Kipi kipya kwenye bajeti za Tanzania?

BAJETI
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi

“Bajeti ya kulipa madeni, mzigo wa kodi,” ndivyo kinavyosomeka kichwa cha habari cha gazeti moja la kila siku nchini Tanzania. Hii ni bajeti ya pili tangu rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuapishwa Machi 2021.

Nchi nyingine za Afrika Mashariki Kenya, Rwanda na Uganda zimesoma bajeti zake za mwaka 2023/24. Bila kuisahau Zanzibar eneo la Tanzania lenye mamlaka yake ya ndani, imesoma bajeti yake jana katika Baraza la Wawakilishi.

Bajeti ya Kenya ni Ksh trilioni 3.6, sawa na dola za kimarekani bilioni 25.75, Tanzania ni bajeti ya Tsh trilioni 19.23, sawa na dola za kimarekani bilioni 44.38, Uganda ni Ush trilioni 52.74 sawa na dola za kimarekani bilioni 13.9 na Rwanda Rwf 5.03 trilioni sawa na bilioni dola za kimarekani 4.4.

Sura ya bajeti ya Tanzania

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliwasilisha bajeti ya serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2023/2024, huku mafungu makubwa mawili ya fedha zilizotengwa ni ulipaji madeni na uendeshaji wa shughuli za utawala.

Katika fedha hizo Sh trilioni 6.31 zitatumika kulipa deni la taifa, huku shilingi trilioni 11.89 zitapelekwa kutoa huduma ya utawala. Katika sekta ya elimu serikali itatumia trilioni 5.95, ulinzi na usalama shilingi trilioni 4.68, ujenzi, usafirishaji na mawasiliano shilingi trilioni 3.84, na nishati itatumia shilingi trilioni 3.05.

Hifadhi ya jamii serikali imepanga kutumia trilioni 2.35, kilimo shilingi trilioni 1.47, maji, nyumba na maendeleo ya jamii trilioni 1.34 na shughuli nyingine za maendeleo ya uchumi, serikali imepanga kutumia shilingi trilioni 1.07.

Kodi, Tozo na Ushuru

Mwanamke

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akiwasilisha bajeti – amebaisha maeneo ambayo kodi zitaongezeka, ushuru na tozo. Tukianza na kodi ya shilingi 100 kwa kila lita moja ya dizeli na petroli itakayo uzwa nchini Tanzania.

Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia na kuhakikisha kodi husika za Serikali kupitia matangazo yanayowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Twitter na Blogs zinalipwa kwa wakati.

Hutuba ya Waziri pia imependekeza kuongeza tozo ya michezo ya kubahatisha kutoka shilingi 10,000 hadi Shilingi 30,000 kwa kila mashine ya Sloti kwenye maeneo ya baa (sehemu za kuuzia pombe).

Kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 30 kwenye sigara na bidhaa za aina hiyo zinazotumia mbadala wa tumbaku, sigara za kieletroniki, shisha na tumbaku inayovutwa kwa bomba. Pia, lipo pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye magari ya abiria yanayoingizwa Tanzania yanayozidi umri wa miaka mitano.

Kwa upande mwingine watoto wameguswa, bajeti inapendekeza kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye taulo za watoto (baby diapers). Lengo likiwa ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha taulo hizo

Nafuu ya bajeti

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bajeti pia imeleta nafuu katika baadhi ya maeneo. Ina pendekezo la kuanzishwa programu ya mikopo kwa wanafunzi waliochaguliwa katika vyuo vya kati. Itakumbukwa kuwa nchini Tanzania, wanafunzi wanao anza shahada ya awali ndio hupata mikopo.

Pia, kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi vya Dar es Salaam Institute of Technology – DIT, Mbeya University of Science and Technology – MUST na Arusha Technical College

Nafuu nyingine, kuanzia Julai 01, 2023, iwe ni marufuku kwa Taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali. Amesema ufungiaji biashara una athari kubwa kwa ustawi wa uchumi wetu kwa kuathiri ajira za wananchi, ustawi wa biashara, mapato ya kampuni na mapato ya Serikali

Hotuba imependekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye uuzaji na ukodishaji wa ndege, injini za ndege na vifaa vyake vinavyouzwa nchini, ili kutoa unafuu kwa waendeshaji wa shughuli za usafiri wa anga kwa kuwawezesha kununua bidhaa husika nchini au kuagiza kutoka nje ya nchi bila kulipa kodi ya ongezeko la thamani.

Lipo pendekezo la kusamehe ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa mujibu wa uwezo wa injini, kwenye magari yanayotumia umeme pekee na magari yanayotumia nishati ya gesi asilia pekee.

Fauka ya hayo, kupunguza ushuru wa bidhaa kutoka shilingi 4,386 kwa lita hadi shilingi 2466.45 kwa lita kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa ndani ya nchi. Lengo likiwa ni kuvilinda viwanda vya ndani.

Bajeti inapendekeza kupunguza ada ya hati miliki kutoka shilingi 50,00 kwa hati hadi shilingi 25,000 kwa hati. Vile vile, kufuta tozo kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa mtumiaji.

Na wafanya biashara wa nyumba bajeti imewaona. Inapendekeza kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye nyumba zinazouzwa na wajenzi wa nyumba za kibiashara zenye gharama nafuu isio zidi milioni 50.

Hali ikoje Zanzibar?

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), nayo imetangaza Bajeti ya 2023/24, ambayo ni Shilingi za Kitanzania trilioni 2.8. Kuna ongezeko ukilinganisha na bajeti ya yake Shilingi trilioni 2.6 ya mwaka 2022/23.

Maeneo mengine ni yale ya usambazaji wa huduma za jamii ikiwemo sekta elimu, afya, usambazaji wa huduma za maji serikali inatarajia kutumia Sh338.8 bilioni kutekeleza miradi mbalimbali.

Katika eneo la mbio za uchumi wa buluu, Zanzibar imepanga kuwawezesha wajasiriamali kwa kuongeza thamani mazao ya baharini na kukuza mitaji yao mradi, katika eneo hilo bilioni 23.5 fedha za Serikali zitatumika.

Waswahili husema, ‘mipango si matumizi,’ wakati nchi za Afrika Mashariki zikimaliza kusoma bajeti zao – macho ya wananchi ni kusubiri utekelezaji wa ahadi kedekede, zilizopo katika bajeti hizo. Vilevile, kujiandaa kulipa ushuru, kodi na tozo katika maneno ambayo mambo hayo yameongezeka.