Marais wa Marekani waliouawa na walionusurika kuuawa wakiwa wagombea

Jaribio la kumuua Donald Trump siku ya Jumamosi, sio kisa pekee cha ghasia za kisiasa zinazowalenga marais wa Marekani, marais wa zamani na wagombea urais.

Kuna matukio ya mauaji na majaribio ya mauaji, ambayo yametokea tangu kuanzishwa kwa taifa hilo mwaka 1776.

Pia unaweza kusoma

Abraham Lincoln, rais wa 16

Lincoln alikuwa rais wa kwanza kuuawa, alipigwa risasi na John Wilkes Booth mwezi Aprili 14, 1865, wakati yeye na mkewe, Mary Todd Lincoln, wakihudhuria onyesho maalumu la vichekesho “Our American Cousin” kwenye ukumbi wa michezo wa Ford huko Washington.

Lincoln alipelekwa kwenye nyumba iliyo kando na barabara kutoka katika ukumbi huo kwa ajili ya matibabu baada ya kupigwa risasi nyuma ya kichwa. Alifariki asubuhi iliyofuata.

Kuunga mkono haki za watu Weusi kulitajwa kuwa ndio sababu ya mauaji yake.

Miaka miwili kabla ya mauaji hayo, wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe kuhusu utumwa, Lincoln alitoa tangazo la uhuru kwa watumwa ndani ya Shirikisho.

Lincoln alirithiwa na Makamu wa Rais, Andrew Johnson.

Booth alipigwa risasi na kuuawa Aprili 26, 1865, baada ya kukutwa amejificha kwenye nyumba ya shambani huko Bowling Green, Virginia.

James Garfield, rais wa 20

Garfield alikuwa rais wa pili kuuawa, miezi sita baada ya kuchukua madaraka. Wakati akitembea kwenye kituo cha treni huko Washington mwezi Julai 2, 1881, ili kupanda treni kwenda New England, alipigwa risasi na Charles Guiteau.

Alexander Graham Bell, mvumbuzi wa simu, alijaribu bila kufaulu kuitoa risasi hiyo iliyokuwa kwenye kifua cha Garfield kwa kutumia kifaa maalumu alichobuni.

Rais aliyejeruhiwa vibaya alitibiwa katika Ikulu ya White House kwa wiki kadhaa lakini alikufa mwezi Septemba baada ya kupelekwa ufukweni mwa New Jersey.

Garfield alirithiwa na Makamu wa Rais Chester Arthur.

Guiteau alipatikana na hatia na kuuawa Juni 1882.

William McKinley, rais wa 25

McKinley alipigwa risasi baada ya kumaliza hotuba huko Buffalo, New York, Septemba 6, 1901. Wakati akipeana mikono na watu waliokuwa kwenye mstari, mwanaume mmoja alifyatua risasi mbili kifuani mwake akiwa karibu.

Madaktari walitarajia McKinley angepona lakini uozo ulitokea karibu na majeraha ya risasi. Alikufa Septemba 14, 1901, miezi sita baada ya kuanza muhula wake wa pili.

Alirithiwa na Makamu wa Rais Theodore Roosevelt.

Leon F. Czolgosz, kijana asiye na ajira, mkazi wa Detroit, mwenye umri wa miaka 28, alikiri kumpiga risasi. Czolgosz alipatikana na hatia na kuuawa katika kiti cha umeme Oktoba 29, 1901.

Franklin D. Roosevelt, rais wa 32

Roosevelt, wakati huo rais mteule, baada tu ya kutoa hotuba huko Miami, ndipo risasi zilisikika nyuma ya gari lake lililokuwa wazi.

Roosevelt hakujeruhiwa katika shambulizi hilo la Februari 1933, lakini lilimuua Meya wa Chicago, Anton Cermak.

Guiseppe Zangara alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.

Harry S. Truman, rais wa 33

Truman alikuwa akiishi Blair House, ng'ambo ya barabara kutoka White House. Novemba 1950 watu wawili wenye silaha walivamia nyumba yake.

Truman hakujeruhiwa, lakini polisi wa Ikulu ya Marekani na mshambuliaji mmoja waliuawa wakati wa kurushiana risasi. Polisi wengine wawili wa Ikulu walijeruhiwa.

Oscar Callazo alikamatwa na kuhukumiwa kifo. Mwaka 1952, Truman alibadilisha hukumu hiyo kuwa kifungo cha maisha jela. Aliachiliwa kutoka gerezani 1979 na Rais Jimmy Carter.

John F. Kennedy, rais wa 35

Kennedy aliuawa kwa kupigwa risasi na muuaji aliyejificha, alipokuwa ziarani huko Dallas mwezi Novemba 1963 akiwa na mke wake Jacqueline Kennedy. Milio ya risasi ilisikika wakati msafara wa rais ukipita Dealey Plaza katikati mwa jiji la Dallas.

Kennedy alikimbizwa katika Hospitali ya Parkland Memorial, ambako alifariki muda mfupi baadaye.

Alirithiwa na Makamu wa Rais, Lyndon B. Johnson, ambaye aliapishwa katika chumba cha mikutano ndani ya Air Force One. Ndiye rais pekee aliyekula kiapo cha urais kwenye ndege.

Saa chache baada ya mauaji hayo, polisi walimkamata Lee Harvey Oswald baada ya kupata sangara ya mshambuliaji huyo katika jengo la karibu, la Texas School Book Depository.

Siku mbili baadaye, wakati Oswald akitolewa makao makuu ya polisi kwenda jela, mmiliki wa klabu ya usiku ya Dallas, Jack Ruby alimwendea na kumpiga risasi Oswald.

Gerald Ford, rais wa 38

Ford alinusurika majaribio mawili ya kuuawa ndani ya wiki kadhaa mwaka 1975 na hakujeruhiwa katika majaribio yote.

Katika jaribio la kwanza, wakati Ford akielekea kwenye mkutano na gavana wa California huko Sacramento, mwanachama wa genge la mhalifu Charles Manson, aitwaye Lynette “Squeaky” Fromme, alijipenyeza kwenye umati wa watu barabarani, akachomoa bastola na kuielekeza kwa Ford. Lakini haikufyatuka.

Fromme alihukumiwa kifungo na kuachiliwa mwaka 2009.

Siku 17 baadaye mwanamke mwingine, Sara Jane Moore, alimshambulia Ford nje ya hoteli huko San Francisco. Moore alifyatua risasi moja na kumkosa. Mpita njia aliyekuwa karibu alimshika mkono wakati akifyatua risasi ya pili.

Moore alifungwa gerezani na kuachiliwa 2007.

Ronald Reagan, rais wa 40

Baada ya hotuba huko Washington, DC, mwezi Machi 1981, wakati akielekea kwenye gari lake la msafara, alipigwa risasi na John Hinckley Jr., aliyekuwa kwenye umati wa watu.

Reagan alipona risasi hiyo. Lakini watu wengine watatu walipigwa risasi vilevile, ikiwa ni pamoja na mwandishi wake wa habari, James Brady, ambaye alipooza kwa risasi hiyo.

Hinckley alikamatwa na kuzuiliwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili baada ya mahakama kumkuta hana hatia kwa sababu ya ugonjwa wa akili.

Mwaka 2022, Hinckley aliachiliwa kutoka usimamizi wa mahakama baada ya hakimu kuamua "hakuwa hatari tena kwake mwenyewe au kwa wengine."

George W. Bush, rais wa 43

Bush alikuwa akihudhuria mkutano wa hadhara huko Tbilisi mwaka 2005 na Rais wa Georgia, Mikhail Saakashvili wakati bomu la kutupa kwa mkono liliporushwa kwake.

Marais wote wote wawili walikuwa nyuma ya kizuizi cha kuzuia risasi wakati guruneti lililofunikwa kitambaa, lilipotua umbali wa futi 100. Guruneti halikulipuka, na hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Vladimir Aruyunian alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Theodore Roosevelt, mgombea urais

Rais huyo wa zamani alipigwa risasi huko Milwaukee mwaka 1912 alipokuwa akifanya kampeni ya kurejea Ikulu ya Marekani.

Roosevelt hapo awali alihudumu mihula miwili kama rais na aligombea tena kama mgombea wa chama cha tatu.

Karatasi zilizokunjwa na kikasha la chuma la miwani kwenye mfuko wake, vilipunguza athari ya risasi hiyo na hakuumia sana.

John Schrank alikamatwa na kukaa katika hospitali za magonjwa ya akili maisha yake yote.

Robert F. Kennedy, mgombea urais

Kennedy alikuwa akitafuta uteuzi wa urais kupitia Democratic alipouawa katika hoteli ya Los Angeles - muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake ya ushindi kwa kushinda mchujo wa jimbo la California 1968.

Kennedy alikuwa seneta wa Marekani kutoka New York na ni ndugu wa Rais John F. Kennedy, ambaye aliuawa miaka mitano kabla.

Watu wengine watano walijeruhiwa kwa risasi.

Sirhan Sirhan alipatikana na hatia ya mauaji na kuhukumiwa kifo. Baadaye ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela. Sirhan bado yuko jela baada ya ombi lake la kuachiliwa kukataliwa mwaka jana.

George C. Wallace, mgombea urais

Wallace alikuwa akitafuta uteuzi wa urais kupitia chama cha Democratic wakati alipopigwa risasi katika kampeni huko Maryland mwaka 1972, tukio ambalo lilimfanya kupooza kutoka kiunoni kwenda chini.

Wallace, gavana wa Alabama, alikuwa maarufu kwa maoni yake ya kibaguzi, ambayo baadaye aliachana nayo.

Arthur Bremer alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo. Aliachiliwa mwaka 2007.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah