Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano Tanzania: Serikali yaijibu jamii ya kimataifa
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Serikali ya Tanzania imeijibu jamii ya kimataifa kufuatia tamko lao kuhusu matukio ya uchaguzi wa Okober 29 nchini humo yaliosababisha maafa ya raia.
Hatua hiyo inajiri baada ya balozi 16 za nchi za magharibi kutoa ripoti za ukiukwaji mkubwa wa mfumo wa haki za binadamu nchini Tanzania baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Serikali imesema imesikitishwa pakubwa na baadhi ya matamshi yaliotolewa na jamii hiyo.
Huku ikitambua umuhimu wa jamii ya kimataifa katika kukuza demokrasia , Tanzania imesema kuwa balozi za mataifa hayo zinapaswa kuheshimu hatua zilizochukuliwa na taifa hilo katika uundaji wa tume inayochunguza matukio ya ghasia za uchaguzi.
Serikali imesema kwamba matukio ya ripoti ya tume hiyo itatoa uelewa kuhusu yaliojiri wakati wa ghasia hizo, hatua itakayoleta majadiliano katika siku zijazo.
Aidha taarifa hiyo imesema kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na jamii ya kimataifa ili kuleta maenedeleo na amani nchini humo , lakini ikatoa wito kwa jamii hiyo kuheshimu kutekelezwa kwa hatua zilizochukuliwa na serikali .
Imeongezea kwamba serikali iko tayari kundelea kushirikiana na jamii hiyo katika kila sekta mbalimbali kwa usawa.
Lakini zikizungumza tarehe 4 mwezi Novemba, balozi hizo katika ripoti yao zilisema, ripoti hizo zinajumuisha tuhuma za mauaji ya kiholela ya mamia ya watu, kutekwa nyara kwa nguvu, na kuwekwa kizuizini kiholela kwa maelfu hususan waandamanaji, viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kiraia katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Walisisitiza kwamba Serikali ya Tanzania ina wajibu wa kutoa taarifa ya kina kuhusu hatima na mahali waliko watu wote waliotekwa nyara.
''Ukamataji watu kiholela na ufichaji wa mili ya waliopoteza maisha. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi mili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu''
''Zaidi, tunatoa wito kwa serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa AU na SADC ambazo ziliweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa mchakato wa uchaguzi''.
Aidha, walitaka serikali kuondoa mara moja vikwazo vyote vinavyokwamisha uhuru wa vyombo vya habari, wakisema vikwazo hivyo vinakiuka wajibu wa kimataifa wa Tanzania chini ya mikataba ya haki za binadamu.
''Tunatambua azma ya serikali ya kudumisha amani na utulivu wa nchi, na tunasisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao''.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, uchaguzi ulifanyika katika mazingira yenye mashaka ya muda mrefu, ikiwemo kukamatwa kwa viongozi wa upinzani bila utaratibu wa kisheria, kutoweka kwa baadhi yao kwa kulazimishwa, na mabadiliko ya kisheria yaliyopunguza uadilifu wa mfumo wa uchaguzi.
Marekani kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania
Hapo jana, Marekani ilisema kuwa inatathimini upya uhusiano wake na Tanzania kufuatia mauaji ya raia wengi wakati wa uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani, ilisema kuwa licha ya uhusiano wake wa muda mrefu uliostawi kati yake na taifa hilo, hatua ya hivi karibuni ya taifa hilo imezua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa uhusiano huo.
Imesema kwamba matukio yanayoendelea kufanywa na serikali ya Tanzania ya kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza , kuwepo kwa vikwazo vya mara kwa mara dhidi ya uwekezaji wa Marekani na ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi ni mambo inalolifanya taifa hilo kutathmini upya uhusiano huo.
Taarifa hiyo ilisema kwamba vitendo hivyo vinawaweka raia wa Marekani , watalii na maslahi ya Marekani nchini tanzania hatarini na kutishia kudhoofisha ustawi na usalama wa pamoja ambao umekuwa alama ya ushirikiano wetu kwa miongo kadhaa.
Imeongezea kwamba Marekani haiwezi kufumbia macho 'vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia wetu, au usalama na utulivu wa kanda'