Papa na viongozi wa Kiprotestanti washutumu sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Papa Francis alisema wale wenye "mielekeo ya mapenzi ya jinsia moja " wanapaswa kukaribishwa na makanisa yao

Papa Francis na viongozi wa makanisa ya kiprotestanti nchini Uingereza na Scotland wameshutumu kuharamishwa kwa uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja.

Wakizungumza na wanahabari baada ya kuzuru Sudana Kusini, Papa alisema sheria hizo ni dhambi na ukiukaji wa haki.

Aliongeza kwamba watu wenye "mielekeo ya mapenzi ya jinsia moja" ni watoto wa Mungu na wanapaswa kukaribishwa na makanisa yao.

Maoni yake yaliungwa mkono na Askofu Mkuu wa Canterbury na Msimamzi wa Kanisa la Scotland.

Askofu Mkuu Justin Welby na Iain Greenshields, Msimamizi wa Baraza Kuu la Kanisa la Scotland, walisafiri na Papa hadi Sudan Kusini ambako kwa pamoja walitoa wito wa amani katika nchi hiyo yenye vita.

Ni mara ya kwanza kwa viongozi wa makanisa hayo matatu kukutana pamoja kwa safari kama hiyo katika miaka 500.

Askofu Mkuu Welby na Dk Greenshields walisifu maoni ya Papa wakati wa mkutano na wanahabari waliokuwa kwenye ndege ya papa walipokuwa wakisafiri kutoka Juba kuelekea Roma.

"Ninakubaliana kabisa na kila neno alilosema hapo," alisema Askofu Mkuu Welby, akibainisha kuwa kanisa la Anglikana lilikuwa na mgawanyiko wake wa ndani kuhusu haki za wapenzi wa jinsia moja.

Mwezi uliopita Kanisa la Uingereza lilisema kuwa litakataa kuwaruhusu wapenzi wa jinsia moja kufunga ndoa katika makanisa yake.

Akitoa uungaji mkono wake mwenyewe, Dakt Greenshields alinukuu Biblia, akisema: “Hakuna mahali popote katika Injili nne ambapo ninaona kitu chochote isipokuwa Yesu akionyesha upendo kwa yeyote anayekutana naye, na tukiwa Wakristo huo ndio usemi pekee tuwezao kumpa binadamu yeyote katika hali yoyote ile".

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Askofu Mkuu Justin Welby (kulia) na Mchungaji Iain Greenshields (kushoto) walionyesha kuunga mkono maoni ya Papa katika mkutano na waandishi wa habari.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari Papa Francis alirudia maoni yake kwamba Kanisa Katoliki haliwezi kuruhusu ndoa za kisakramenti za wapenzi wa jinsia moja.

Lakini alisema anaunga mkono kile kinachoitwa sheria ya muungano wa kiraia, na kusisitiza kuwa sheria zinazopiga marufuku mapenzi ya jinsia moja ni "tatizo ambalo haliwezi kupuuzwa".

Alisema kuwa takriban nchi 50 zinawafanya watu wa LGBT kuonekana wahalifu "kwa njia moja au nyingine", na takriban 10 zina sheria zinazobeba hukumu ya kifo.

Hivi sasa nchi 66 wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja, kulingana na ILGA World - Jumuiya ya Kimataifa ya LGBTQ .

"Hii si sawa. Watu wenye mielekeo ya mapenzi ya jinsia moja ni watoto wa Mungu," Papa alisema.

"Mungu anawapenda. Mungu anaandamana nao... kumhukumu mtu wa namna hii ni dhambi."

Chini ya mafundisho ya sasa ya Kikatoliki, mahusiano ya wapenzi wa jinsia moja yanajulikana kama "tabia potovu" na Papa Francis hapo awali alisema "ana wasiwasi" na "suala zito" la wapenzi wa jinsia moja miongoni mwa makasisi.

Lakini baadhi ya Wakatoliki wa kihafidhina wamemkosoa kwa kutoa maoni wanayosema yana utata kuhusu maadili ya tendo la ngono.

Mnamo 2013, mara tu baada ya kuwa Papa, alisisitiza msimamo wa Kanisa Katoliki kwamba vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ni dhambi, lakini akaongeza kuwa mwelekeo wa ushoga sio.

Miaka mitano baadaye, wakati wa ziara yake nchini Ireland, Papa Francis alisisitiza kwamba wazazi hawawezi kuwakana watoto wao wa LGBT na walipaswa kuwaweka katika familia yenye upendo.