'Who are you?' na hoja 6 zilizotikisa hotuba ya Rais Samia

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wazee kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa hotuba ndefu na yenye uzito wa kisiasa ambayo imeibua mjadala mkali ndani na nje ya nchi.

Hotuba hiyo, ambayo ilichukua takribani saa moja, iligusa masuala kadhaa ambayo BBC imeyachambua kupata hoja sita kubwa: Hali ya upinzani, urithi wa urais 2030, nafasi ya mataifa ya nje kwenye siasa za Tanzania, msimamo wa viongozi wa dini, ghasia za Oktoba 29, na taarifa za maandamano yanayodaiwa kupangwa Disemba 9.

Kauli za Rais zinakuja katika kipindi ambacho nchi iko katika mjadala mkali kuhusu mustakabali wa demokrasia, marekebisho ya kisiasa, na nafasi ya vyombo vya dola kufuatia kilichoelezwa na serikali kuwa "vurugu zilizopangwa" wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

1. "Upinzani umeishiwa pawa"

Rais Samia alielekeza mashambulizi ya kisiasa kwa vyama vya upinzani, akidai vilikuwa vimepoteza mvuto na nguvu hata kabla ya uchaguzi kufanyika. Alitumia neno "pawa", likiwa rejea ya wimbo wa msanii maarufu Mbosso wa Tanzania kueleza kudhoofu kwao. Hili linaashiria mtazamo wa serikali kuwa hoja za upinzani kutoshiriki uchaguzi hazikuwa za msingi bali za kujihami kisiasa.

Katika maelezo yake, Rais alisema baadhi ya vyama vilitafuta visingizio ili kuepuka aibu ya kushindwa, akitaja kuwa nguvu za nje pia zilikuwa zikiwapa moyo bandia. Chadema, chama kikuu cha upinzani, hakikushiriki uchaguzi huo kikitaka kwanza mabadiliko ya sheria na katiba, huku ACT Wazalendo likipata pigo baada ya mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina, kuenguliwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) jambo ambalo Rais alihusisha na ushindi mkubwa wa CCM wa asilimia 97%.

Rais Samia alihoji nia ya vyama ambavyo vinadai masharti kabla ya mazungumzo ya maridhiano, akieleza kuwa kuna shinikizo kutoka nje ya nchi ambalo halikubaliki. Alisema:

"Tumesema tuzungumze, lakini wengine wanakuja na masharti, 'mumuachie huyu, mfanye hili na hili'. Huu si utaratibu wa nchi inayoheshimu mamlaka yake."

Akionekana kupeleka ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa, alisisitiza kuwa Tanzania itafanya mazungumzo kwa misingi ya usawa, si kwa mashinikizo.

2. Mbio za urais 2030: "Safari hiyo isiende kutuvurugia nchi yetu"

Katika moja ya sehemu zilizovuta hisia za wengi, Rais Samia aligusia mjadala unaoibuka wa nani atamrithi mwaka 2030 atakapomaliza muhula wake wa mwisho kikatiba. Aliwatahadharisha wanasiasa wanaoanza kujipanga mapema, akisema safari ya madaraka isiingilie utulivu wa nchi.

"Watoto wangu wanaoangalia mbele 2030, safari hiyo isiende kutuvurugia nchi yetu," alisema.

Rais alifichua kuwa tayari ameshawaonya baadhi ya mawaziri wake ambao anahisi wana muamko wa urithi wa madaraka. Aliwasisitizia kuwa iwapo wana nia ya kugombea urais, basi wafanye hivyo nje ya Serikali yake ili kuepusha mgongano wa maslahi.

"Niliwaambia: una interest (unautaka urais) huko? Kaa nje, kafanye huko. Usifanye ukiwa ndani ya serikali yangu," alisema akionyesha kutoridhishwa na kampeni za kimyakimya zinazodaiwa kuanza serikalini.

Kauli yake pia ilijikita katika imani ya kwamba Mungu ndiye anayechagua kiongozi wa taifa. Alisema suala la urithi wa madaraka halipaswi kugeuzwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya chama au taifa.

"Mungu ndiye anajua nani kiongozi wetu baadae. Ni Mungu peke yake," alisisitiza, akitaka mjadala wa urithi wa madaraka ufanyike kwa staha na wakati mwafaka.

3. Mabeberu wanyooshewa vidole: "Who are you?"

Moja ya sehemu kali zaidi za hotuba hiyo ni pale Rais alipolenga mataifa ya nje, akisema yamekuwa yakitoa maagizo kuhusu jinsi Tanzania inavyopaswa kuendesha mambo yake. Alisema Tanzania haiwezi kukubali kudhibitiwa au kuwekewa masharti kwa kisingizio cha misaada au ushirikiano.

"Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye hivi, ifanye vile… (wao kina nani) who are you? Wanadhani wao bado ni masters (watawala) wetu?" alihoji.

Alisisitiza kuwa baadhi ya mashinikizo ya kimataifa yanatokana na tamaa ya kutaka kufaidika na rasilimali za Tanzania, hususan madini adimu ambayo nchi inamiliki.

Kwa mujibu wake, Tanzania imekuwa ikilengwa kwa sababu ya utajiri wake wa kiasili, na iwapo wazawa hawatakuwa waangalifu, rasilimali hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa.

"Maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana tukauana sisi kwa sisi kwa kushawishiwa na wanaotolea macho nchi yetu," alisema.

Kwa msisitizo mkali, Rais aliwataka Watanzania kushikamana na kutoacha tofauti za kisiasa au ushawishi kutoka nje kuigawa nchi. Alisisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kujiendesha kwa amani kama raia wake wanatoa mwanya kwa nguvu za nje kuingilia mambo yao ya ndani.

4. Viongozi wa dini: "Matamko 8 yametolewa na TEC"

Rais Samia pia alizungumzia nafasi ya viongozi wa dini kufuatia matamko kadhaa yaliyotolewa na taasisi mbalimbali, hususan Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuhusu utekaji, haki za binadamu, na upungufu wa demokrasia nchini. Alisema baadhi ya matamko hayo yamekuwa yakiibua mpasuko na hayajengi.

"Hatujaipa dini yoyote mamlaka ya kutoa tamko la ku-override (kubatilisha) mengine," alisisitiza, "Tanzania hatutaendeshwa na madhehebu ya dini".

Aliongeza kuwa hata ndani ya taasisi hizo, kuna mgongano wa maoni unaoonyesha kuwa matamko si mwafaka wa pamoja.

"Matamko manane yametolewa na TEC, lakini ukienda chini wenyewe wanapingana. Waliosimama kwenye haki wanaona ni batili iliyofanyika," alisema.

Samia alikumbusha kwamba mamlaka za nchi hutoka kwa Mungu iwe ni kiongozi mwanamume au mwanamke na kwamba hakuna kitabu cha dini kinachokubali kutumia imani kama chombo cha kuleta vurugu. Alisema wachache wanaogeuza dini kuwa chombo cha kisiasa wanatakiwa kujitafakari.

"Hakuna kitabu chochote cha dini kimesema tutazitumia dini zetu kuvuruga nchi. Ni ubaya wa nafsi za watu," alisema.

5. Vurugu za Oktoba 29: "Wanadai haki, haki gani?"

Sehemu ya tano ya hotuba ya Rais iligusia ghasia za Oktoba 29, 2025 ambazo serikali ilizitaja kuwa jaribio la kuleta mapinduzi. Aliyaelezea maandamano hayo kama vurugu zilizopangwa kwa ustadi na makundi yaliyotaka kuichafua nchi kwa makusudi yakiwa na mkono wa nje ya nchi.

"Yale hayakuwa maandamano. Zilikuwa vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalumu," alisema kwa msisitizo.

Rais alidai vijana wengi waliojitokeza hawakuwa na uelewa wa agenda waliyopewa, akisema waliingizwa barabarani kama "makasuku" waliotamkiwa maneno wasiyoyajua.

"Vijana wetu waliimbishwa wimbo wasioujua. Wanadai haki, haki gani? Kwa njia ipi? Hadi wachome vituo?" alihoji.

Aidha, aliweka mzigo kwa wazazi, akisema wanapaswa kuwazuia vijana wao kushiriki maandamano ya vurugu. Alisema majonzi yanayotokea ikiwa ni pamoja na vifo na majeraha yanazuilika endapo wazazi wangeingilia kati mapema.

"Unaporudi leo mzee na kulia kijana wako ameumia au amekufa… ulishindwa nini kumzuia?" alisema kwa hisia.

6. Maandamano ya Disemba 9: "Wakija, tumejipanga wakati wowote"

Rais aligusia katika hotuba yake kuhusu taarifa za maandamano mapya yanayodaiwa kupangwa kufanyika Disemba 9 siku ya Uhuru na baadaye mipango mingine wakati wa sherehe za Krismasi. Alisema serikali ina taarifa za maandalizi hayo na imejipanga kikamilifu kukabiliana nayo ama Disemba 9 ama Krismasi kama yatahairishwa.

"Kwa maneno tunasikia liko jengine linapangwa, lakini inshallah mola hatasimama nao litapeperuka.."alisema.

Alitoa onyo kali kwa waandaaji, akisisitiza kuwa dola haitasita kuchukua hatua endapo kutajitokeza dalili za vurugu.

"Wakati wowote wakija, tumejipanga," alisema, akiongeza kuwa tofauti za kisiasa zina njia sahihi za kufikishwa. "Kama humpendi Samia, hakuna haja ya kuvuruga nchi."