Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano Tanzania: Serikali yamburuza Mahakamani mwanaharakati Mange Kimambi
Serikali ya Tanzania imemfungulia mashataka ya kiuchumi mwanaharakati Mange Kimambi ambaye anayeishi nchini Marekani.
Tovuti rasmi ya Mahakama nchini Tanzania, inaonesha kuwa kesi hiyo itatajawa kwa mara ya kwanza Alhamisi wiki hii ya Disemba 4, 2025.
Hakuna maelezo zaidi katika tovuti juu ya mashtaka hayo yanayomkabili Mange.
Hatahivyo gazeti la Citizen limeripoti kuwa kesi hiyo itasikilizea mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Shauri hilo liliwasilishwa na upande wa mashtaka Agosti 28 mwaka huu.
lakini hatua hii inakuja mwezi mmoja baada ya mwanasheria mkuu wa serikali nchini humo Hamza Johari kumlaumu mwanaharakati huyo kwa kuchochea maandamano ya ghasia yaliyotokea katika Oktoba 29 2025 siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Maandamano hayo yameripotiwa kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali za umm ana binafsi.
Johari alisisitiza kuwa watachukua hatua dhidi ya mwanaharakati huyo na kusema kuwa lazima akamatwe.
"Haiwezekani mtu mmoja amekaaa nje ya Tanzania, dada tu hata ukimuangalia muonekane wake anawaambia watu wakafanye hivyo na wanaenda kufanya kweli, halafu imetokea anaanza kutamba, anasema bado ntakuja kivingine, lazima tumkamate", alisema Mwanasheria huyo mkuu.
Pengine hatua ya sasa ni utekelezaji wa kile alichokisema Johari.
Mange Kimambi 'anayesugua vichwa' ni nani hasa?
Mange Kimambi ni mwanamitindo aliyebadilika kuwa mwanaharakati wa siasa, ndie muasisi wa maandamano yaliyotokea octoba 29 kwa kupinga kile anachokiita kuwa ni muendelezo wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uminywaji wa haki za kiraia nchini Tanzania.
Amekuwa akihamasisha mabadiliko ya kimfumo ikiwemo tume ya uchaguzi, katiba mpya, kupinga rushwa na viongozi kujilimbikiza mali.
Amekua akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii ambayo yanawafuasi wengi kutoka Tanzania.
Mange ni mama wa watoto watatu anayeishi Los Angeles, nchini Marekani. Harakati za Mange kupinga serikali ya Tanzania zilianza tangu wakati wa rais wa awamu ya tano John Magufuli takribani miezi sita tu baada kuingia madakari na rais huyo kupinga kuonyeshwa mubashara kwa mikutano ya bunge. Alijaribu bila mafanikio kuitisha maandamano wakati wa Magufuli Aprili 2018.
Mange, akiwa na wafuasi karibu milioni tatu kwenye ukurasa wake wa Instagram miaka minne iliyopita alitumia umaarufu wake mitandaoni kumuunga mkono Rais Samia alipoingia madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake John Magufuli, na hata kuhudhuria katika ziara yake ya kwanza nchini Marekani na wawili hao walipiga picha. Hata hivyo, mambo yakabadilika na leo hii anautumia ukurasa huo huo na ushawishi wake kumpinga.
Mange ni mmoja wa watu wa awali nchini Tanzania miaka ya mwanzo ya 2000, kufungua blogu na kuzungumzia maisha yake na marafiki zake pamoja na mitindo ya mavazi. Lakini Mange alizungumzia pia habari binafsi mbalimbali za watu maarufu waishio ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo walimbwende, wanamuziki na waigizaji filamu.
Kutoka urembo mpaka uanaharakati na udaku
Katika miaka ya hivi karibuni Mangi aliendeleza kazi hiyo na kutengeza 'app' ambayo alijikita kutengeneza maudhui ya udaku, umbeya na mitindo ya maisha ya watu maarufu. Lakini app hiyo pia ilikuwa ikichapisha video za utupu ama ngono za watu maarufu zilizovujishwa ambazo zilifahamika zaidi nchini Tanzania kama 'connection'.
Lakini baadae kujikitia kutumia kurasa zake kwa harakati za kisiasa na kukosoa serikali ya Samia Suluhu.
Mange, ambaye aliwahi pia kuomba ridhaa ya uteuzi kutoka Chama Cha Mapinduzi kuwania nafasi ya ubunge jijini Dar es Salaam, amejikusanyia wakosoaji wengi kama ambavyo alivyo na mashabiki wengi.
Wakosoaji wake wengi wamekuwa wakipuuza harakati zake za kisiasa kwa kile wanachodai kuwa wakati mwingine Mange amekuwa akitumia lugha ya matusi na isiyo na staha hasa anapomkosoa Rais na viongozi wengine wa serikali.
Lakini kwa wanaomuunga mkono, ukurasa wa Instagram wa Mange umekuwa jukwaa lao la kupaza sauti kuhusu changamoto za huduma za kijamii na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini Tanzania
Wakati ambapo shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani zimedhibitiwa na watu kadhaa wamekamatwa na kushtakiwa kwa kuikosoa serikali kwa namna ambayo mamlaka haikupendezwa nayo, ukurasa wa Instagram wa Mange umefanyika sauti kuu kwa wakosoaji wengi wa serikali ya Samia.
Na inaonekana serikali imekuwa ikimtilia maanani.
Wakosoaji wa serikali na wanaharakati wa haki za binadamu wameendelea kuonya kwamba haki za kisiasa na uhuru vyombo vya habari na watu kujieleza imeendelea kuminywa nchini Tanzania. Hata hivyo serikali imekuwa ikitupilia mbali madai haya.