Je, maadili ya matibabu ni yapi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kumekuwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu video ya daktari wa Kisomali ambaye alirikodi video ya moja kwa moja kwenye akaunti yake ya TikTok, akimfanyia upasuaji mwanamke.
Watu walihoji usalama wa mwanamke huyo na mtoto, kwani daktari alikuwa mubashara kwenye Tiktok.
Daktari alisema upasuaji huo haukuwa wa haraka, “baada ya kumaliza upasuaji nilimtoa mtoto na kurekodi video mubashara,” alisema.
Daktari huyu wa upasuaji, ambaye anafanya kazi katika moja ya hospitali mjini Mogadishu, alisema majukwaa ya mtandaoni, kama TikTok, huwashauri watu kuhusu masuala ya afya.
“Video ya upasuaji huu ilikuwa ya kuelimisha, nikiwa natunza taarifa za mgonjwa, nilipata wazo la kuwaelimisha akina mama na kuwaeleza mambo yanayoweza kusababisha matatizo mfano tumbo la uzazi kupasuka,” alisema.
Daktari huyo, ambaye ana maelfu ya wafuasi kwenye Tiktok, alisisitiza - video hiyo ilikuwa ya kuelimisha, akikana kufanya kosa lolote.
Serikali ya Somalia inasema suala hilo linachunguzwa.
Je, maadili ya matibabu yanasemaje?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Dkt. Saeed Sheikh Mohamed, mtaalamu wa upasuaji wa watoto, anaefanya kazi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Jazeera mjini Mogadishu, aliambia BBC, si jambo geni kwa huduma za matibabu kwa wagonjwa kutazamwa moja kwa moja.
Anasema sababu kubwa ya kumrekodi mgonjwa huyo ni kuitumia video hiyo kisayansi, na kuelezea aina ya upasuaji utakaofanyika.
“Sasa suala lililojitokeza ni kupeperushwa moja kwa moja, hilo ni jambo ambalo linahitaji utafiti wa muda mrefu kuhusiana na faida na hasara zinazoweza kupatikana kutokana na hilo,” anasema.
Dkt. Mohamed aliambia BBC, taaluma ya matibabu ni kazi inayohusiana na binadamu, na ina sheria zake kali.
Maadili ya taaluma ya matibabu kwa ujumla yanategemea nguzo kuu nne:
- Kumpa mgonjwa huduma muhimu itakayo msaidia, na kumlinda kutokana na mambo yasiyo faa, iwe ni katika uchunguzi, upasuaji au dawa.Kwa mfano, unafanya upasuaji wa saratani isiyotibika na unajua kwamba ikiwa atawekewa dawa ya ganzi, mgonjwa atalazwa ICU au atakufa kwa ganzi.
- Usisababishe madhara kwa mgonjwa, ikiwa hujui tatizo lake. Mfano mgonjwa akija kwako akilalamikia jambo linalohusiana na taaluma tofauti na uliyosomea na kuna madaktari wanaofaa kumsidia mgonjwa huyo. Wewe hupaswi kumtibu.
- Ili kumpa mgonjwa uhuru wa kuchagua - daktari anahitajika kumueleza mgonjwa ikiwa kuna njia nyingine kadhaa za kutibu ugonjwa huo, na kila njia faida na hasara. Unapaswa pia kumpa ushauri wa matibabu. Pia, usiri wa mgonjwa lazima ulindwe na hauwezi kuelezwa kwa mtu mwingine au daktari mwingine bila ridhaa ya mgonjwa.
- Utoaji wa huduma za afya haupaswi kuzingatia jinsia/mwanaume, mkubwa au mdogo, adui au rafiki, na hali ya kijamii ya mgonjwa kama maskini au tajiri.
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












