Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bei ya Unga Kenya: Je ni mchezo wa paka na panya Wakenya wakiendelea kuumia?
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili
Mjadala kuhusu bei ya unga nchini Kenya ni suala ambalo limetawala mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni huku serikali na wafanyabiashara wa unga wakiwa wahusika wakuu.
Hali hiyo imewaacha raia na manung’uniko wasijue la kufanya wakati huu ambapo mfumuko nchini Pamoja na vita vya Ukraine vinaendelea kulazimu kupanda kwa bei za bidhaa muhimu duniani.
Kufikia sasa bei ya Unga imepanda hadi kufikia ksh.230 kutoka ksh. 140 mwezi Juni.
Hali hiyo imewapatia fursa wanasiasa nchini wakati huu wa kampeni za uchaguzi kulivalia njuga suala hilo na kutoa ahidi kedekede iwapo wangechaguliwa.
Je ni nini haswa kinachochochea kupanda kwa bei ya Unga Kenya?
Mwaka 2021 serikali iliongeza ushuru wa bidhaa muhimu . Hi ni baada ya Kenya kuingia katika mkataba wa kutafuta mkopo kutoka kwa Shirika la Fedha duniani IMF kama hatua mojawapo ya kufidia janga la corona lililoathiri sekta kubwa ya uchumi.
Mbali na hilo Mishtuko ya uzalishaji kutokana na hali mbaya ya hewa pamoja na kupanda kwa gharama ya uchukuzi ni miongoni mwa vichochezi vya kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.
Kupanda kwa bei ya mafuta kunakochangiwa zaidi na vita vinavyoendelea nchini Ukraine kumesababisha gharama ya uchukuzi kupanda hali inayosababisha kupanda kwa mzigo wa gharama ya usafirishaji – ambapo wakati mwingi huwachiwa raia mlipa kodi.
Je serikali imefanya nini?
Tarehe 29 mwezi Juni 2022, serikali ya Kenya ilifutilia mbali kodi yote inayotozwa mahindi yanayoagizwa kutoka nje kwa lengo la kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Hatua hiyo ilionekana kama afueni kwa Wakenya huku matarajio ya kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu yakiwa juu.Hata hivyo kufikia wakati wa kutayarisha makala hii,bei ya unga haikuwa imeshuka kama ilivyotangazwa huku wasagaji wa nafaka wakisema hawakuwa wameafikiana na serikali kuhusu mpango wake wa ruzuku .
Waziri wa kilimo nchini kenya Peter Munya alisema kwamba hatua hiyo ya kuondoa kodi ililenga kuhakikisha kwamba kuna mahindi mengi nchini na hivyobasi kushinikiza kupungua kwa gharama ya uzalishaji wa unga wa mahindi.
Bwana Munya aliyekuwa akizungumza kutoka katika mpaka wa Kenya na Tanzania alisema kwamba mahindi yote yatakayonunuliwa kutoka Tanzania pampja na mataifa ya COMESA yaruhusiwe bila kutozwa kodi yoyote kuanzia tarehe mosi mwezi Julai.
Lengo lake alisema ni kuharakisha kuruhusiwa kwa malori yanayobeba mahindi kuingia nchini Kenya kutoka mipaka yote. Vilevile aliwaonya wale wanaozuia mahindi kwa lengo la kusababisha uhaba ili wayauze kwa bei ya juu kutolalamika wakati mahindi ya bei ya chini yatakapoingia nchini.
Serikali iliongezea kwamba mbali na hatua ya serikali kufutilia mbali kwa muda kodi , pia iliondoa kodi iliowekewa kampuni zinazoagiza mahindi ambazo sasa zitaagiza mahindi hayo bila kodi yoyote.
Tofauti iliopo kati ya wafanyabiashara wa mahindi na Serikali
Muda mfupi baada ya serikali kutangaza kwamba inaondoa kodi ya mahindi yote yanayoingia nchini kwa lengo la kupunguza bei ya bidhaa hiyo hadi shilingi 100 kwa pakiti ya kilo mbili ya Unga wa mahindi , wafanyiabiashara wa bidhaa hiyo wamepinga hatua hiyo wakisema kwamba hawajakubaliana na serikali kuhusu bei hiyo.
Nyaraka zilizovuja mapema siku ya Jumatatu na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari Kenya zilibaini kwamba Wizara ya Kilimo ilikuwa na mpango wa kuanzisha programu ya ruzuku ya unga wa mahindi.
Mpango huo ambao ungeendelea kwa mwezi mmoja ungepelekea bei ya rejareja iliyopendekezwa kwa pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi kushuka hadi Ksh.100 kutoka kiwango cha juu cha sasa cha Ksh.210 na Ksh.52 kwa kilo ya unga wa mahindi uliosagwa.
Serikali nayo ingewalipa fidia wafanyabiashara wanaosaga mahindi kwa tofauti hiyo (bei iliyopo ya kuuza na bei mpya ya ruzuku ya kibinafsi). Kulingana na hati hizo zilizofichuliwa, ruzuku hiyo ingeungwa mkono na akaunti ya escrow katika Benki Kuu ya Kenya (CBK) ambayo ingetumika kuwafidia wanaosaga unga wa mahindi Kenya.
Hata hivyo, aakizungumza na BBC waziri wa Kilimo Peter Munya amekana madai hayo.
Masharti ya wafanyabiashara wa unga wa mahindi
Katika taarifa ya pamoja mwezi Juni , Muungano wa Wafanyabiashara wa bidhaa hiyo UGMA ulisema kwamba Wakenya wataendelea kulipia gharama ya juu kwasababu ya uhaba wa bidhaa hiyo unaoendelea kushuhudiwa kote nchini. Kulingana na wafanyabiashara hao , uhaba huo unasababishwa na hali ya ukame usioisha mbali na upungufu wa uagizaji wa bidhaa hiyo.
Ili kukabiliana na mahitaji ya juu ya bidhaa hiyo , wafanyabiashara hao wanasema kwamba wamelazimika kuagiza kutoka mataifa mengine kwa bei ya juu. Na ili kuilinda nchi dhidi ya uhaba huo huo , wafanyabiasara hao wanaitaka serikali kuweka usawa katika soko la uagizaji kupitia kondoa kodi za mahindi na ngano kutoka mataifa ya nje.
Pia wanaitaka serikali kuruhusu uagizaji wa mahindi bila kutozwa ushuru kutoka Umoja wa Ulaya, na kuwahimiza wakulima wa Kenya kutoa hifadhi yao ya mahindi.
Kufikia mwisho wa mwezi Mei, Chama cha Wazalishaji wa Kenya (KAM) na Chama cha Wasagaji Nafaka (CMA) kilikuwa kimewatahadharisha Wakenya kwamba bei ya unga wa mahindi bado ingepanda licha ya Bunge la taifa kupinga kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa hizo kama ilivyopendekezwa na mswada wa Sheria ya Fedha wa 2022.
Je hatua hiyo inawawacha wapi Wakenya?
Huku mafahali hao wawili wakiendelea kukabiliana na kutofautiana kuhusu bei ya Unga wa mahindi kwa kweli ni nyasi zinazoumia. Mjadala kati ya serikali na wafanyabiashara wa mahindi kuhusu bidhaa hiyo unawawacha Wakenya wengi wasioweza kuhimili bei ya bidhaa hiyo na njaa.
Hali hiyo imewafanya baadhi ya Wakenya kufanya maandamano wakiishinikiza serikali kuchukua hatua ya kuwapatia afueni Wakenya
Swali ni je , kati ya mafahali hao wawili ni nani atakayerudi nyuma wa Kwanza ili kuweka mbele maslahi ya Wakenya?