WARIDI WA BBC:‘Najuta kwenda Saudia Arabia kufanya kazi za nyumbani’

Na Anne Ngugi

BBC Swahili,Nairobi

th

Chanzo cha picha, Hellen

Raha kugeuka kuwa karaha.Ndio muhtasari unaoweza kubeba matumaini ya Hellen Ndege yaliyoyeuka pindi alipokanyaga ardhi ya Saudi Arabia .

Mpango wake ulikuwa rahisi sana-kwenda nchi hii ya kigeni kufanya kazi za nyumbani kwa miaka ili kuboresha maisha yake.Tatizo ni kwamba kitumbua kilipoingia mchanga,haikuwa rahisi yeye kurejea nyumbani kama alivyotamanI.Tayari alikuwa amejinasa kwa minyororo ya mikataba alioitia saini kabla ya kuanza safari yake .

Hellen aliwasili Saudia mwaka wa 2019 na misheni yake kwa kauli yake mwenyewe ilikuwa hii:

‘Mimi nimepitia shida nyingi sana kabla sijaamua kusafiri hadi nchi ya Saudia kutafuta riziki .

Nilikuwa nimeacha shule nikiwa darasa la sita na nilihisi kwamba njia pekee ya kufaulu pamoja na kuisaidia familia yangu kumaliza umaskini ni kusafiri kwenda nje ya nchi ”

 Kwanini alikubali kusafiri Saudi Arabia ?

th

Chanzo cha picha, Hellen

Fursa ya kwenda Saudi Arabia ilipochipuka hakufikiria mara mbili kuhusiana na yale yaliokuwa mbele . Anasema kwamba alikuwa ameyasikia masaibu mengi ambayo yalikuwa yamewapata baadhi ya wasichana wa kazi za nyumbani waliokuwa wamesafiri katika nchi tofauti mashariki ya kati , ila kwake alikuwa na matumaini kwamba angeyavumilia yote ilimradi aafikie ndoto za kuaga umasikini .

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kati ya siku ambazo hawezi kuzisahau ni tarehe 9 mwezi Februari mwaka wa 2019 ambako alijificha wakati akiondoka kusafiri Saudia ili mtoto wake wa kiume asimuone akiondoka .

Mama huyu alihisi uchungu kumuacha mtoto wake wakati huo akiwa na miaka minne , ila kimoyomoyo aliona miaka miwili kama muda mfupi kuafikia malengo yake .

Baada ya kuwasili Saudi Arabia Hellen anasema kwamba yeye alipokewa na baba na mama kutoka jamii iliyokuwa imempa kandarasi ya kufanya kazi na moja kwa mmoja kuelekea nyumbani kwao .

Kulingana na mwanadada huyu ,japo alikuwa amefanya kazi za nyumbani nchini Kenya kwa miaka zaidi ya 10 alianza kuwa na changamoto kuanzia siku ya kwanza kwa sababu ya changamoto ya lugha na mawasiliano yakawa magumu na mwajiri wake .Pia joto lilikuwa kali na kwa sababu ya kutozoea hali hiyo ilipata usumbufu mkubwa sana .

 Imani yake kwamba mambo yangeboreka ilisalia kuwepo na akapiga moyo kondo kuyafumbia macho mambo hayo akifikiri ni madogo sana kumzuia kutimiza malengo yake .

Hata hivyo siku zilivyozidi kwenda aligundua kwamba kazi zilikuwa ni nyingi mno na kila siku alikuwa akilazimika kuamka asubuhi na mapema na kulała nyakati za usiku wa manane mara nyingi saa kumi za asubuhi .

Unaweza pia kusoma
th

Chanzo cha picha, Hellen

Kando na hayo kulikuwa na kazi nyingine za kuhakikisha kwamba ameandaa mapishi kwa wakati , anadai kwamba wenye nyumba walikuwa hawaingii jikoni na ilikuwa kazi yake kulingana na kandarasi aliyotia sahihi .

Hellen anasema kwamba baada ya miezi 9 ya kwanza kufanya kazi alihisi kwamba wakati ulikuwa umefika kwake kurudi nyumbani - Kenya , lakini kikwazo kikawa ni kandarasi yake .

Jaribio lake la kutoroka liligonga mwamba kwani kwa sababu kwa mujibu wa masharti ya mkataba wake ,lazima angefanya kazi kwa mwajiri yul kwa miaka miwili . Dhulma dhidi yake zilikuwa zimekuwa jambo la kawaida na kwa uvumilivu aliendelea kufanya kazi .

Hellen anasema kwamba wakati alipoanza kazi walikuwa wamekubaliana na mwajiri wake kwamba angepokea karibu dola mia mbili hamsini kila mwezi au Riyal mia tisa kila mwezi .Mwanadada huyu anasema kwamba aliamua kuhakikisha kwamba ametuma Riyal mia tano nyumbani kwa sababu ya mahitaji ya mtoto wake na kisha Riyal mia nne zilizosalia aliamini tajiri wake angemuekea akiba hadi wakati angerudi nchini Kenya .

Kwa muda anasema mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 29 mzaliwa wa magharibi mwa Kenya anasema alivumilia kila hali ya kazi na pia maisha ya kufanya kazi bila kupumzika .

Unyanyasaji wa Kingono

TH

Chanzo cha picha, Hellen

Hellen anakumbuka tukio la kuogofya siku moja mbapo mwajiri wake mama mwenye nyumba alikuwa ametoka na wanawe kwenda kujivinjari kama ilivyokuwa ada yao katika siku maalum .Baba mwenye nyumba alirejea nyumbani ghafla na alipoingia katika nyumba aliifunga milango yote .

 Alimtaka amuandalie kahawa jikoni na alipokuwa akifanya hivyo alimshtukiza na kumshika kwa nguvu ,mapambano ya dakika kama thelathini yalitokea huku lengo la mwajiri wake huyo likiwa kumdhullumu kimapenzi .Hellen alijaribu kupiga ukemi lakini alifahamu hilo halingemsaidia kwani jumba lenyewe lilikuwa kubw ana hakuna aliyweza kumsikia .

Afueni yake ilitokea wakati simu ya nyumba alipopigwa na mwajiri wake akaacha kwa muda kumshika kwa nguvu na ndipo alipopata nafasi ya kukimbia hadi bafuni alikojifungia hadi mama mwenye nyumba na watoto wake waliporejea .

‘Kisa hiki kilinisukuma kupigana kurudi nyumbani kwa vyovyote vile , niliogopa kumueleza mtu yeyote kuhusiana na yaliyojiri.Hofu yangu kuu ilikuwa kwamba hakuna ambaye angeniamini na nilihofu kwamba ningesingizwa lawama kwa kilichotokea .Niliamua kutafuta ajenti walionileta hadi huko’

Baada ya hapo Hellen alianza kutafuta kila mbinu kupiga simu nyumbani katika juhudi za kutaka ujumbe uwafikie mawakala wake nchini Kenya kwamba yeye alikuwa hana amani na alitamani arejee kutokana na tishio la dhuluma dhidi ya maisha yake .

TH

Chanzo cha picha, Hellen

Mchakato wa kurudi Kenya ulianza wakati mawakala wake kwa upande wa nchi ya Saudi Arabia walianza mawasiliano na mwajiri wakitaka aheshimu kandarasi yake ambayo ilikuwa inakaribia kufika mwisho wake baada ya miaka miwili .Hellen anasema kwamba hakuwahi kufunguka kuhusiana na jaribio ya ubakaji kwa uwoga .Anaongeza kwamba alichotamani sana wakati huo ni kurudi nyumbani

Tarehe 6 mwezi mei mwaka huu Hellen aliraushwa mapema na tajiri wake na kuelezwa kwamba alifaa kufunga safari ya kurudi Kenya , aliambiwa kwamba tiketi yake ya ndege ilikuwepo na hata kuwa na muda wa kujitayarisha . 

Kinachompa machungu sana kando na mateso mengi aliyoyapitia akiwa huko ni kwamba kati ya pesa takriban Riyal alfu kumi na tatu ambazo mwajiri wake alikuwa amemuwekea kama akiba yake kutoka kwa mshahara wake wa kila mwezi mwanadada huyu anadai kwamba tajiri wake aliamua kumlipa nusu ambayo ni Riyal 6500.Jasho lake la miaka miwili aliyojinyima mengi halikuzaa matumaini aliyoyabeba akienda nchini humo .

Hata hivyo Hellen anafuraha kwamba alirudi akiwa mzima wa afya .

Anasema kwamba changamoto kuu inayowakabili wasichana wengi wanaokwenda uarabuni kwa kazi za ndani ni ukosefu wa habari kuhusiana na jinsi ya kujilinda wakati shida inapowapata na hasa kwa kuwa hawaelewi mazingira wanayoyaishi pamoja na mila na desturi za huko .

 Cha pili anasema kwamba wengi wa waajiri wa huko wanawaona wasichana kama Hellen kama watumwa , hii inatokana na kwamba wanalipa pesa nyingi kupitia mawakala ili kuajiri wasichana wa kazi za ndani kutoka nchi mbali mbali Afrika na pia bara Asia

Kwa sasa Hellen ameanza biashara ya uuzaji dagaa viungani mwa mji wa Nairobi na anasema kwamba anatosheka na kidogo anachopata .