'Nilinyimwa huduma katika mgahawa kwasababu ya uso wangu'

Ingawa likabiliwa na kudhalilishwa na uonevu wa kikatili alipokuwa akiwa mtoto, Amit Ghose anasema bado analazimika kuhangaika kitendo cha watu kumshangaa mara kwa mara, kummyooshea kidole na kutolewa maoni, na hata amenyimwa huduma katika mkahawa kwasababu ya uso wake.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 35 kutoka Birmingham nchini Uingereza alielezea jinsi alipotembelea mgahawa huru huko London hivi karibuni ambapo "kila mtu alikuwa akinitazama, na ilikuwa kama walikuwa karibu kuona shetani".
"Mtu anayehudumu alinitazama na kusema: 'Ah, tumeacha kutoa huduma'.
"Aligeuka na kuondoka. Lakini ni wazi, ni wazi walikuwa bado wanatoa huduma."
Amit alizaliwa na aina ya 1 ya Neurofibromatosis, hali ambayo husababisha uvimbe usio na saratani kukua kando ya mishipa.
Lakini baada ya "kujifunza, kujikubali" kwa ulemavu wa uso wake, sasa anashirikisha umma hadithi yake kwa lengo la kuwasaidia watoto mashuleni "kukumbatia haiba zao na kusherehekea hali zao".

Chanzo cha picha, Amit Ghose
Amit aliondolewa jicho lake la kushoto kwa upasuaji akiwa na umri wa miaka 11, na kusababisha kuharibika zaidi kwa uso na hivyo kukabiliwa zaidi na unyanyasaji na unyanyapaa.
Mwaka mmoja kuelekea sherehe za Halloween , mtoto shuleni alimuambia "hauitaji kinyago cha Halloween, wewe ni kinyago cha kutosha kwa maisha yote", alikumbuka.
"Hilo lilinivunja moyo kiasi kwamba sikukubali upande wa kushoto wa uso wangu," alisema.
"Kwa muda mrefu sana nilificha uso, sikuwa na raha kuunyesha kwa ulimwengu hata kidogo."
Akiangalia maisha ya nyuma, alisema hakuelewa kina cha kukata tamaa na wasiwasi aliopata wakati huo.
"Watoto wengine ambao hawakutaka kuja kukaa karibu nami au kujificha nyuma ya wazazi wao wote waliniathiri kiakili ," alisema.
Shuleni, kriketi ilikuwa shauku yake na ilikuwa kupitia kucheza mchezo huo kwamba hatimaye alipata marafiki.
"Kriketi ilinisaidia kuwa Amit, yule mvulana anayecheza kriketi, mvulana ambaye ana uso wa kuchekesha," alielezea.

Chanzo cha picha, Amit Ghose
Lakini, alisema, hata akiwa mtu mzima bado "kutazamwa kwa mshangao mara kwa mara".
"Kunyooshewa kidole, marafiki kusema 'umeona uso wa mtu huyo', hilo pia ni jambo linalotokea kila wakati," alisema.
''Huyu ndiye mimi, mnikubali msinikubali''
Ni mkewe Piyali ambaye mwishowe alimfundisha "jinsi ya kujikubali," alielezea.
"Kwa kweli lazima nijikubali kabla ya wengine kunikubali," aliongeza.
Pia alimshawishi aanze kushiriki hadithi yake kwenye mitandao ya kijamii.
"Nilidhani TikTok ilikuwa kuhusu kuimba na kucheza, na nilifikiri labda sivyo, lakini alinishawishi.
"Niliunda video na nikauambia ulimwengu: 'Nataka kuwapeleka nyote kwenye safari ya kukusaidia na na kuwatia moyo kwa kutumia uzoefu wangu wa kuishi.'"
Alianza akaunti yake mapema 2023, na tangu wakati huo ameendelea kupata karibu wafuasi 200,000 na mamilioni ya watu waliopenda(likes), akaunti yake.
"Kwangu mimi kuwasaidia watu kwenye mitandao ya kijamii kwa kushiriki hadithi yangu imenisaidia kujikubali zaidi.
"Sasa ninauambia ulimwengu, huyu ni mimi, mnipende msinipende."

Chanzo cha picha, Amit Ghose
Karibu wakati huo huo, aliacha kazi yake katika kampuni ya mawakili ili kufanya kazi ya mazungumzo ya motisha wakati wote.
Kusaidia vijana ilimfanya ajihisi kuwa muhimu zaidi, alisema.
Pia anakaribia kuzindua kipindi cha mazungumzo ya matandaoni (podcast) ambapo atakuwa akizungumza na watu wengine ambao wamekuwa na uzoefu kama wake, akiwemo Oliver Bromley ambaye alifukuzwa kutoka kwenye mghahawa kwasababu wafanyakazi walisema "alikuwa akiwatisha wateja".
"Tutafurahishwa sana na kuwahamasisha watu wengi," alisema.
"Uwe mlemavu au usiwe mlemavu, sote tuna ukosefu wa usalama, sote tuna mambo ambayo tunakabiliwa nayo, na changamoto tunazokabiliana nazo.
"Nataka tu kutoa simulizi hii kwa watu kwamba ikiwa tutasherehekea kweli sisi ni nani, kujikubali tulivyo, tujipende tulivyo, basi tunaweza kuwa na ujasiri zaidi."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












