Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Wadukuzi walivujisha picha zangu za utupu baada ya kipakatalishi changu kuibiwa'
Wadukuzi walipotishia kuvujisha picha za utupu za mtengenezaji filamu zilizohifadhiwa kwenye kipakatalishi chake kilichoibiwa yaani ‘laptop’, aliamua kuangazia yaliyojiri na kuandika masaibu aliyopitia.
Muelekezi wa filamu kutoka Uhispania Patricia Franquesa alikuwa ameketi kwenye mkahawa huko Madrid wezi walipoondoka na kipakatalishi chake mnamo mwaka 2019.
Miezi mitatu baadaye, wadukuzi waliwasiliana naye wakimlaghai na kutishia kuvujisha picha za utupu alizokuwa amehifadhi kwenye kifaa hicho ikiwa hatatoa pesa.
Franquesa hakujua kwa uhakika - na bado hajui - ikiwa mtu anayejaribu kumlaghai ni yuleyule aliyeiba kipakatalishi chake.
Lakini katika hali ambayo waathiriwa wana udhibiti mdogo, Franquesa aliweza kurekodi yote yaliyotokea na kutengeneza filamu kutokana na mtazamo wake jinsi hali ilivyoendelea kujitokeza.
Matokeo yake ni filamu kwa jina, ‘My Sextortion Diary, ambayo ilionyeshwa hivi karibuni kwenye Tamasha la Filamu la Sheffield.
"Kutengeneza filamu ilikuwa njia yangu ya kuchukua udhibiti na mamlaka," Franquesa aliambia BBC News. "Ilikuwa njia yangu ya kujilinda, sio kujidhuru mwenyewe na kunitenganisha, ilikuwa kama njia ya kukataa kilichoendelea."
Utengenezaji filamu ulikuwa kitu muhimu, na pia kulimsaidia kutafakari kilichokuwa kikiendelea. "Bado ni mimi bila shaka, lakini nilihitaji kujitenga. Nilikuwa nazungumzia 'Pati', lakini kuna Pati mhusika na Pati mkurugenzi."
Anatania kwamba inafaa sana kwamba masaibu kama hayo "yangemtokea mtu ambaye hufanya filamu, kwa hivyo ni fursa nzuri ya kugeuza mambo".
Kupiga, kuhifadhi na kutuma picha za utupu ni kawaida kabisa kwa kizazi kizima ambacho kimekua na mtandao.
Lakini inafungua ulimwengu mzima wa hatari ambao wale waliozaliwa katika miongo ya mapema hawakuwahi kukumbana nayo.
"Baba yangu alimpiga mama yangu picha akiwa amevalia vazi la kuogelea ambalo huenda lilionekana wazi," Franquesa anatabasamu anapokumbuka enzi ambayo inaonekana kuwa ngumu kwa kulinganisha. "Lakini tangu tulipoingia katika ulimwengu wa kidijitali, ni njia yetu mpya ya kuwa na ukaribu."
Kwa upande wake, wadukuzi hao walionyesha jinsi walivyokuwa wakimaanisha kwa kuvujisha baadhi ya picha zake za utupu kwa marafiki zake, familia na wafanyakazi wenzake, ambao waliwapata kupitia mawasiliano yake ya mitandao ya kijamii.
Lakini Franquesa alisonga mbele kadiri filamu ilivyoendelea. Polisi walimwandikia barua kumwambia wamemkamata mhalifu baada ya kukagua picha za CCTV kutoka kwenye mkahawa - ambazo hatimaye alizipata na kuzijumuisha kwenye filamu.
Inaonyesha jinsi kipakatalishi kilivyochukuliwa na wanaume watatu, nyuso zao zikiwa zimefunikwa kwa ajili ya filamu hiyo, wakishirikiana pamoja kutoka pembe tofauti ndani ya mkahawa huo.
Lakini bila kujali kwamba uchunguzi wa polisi unaoendelea, wadukuzi waliendelea na majaribio yao ya kutaka atoe pesa.
Akiwa amechoka, bila chaguo na akiendelea kukataa kulipa pesa, hatimaye Franquesa aliamua kuchapisha picha hizo kwenye mitandao yake ya kijamii - jambo la mwisho la kutisha, lakini ambalo liliwaacha wadukuzi bila nguvu tena.
"Ilikuwa jambo gumu sana kufanya, nilikuwa nalia," anakumbuka. "Ilionekana kama dakika ya mwisho ya mbio za marathon. Sikutaka kuchapisha picha hizo, nilitarajia na kusubiri labda mtu huyu angewacha kufanya hivyo, lakini unaona kwamba haachi, kwa hivyo sikuwa na kitu kingine cha kufanya."
Hata hivyo, kumfanya mdukuzi huyo kukoma kusambaza picha zake haikuwa kitu pekee alichokusudia. "Ilikuwa kwa ajili yangu kusema, ‘jamani huyu mdukuzi ana picha hizi, na anatumia walio kwenye mawasiliano yangu, nisaidieni'."
Hiyo ilibadilisha nguvu yake kwa kiasi fulani, na ilimaanisha kuwa Franquesa angeweza kuelezea marafiki na wafuasi wake wamsaidie kumjua mdukuzi na tabia zake.
"Ambayo ilibadilisha uhalisia wa mambo, anasema. “Nilitaka walio kwenye mawasiliano yangu waniambie wamezipata lini picha hizo, maana hapo nitakuwa na ushahidi zaidi wa kuupeleka polisi na kuweka wazi upelelezi.
"Ilikuwa kumaliza aibu," anaakisi yaliyojiri. "Jaribio la mtu mwingine kunitia aibu limemalizika kwa sababu ninamiliki picha zangu. Na kisha likakoma, kimuujiza."
Ukweli kwamba mdukuzi huyo aliacha kuwasiliana na watu waliokuwa kwenye orodha ya mawasiliano yake muda mfupi baada ya Franquesa kuweka picha hizo kunaonyesha kuwa ni mtu ambaye tayari alikuwa akimfuatilia alipobadilisha akaunti zake kuwa za faragha baada ya jaribio la kwanza la kumlaghai - lakini bado hajui ni nani.
Filamu hiyo imefanya vizuri kwenye tamasha ambazo tayari imeonyeshwa. Mark Adams wa Business Doc Europe aliielezea kama "hadithi ya maisha halisi yenye nguvu, inayoonyesha hali halisi isiyo na furaha inayowakabili watu ambao wanalazimika kukabiliana na tabia mbaya ya wadakuzi wanaotaka kulaghai watu".
Mwisho ulio na 'tamu chungu'
Mwanamume ambaye aliiba kipakatalishi chake hatimaye alifungwa jela. Lakini kwa Franquesa, jambo la msingi halikuwa kipakatalishi, lakini zaidi jinsi data yake mwenyewe ilitumiwa dhidi yake.
"Alihukumiwa kifungo cha miezi 10 jela, kwa kuiba kipakatalishi. Na niliweza, katika hukumu ya hakimu, kusema kwamba anahusishwa na uwezekano wa udukuzi," anaeleza.
Lengo la Franquesa tangu wakati huo limehamia kwenye kuongeza ufahamu wa kile kilichotokea - na kuuliza maswali kuhusu jinsi mitandao hii ya uhalifu inavyofanya kazi.
"Niliwaambia polisi, yule mtu [aliyeiba kipakatalishi] anajua alichofanya na kifaa hicho. Lakini polisi waliniambia kuwa kifaa hicho hakitapatikana, nikasema, 'Najua hivyo, lakini wanafanya nini na kifaa kilichoibiwa?'
“Kwa sababu sasa hivi kuna mafia wengi, Hispania wanaiba vifaa na kuviuza, halafu wanaenda kwa watu wanaodukua vifaa na kuchukua data, na kuanza kulaghai watu ili wawapore pesa. Nataka kuelewa ni mfumo gani huo."
Anasema: "Sio tu juu ya kupata haki katika kesi yangu, kwa sababu imekwisha kwangu, lakini ni kwa polisi kuelewa kinachoendelea katika kesi za aina hii. Je! ni mfumo gani wa mafia hawa? Kama ningekuwa polisi, ningetamani sana kujua."
Changamoto kubwa ilikuwa jinsi ya kutengeneza kitu kama filamu kutoka kwa nyenzo kidogo sana. Franquesa anaweza tu kuandika upande wake wa hadithi, na mengi hutokea kupitia mawasiliano ya maandishi - barua pepe kutoka kwa wadukuzi, barua kutoka kwa polisi au ujumbe kati ya Franquesa na marafiki zake.
Muongozaji "hakuona hiki kama kizuizi" kwasababu madhumuni ya filamu ilikuwa ni "shajara ya kidigitali".
Wadukuzi hao wanawakilishwa na sauti ya kike iliyobadilishwa kidijitali, huku mazungumzo ya maandishi yakiwakilishwa na matamshi ya kidijitali ambayo yanaiga yaliyokuwa yakiendelea kwenye jukwa la mtandao wa WhatsApp.
Lakini "pia ni aina hii ya utunzi wa simulizi ambayo inachangia filamu kupokelewa vyema ndani ya kipindi kifupi," alibainisha Blake Williams wa HyperReal Film Club.
"Shajara yangu ya ulaghai wa mtandaoni kwa kutishia kutoa picha zangu za utupu inasababisha hisia kila wakati na kujiweka katika simulizi yenye kuvutia licha ya mbinu yake ya uelezeaji isiyo ya kawaida."
Filamu hii inaishia kabla ya hukumu kutolewa, kwa sababu, Franquesa anacheka, "Tulihitaji kumaliza filamu kwa wakati kwa ajili ya tamasha ambapo filamu ilionyeshwa mnamo mwezi Machi. Anasema sasa sehemu mapya itaongezwa mwishoni mwa filamu hiyo kufuatia mhusika kukutwa na hatia.
Franquesa hatimaye anatumai kuwa filamu itasaidia kuleta mabadiliko, kwa sababu anahisi kuwa sheria hazibadiliki haraka vya kutosha ili kuendana na tabia ya uhalifu.
"Nataka kupaza sauti na kusema kwamba njia hii haifanyi kazi, sheria za data zetu. Mfumo wetu unaohitaji kutulinda unakwenda polepole sana. Kuna shida hapa kuhusu ulinzi tulionao.
"Kitu cha kuridhisha kwa kesi hii ni kwamba sasa tunazungumzia, mwisho wa filamu ulio tamu uchungu, mafanikio ya Pati ni kutengeneza filamu, lakini kwa mdukuzi na haki havijakamilika."
Anahitimisha kwa kusema: "Natumai kesi yangu itatumika kuelewa kile [wahalifu] wanafanya, ninajiweka mbele ili waweze kutafiti kesi yangu na kusaidia watu wengine."
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Yusuf Jumah