Familia yangu bado iko hai? Swali la kila siku wanalojiuliza Wahaiti

xx

Kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, Nun Neethoudjif Méléance amezoea utaratibu wenye machungu. Yeye huangalia simu yake kila siku ili kuona ikiwa familia yake bado iko hai.

Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 22 anaishi Cap-Haitien pamoja na kaka yake.

Lakini watu 10 wa familia yake akiwemo babake na ndugu zake wengine bado wako Port-au-Prince, ambapo magenge yanadhibiti takriban asilimia 80 ya mji huo mkuu.

"Wanaishi katika aina ya gereza la wazi kwa sababu hawawezi kwenda mbali sana kutokana na sababu za kiusalama. Wanamiliki duka ambapo wanauza chakula lakini ni vigumu kwao kununua bidhaa za kuuza."

Umoja wa Mataifa umeelezea hali ya Haiti katika maneno ya janga, kama taifa lililo "karibu kuporomoka".

Taifa hilo maskini la Caribbean linakabiliwa na ukosefu wa serikali na kujazwa na magenge ya watu wenye silaha, ambapo silaha haramu zinaendelea kumiminika nchini humo, na kuipeleka nchi karibu na hali ya janga.

Nun anafungua programu yake ya kutuma ujumbe.

Baba yake ameacha ujumbe akisema kulikuwa na ufyatuaji risasi karibu nao asubuhi. Wako sawa lakini anahisi kuvunjika moyo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zaidi ya watu 30,000 wameikimbia Port-au-Prince, wengi wao wakistahimili safari ndefu hatari za basi kwenye barabara zinazodhibitiwa na genge ili kufika hapa. Anatamani familia yake ingefanya hivyo pia lakini anasema mabadiliko ni magumu kwao - wanasitasita sana kuacha nyumba na biashara zao.

"Ninahisi kama sina uwezo kwa sababu ni wazazi wangu," anasema kwa hasira. "Siwezi kuwaambia la kufanya."

Maisha ya ujana ya Nun kwa njia nyingi yanaonyesha majanga yanayofuatana nchini mwake.

Mama yake aliuawa katika tetemeko la ardhi la mwaka 2010 ambalo liligharimu maisha ya zaidi ya 100,000. Binamu yake aliuawa na genge mwaka jana, huku wanafamilia wengi wakishindwa kuhudhuria mazishi kwa sababu ya ghasia zinazozidi kuongezeka mitaani.

Alisema baba yake hakutaka awe mwathirika, na akamtia moyo kuondoka Port-au-Prince kufuata matamanio yake.

"Jirani yangu huko Port-au-Prince alikuwa na wana sita au saba, na wawili kati yao waliishia katika magenge. Baba alikuwa mtu wa kanisa, Mkristo. Wavulana walikuwa wakienda kanisani na walikuwa wakiimba. Walikuwa na maisha mazuri ya baadaye, lakini hiyo haikuwazuia kujiunga na magenge."

Huu ni uhalisia wa kikatili unaowakabili watoto wengi.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema zaidi ya watu 1,500 wameuawa na ghasia za magenge katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu. Magenge hayo huajiri na kuwanyanyasa wavulana na wasichana wadogo, ripoti hiyo inasema, wakati mwingine huwaua wale wanaojaribu kutoroka.

"Watu huuliza kwa nini niko Haiti?" Anasema Nun. "Sawa, unaweza kukaa na kupigana, au uende na upate amani."

Wengi huchagua kuondoka. Uwanja wa ndege wa Cap-Haitien ulifunguliwa tena mapema wiki hii ambapo watu kadhaa walipanga foleni kwenye lango ndogo la kuondoka. Wakiwa wameshikilia hati muhimu, walikuwa tayari kuondoka haraka iwezekanavyo.

Baptiste Moudeché, 23, alikuwa akielekea Florida kwa mara ya kwanza na dadake mdogo. Alifunga safari kutoka Les Gonaïves, jiji la nne kwa ukubwa nchini Haiti, ambalo limekumbwa na ghasia za magenge kwa miongo kadhaa. Wazazi wake wamebaki pale kwa sasa.

"Ninaondoka kwa sababu ya maswala ya ukosefu wa usalama na shida. Tumekuwa tukiishi katika kipindi cha kuhangaika sana na familia yangu."

Hajui atarudi lini.

"Ndoto yangu ni kwa Haiti kuwa na serikali ya kawaida ambayo inafikiria sana ustawi wa taifa," alisema Baptiste. "Mahali ambapo haki za binadamu zinaheshimiwa kikamilifu na ambapo kijana yeyote anaweza kuendelea."

Waandamanaji walikusanyika nje ya ubalozi wa Canada siku ya Ijumaa wakitaka Jumuiya ya Caribbean (Caricom) iheshimu katiba.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waandamanaji walikusanyika nje ya ubalozi wa Canada siku ya Ijumaa wakitaka Jumuiya ya Caribbean (Caricom) iheshimu katiba.

Nchi hiyo sasa inasubiri kuona ni nani hasa atakabiliana na magenge hayo yanayozozania madaraka. Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye hakuwa amechaguliwa, aliahidi kujiuzulu mara tu Baraza la Mpito la Rais litakapoanza rasmi kuhudumu.

Orodha yake kamili bado haijafichuliwa, lakini wiki iliyopita, katika taarifa yake ya kwanza, iliahidi kurejesha utulivu na demokrasia kwa taifa ambalo liko katika hatua muhimu ya kihistoria.

Lakini pia muhimu ni kupata imani ya watu wa Haiti kufanikisha hilo. Wengi wana mashaka makubwa na suluhisho lililopendekezwa na jumuiya ya kimataifa.

Ingawa baraza hilo linaonekana kuwa na viongozi wa Haiti, limeundwa na shirika la kiserikali linalojumuisha mataifa 20 yaliyo katika Carribea. Wahaiti wengi wanaliona kama "uingiliaji wa kigeni".

Magenge hayo ambayo kwa sasa ni watawala wa Haiti pia yamepuuzilia mbali baraza hilo.

Mmoja wa viongozi wa magenge wenye nguvu nchini humo Jimmy ‘Barbecue’ Chérizier alisema atafikiria kusitisha mapigano: “Ikiwa jumuiya ya kimataifa itakuja na mpango wa kina, tunaweza kukaa pamoja na kuzungumza, lakini hawatatulazimisha kile tunachopaswa kuamua. "

Lakini pia itakuwa vigumu kuwashawishi Wahaiti kukubali viongozi wa magenge kama viongozi wa baadaye wa kisiasa.

Yvrose Pierre, meya wa Cap-Haitien
Maelezo ya picha, Yvrose Pierre, meya wa Cap-Haitien, anasema magenge "hayana huruma yoyote"

Yvrose Pierre, meya wa kwanza wa kike aliyechaguliwa wa Cap-Haitien, anasema: "Magenge yanaposhambulia yanawatishia watu na hawana huruma yoyote, wanaua tu. Na hatuwezi kuruhusu hilo litokee, ikiwa itakuwa hivyo mtu ambaye atauawa atakuwa wao, sio sisi."

Takriban watu milioni tano nchini Haiti - ikiwa ni pamoja na mtoto mmoja kati ya wawili - wanakabiliwa na tishio la njaa, kulingana na shirika la Save the Children.

"Watu wanakufa kwa sababu ni nchi ainayoangamia. Wakati Bandari, uwanja mkuu wa ndege na hospitali hazifanyi kazi - hakika watu watakufa.

"Ndoto yangu ni kuona wananchi wa Haiti wakikuja pamoja ili kutatua mgogoro huu. Ndoto yangu ni kuiona Haiti niliyoizoea nikiwa mtoto."

Wahaiti wengi wana ndoto sawia na hiyo. Wikendi hii ya Pasaka huku kukiwa na hali ya vurugu, nchi iliadhimisha likizo yake kuu ya kwanza kwa amani.

Ingawa Port-au-Prince haikuwa na shughuli zozote, maelfu ya waumini huko Cap-Haitien walitembea kwenye mitaa yenye vumbi wakiwa wamevalia nguo wakiimba nyimbo. Wengine walinyoosha mikono yao kuelekea angani katika hali ya kumsifu Mungu.

Kikundi cha wanawake kilikusanyika nje ya shule ya upili ya Kikatoliki kutazama uigizaji wa kusulubishwa na kufufuka kwa Yesu. Mwanamke mmoja alituambia Pasaka hii ilikuwa ya machungu: "Sijisikii vizuri ninapoona Haiti inaangamia. Hasa ninapoona kaka na dada zangu wakiuliwa kwa risasi huko Port-au-Prince."

Mwingine alisema: "Nadhani muujiza tu ndio unaweza kutusaidia."

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi