Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini mauaji ya Rais John F. Kennedy yamegubikwa na utata?
- Author, Claire Thorpe
- Nafasi, BBC
Novemba hii inatimia miaka 60 tangu kuuawa rais wa 35 wa Marekani - John F. Kennedy. Kumbukumbu hii hutoa fursa ya kuyakumbuka na kuyadurusu matukio ya zamani.
Hisia kuhusu kifo cha JFK hazijawahi kupungua. Mara tu baada ya kupigwa risasi huko Dallas, habari kuhusu kifo chake zilianza kuenea na zinaendelea hadi leo.
Maelfu ya vitabu, filamu, vipindi vya televisheni, na sinema za Hollywood zimetolewa kuhusu kile kilichotokea Novemba 22, 1963 na kuushangaza ulimwengu.
Habari mpya bado zinaendelea kuibuka. Hivi karibuni, mlinzi wa zamani wa JFK alitoa habari mpya ambayo ilizua sintofahamu kuhusu maelezo rasmi ya mauaji ya JFK.
Paul Landis, katika kitabu chake kipya cha kumbukumbu, anasema alipata risasi kwenye gari la JFK na kuiweka kwenye machela ambayo rais alikuwa amebebwa.
Hili linaweza kuonekana kama jambo dogo, lakini taarifa hii inaonekana kutofautiana kidogo na taarifa rasmi ya tukio hilo.
Katika ripoti rasmi, risasi ilipatikana kwenye machela ambayo Gavana John B. Connelly alikuwa amewekwa. Ripoti hiyo inasema John B. Connelly alipigwa risasi akiwa katika gari la rais. Mkanganyiko huu unatoa dhana kwamba mshambuliaji Lee Harvey Oswald huenda hakuwa peke yake katika tukio hilo.
"Kuna sababu nyingi za kukata rufaa kuhusu kifo cha JFK. Alikuwa rais wa mfano kwa watu wengi," anasema Peter Laing, Mwenyekiti Mstaafu wa masomo kuhusu Marekani katika Chuo Kikuu cha Nottingham na mwandishi wa wasifu wa John F. Kennedy.
Alikuwa rais wa kwanza wa enzi ya televisheni. Kijana aliyekuwa na mke na watoto.
Katika kitabu cha Laing kinachofuata, kitakusanya baadhi ya barua za rambirambi zilizotumwa kwa mkewe Jackie baada ya kifo cha mume wake. Zilitumwa kutoka kote ulimwenguni na ziko katika Maktaba ya John F. Kennedy huko Boston. Barua hizi zinaonyesha jinsi kifo cha John F. Kennedy kilivyokuwa maarufu.
Siku ya Tukio
Mwaka mmoja baada ya kifo cha JFK, Ripoti ya Warren, iliyoagizwa na Rais Lyndon Johnson, ilitangaza matokeo yake. Kulingana na ripoti hii, Oswald alimpiga risasi Kennedy peke yake.
Alifyatua risasi tatu kutoka kwenye dirisha la ghorofa ya sita ya jengo la Texas Book Depository. Risasi ya pili na ya tatu ilimpata John F. Kennedy nyuma ya kichwa, na risasi ya tatu ndiyo iliyomuua.
Ripoti hiyo ilikataa tuhuma zozote za njama kutoka ndani au nje ya nchi ya kumuua Rais Kennedy na ikaeleza kuwa Jack Ruby alimpiga risasi na kumuua Oswald siku mbili baadaye kutokana na hisia za uzalendo.
"Tatizo la msingi katika mauaji ya Kennedy ni kwamba hatukusikia maelezo ya Oswald kuhusu kilichotokea," anasema Laing. ''Hakupata nafasi ya kufika mahakamani.''
Licha ya mgawanyiko mkubwa - Wamarekani wengi wanakubaliana juu ya jambo moja: Kuna maelezo mengi kuhusu mauaji ya JFK ambayo hatuyajui. Kulingana na utafiti uliofanywa 2017, 61% ya Wamarekani wanaamini watu wengine walihusika katika mauaji haya.
Maelfu ya Machapisho na Filamu
Takriban vitabu 40,000 vimechapishwa kuhusu Kennedy. Wakati huo huo, kuna vitabu vingine vingi kuhusu nadharia mbalimbali za mauaji haya. Nadharia ya kuhusika kwa Urusi, Fidel Castro, wa-Cuba walio uhamishoni, CIA, FBI na vikundi vya wahalifu.
Norman Miller alizama ndani kutafiti maisha ya Oswald katika kitabu chake kiitwacho The Story of Oswald, kilichochapishwa mwaka 1995.
Katika riwaya ya 11.22.63, ya Stephen King anaelezea msafiri ambaye anasafiri kurudi nyuma ya wakati, ili kujaribu kuzuia mauaji ya Kennedy.
James Ellroy anasimulia hadithi ya kifo cha JFK katika kitabu chake cha American Tabloid kwa kutumia wahusika watatu ambao ni maafisa wavunja sheria.
Riwaya ya Don DeLillo ya 1988 Libra inamweka Oswald katikati ya njama ya CIA. Alifanya utafiti kwa miaka mitatu ili kuandika kitabu hiki. Aliliambia gazeti la New York Times, ''ikiwa siku moja kutakuwa na ushahidi wa njama, nina hakika utakuwa ushahidi wa kuvutia zaidi kuliko riwaya yoyote.''
Mauaji haya yameonyeshwa kwenye televisheni kwa njia tofauti. Katika filamu ya 1993 Line of Fire, Clint Eastwood anacheza kama mlinzi anayeitwa Frank Harrigan. Afisa ambaye anatakiwa kumlinda Kennedy siku hiyo huko Dallas.
Katika filamu ya 2019 Jackie, Natalie Portman anaigiza kama mke wa rais katika siku za mwanzo baada ya kifo cha mumewe.
Lakini filamu muhimu zaidi kuhusu mauaji haya ni filamu yenye utata ya Oliver Stone JFK. Filamu hii iliteuliwa katika tuzo nane za Oscar, lakini wakosoaji wanaona ni filamu hatari.
Filamu ya JFK inachanganya picha halisi na za kubuni. Katika filamu hiyo - CIA walitaka kumuua Kennedy kwa sababu alitaka kumaliza Vita vya Vietnam. Filamu hiyo inaeleza CIA hawakutaka Kennedy awe hai ili waendeleze Vita vya Vietnam. Hii ni dhana ambayo wapo Wamarekani wanaoiamini.
Maswai ni Mengi
1992 kutokana na filamu ya Oliver Stone, Bunge la Marekani lilipitisha Sheria ya Rekodi za Mauaji ya John F. Kennedy, ambapo mamilioni ya nyarakia za siri kuhusu mauaji hayo zilitolewa.
Nyaraka hizi zinachapishwa katika vipindi tofauti, na mwaka huu katika utawala wa Joe Biden, mfululizo wa mwisho wa nyaraka hizo ulichapishwa.
"Kitabu cha Landis kinafichua jambo la msingi," anasema Laing. ''Kwa sababu risasi iliyopatikana kwenye machela ya Gavana Connelly, kulingana na ripoti ya Warren, ni risasi ile ile iliyompiga Connelly baada ya kupita kwenye mwili wa Kennedy. Lakini wengi walikuwa na shaka na hilo.''
Lakini Laing bado ana mashaka pia kuhusu ukweli wa taarifa hii mpya. Kwa nini Landis alingoja miaka mingi kufichua habari hii?
Katika mahojiano na Vanity Fair, mwanahistoria James Rubenault anasema anaamini maneno ya Landis: "Hadi sasa, habari hii ni muhimu zaidi kuhusu mauaji ya 1963."
Ni mapema sana kusema ni wapi habari hii mpya itatupeleka, lakini jambo moja la hakika: Watu hawataacha kuhoji kuhusu kile kilichotokea siku hiyo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi