoro wa Urusi na Ukraine umeongeza matatizo katika mizunguko muhimu ya ugavi katika masoko ya bidhaa, na ongezeko la bei la sasa na linalotarajiwa katika bidhaa za kilimo na pembejeo kama vile nafaka na mbolea," ilisema taarifa hiyo.

"Madhara makubwa zaidi ni athari za chini za vizuizi vinavyowezekana vya ugavi ambavyo vinaweza kuongeza bei, kuongeza hatari na ukosefu wa usalama wa chakula, kujenga shinikizo lisiloweza kudumu kwa mazingira tayari ya kifedha."

Mgogoro wa Ukraine umesababisha uhaba wa ngano, mahindi, na nafaka nyinginezo, pamoja na mbolea katika nchi kadhaa za Afrika, nyingi ambazo ni waagizaji wa vyakula kutoka nje ambao hupata zaidi ya asilimia 80 ya ngano na mahindi yao kutoka Urusi na Ukraine.

Hii imeshuhudia bei za bidhaa za chakula na mafuta zikipanda na sarafu zikishuka thamani katika nchi za Afrika.

Nchini Kenya, bei iliongezeka kwa asilimia 6.47 mwezi wa Aprili pekee, wakati shilingi iliposhuka hadi rekodi ya chini ya Ksh117 kwa kila dola ya Marekani.

Uganda ilisajili kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 1.4 mwezi Aprili na sarafu yake imekuwa ikiyumba dhidi ya dola ya Marekani. Nchini Tanzania, bei ilipanda kwa asilimia 3.8, huku Rwanda ikipanda kwa asilimia 3.5 mwezi Aprili pekee.

Mikopo ya kutoa afueni kwa wananchi

Nchini Tanzania kulikuwa na matumaini mwezi Julai kwamba wanannchi wangepata afueni baada ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kutoa mkopo wa trilioni 2.4 kwa Tanzania ili kutoa unafuu wa gharama za maisha.

Bodi ya Utendaji ya IMF iliidhinisha Dola za Kimarekani bilioni 1.046.4 (kama trilioni 2.4/-) za Msaada wa Kulipa Mikopo (ECF) kwa Tanzania.

Madhumuni makubwa ya utoaji wa mikopo hiyo yalikuwa kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, ambavyo vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa nyingine duniani kote.Hata hivyo licha ya hatua hiyo wananchi wamezidi kuathirika na gharama ya juu ya bidhaa muhimu ingawaje mamlaka zinasema hali ingekuwa mbaya zaidi iwapo haingeingilia kati kuzuia ongezeko zaidi la bidhaa kama vile mafuta .

Kando na juhudi hizo ,serikali ya Tanzania pia ilitoa onyo kwa wafanyabiashara dhidi ya kuongeza bei za bidhaa ili kuwalinda wananchi dhidi ya gharama ya juu ya maisha.