Watu wenye ulemavu waliovuka changamoto na kufikia mafanikio

Chanzo cha picha, Sophia Mbeyela
- Author, Na Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili News
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 10
Katika ulimwengu ambao mara nyingi huhusisha mafanikio na ukamilifu wa kimwili na kiakili, ni muhimu kufahamu kuwa kuna watu wenye ulemavu ambao wameweza kuvuka changamoto hiyo na kutenda mambo makubwa ambayo yanaweza kuwa mfano wa kuigwa duniani.
Katika historia, watu wengi maarufu wenye ulemavu sio tu kwamba wamebadili mtizamo na matarajio ya jamii kwamba hawana uwezo , lakini pia wameacha alama isiyofutika katika nyanja zao husika.
Katika Makala haya tunawaangazia baadhi ya watu wenye ulemavu ambao wamekuwa mashuhuri kwa kushinda changamoto ya ulemavu na kufikia mafanikio ya hali ya juu katika Nyanja zao. Hawa ni baadhi yao.
Sophia Mbeyela

Chanzo cha picha, Sophia Mbeyela
Sophia Mbeyela, ni mwanaharakati wa haki za walemavu nchini Tanzania mwenye ulemavu. Licha ya changamoto hiyo ameonekana kuwa mwanamke mwenye uwezo wa kuelimisha jamii, pia ameweza kujitoa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu walio katika makundi matatu -albino, walemavu wa viungo na yatima.
Sophia ambaye ni mwalimu wa sekondari ni Mkurugenzi mkuu na Muasisi wa taasisi ya walemavu -Peace Life for Persons with Disability Foundation (PLPDF) , shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania, linalowatetea na kuwawezesha watu wenye ulemavu ili kuwa na maisha huru na yenye kuridhisha.
Alilianzisha shirika hilo mwaka wa 2015 na kusajiliwa rasmi mwaka wa 2017, na tangu wakati huo limekuwa likitoa elimu ya ujasiriamali, msaada wa kiuchumi, na hatua za kujitambua ili kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu kote nchini.
‘’ Wazo la kuanzisha NGO lilikuja kutokana na kwamba mimi mwenyewe nimo ndani ya hilo kundi, niliona kuna pengo, katika jamii, wazazi, na watu wengi kwa ujumla hawajapata elimu kuelewa kuwa mtu mwenye ulemavu wana uwezo. Nilitaka kuonyesha kuwa hata kama mimi ni mlemavu nina uwezo wa kufanya zaidi ya vile wanavyofikiria’’, Sophia aliieleza BBC.
Mafanikio

Chanzo cha picha, Sophia Mayela
Kupitia taasisi yake (PLPDF) Bi Sofia mejitolea binafsi kuwa mfano wa kuionyesha jamii ya watu wenye ulemavu kuwa wanaweza kuishi maisha mema iwapo wataweka bidii katika uwezo walio nao.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
‘’Nimeweza kutoa elimu kubwa na kuhakikisha ujumuishi wa watu walemavu katika shughuli za kijamii’’, anajivujia Bi Mbeyela.
Mipango ya kielemu ya shirika lake imeweza kuathiri maisha ya maelfu ya watu wenye ulemavu kwa njia chanya, kwa kuwapatia maarifa, ujuzi na fursa za maisha bora ya baadaye.
‘’Nimeweza kuonyesha kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kutumia kitu chochote walicho nacho kufanya mambo ambayo yanaweza kuleta mabadiliko kwao na kwa jamii nyingine’’, anasema.
Kupitia shirika lake, ameweza kuchangisha pesa za ujenzi miundo mbinu inayowasaidia wanafunzi wanaoishi na ulemavu kusoma kwa urahisi ikiwemo shule ya sekondari ya wasichana jijini Dar es Salaam.
‘’@peacelifedisabilityfoundation tunapenda kuwashukuru watu wote 🙏 binafsi, makampuni,Bank na wadau mbalimbali mliojumuika nasi 2023 kufanikisha jambo hili kwa awamu ya kwanza kwa michango yenu ya vifaa na fedha tulifanikiwa kujenga jengo la vyoo rafiki maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya wasichana Jangwani Sekondari’’, Sophia Mbeyela aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa Instagram hivi karibuni.
Kutokana na kazi zake ameweza kutambuliwa na kupata tuzo mbali mbali kama vile, Tuzo ya teknolojia ya mawasiliano kutoka Chuo cha ICT technology nchini Misri -2019, Tuzo ya mwanamke wa shoka kutoka radio ya EFM Tz, kipengele cha harakati za usawa - 2023 Kutoka Taasisi ya tisha mama TZ - kwa harakati za elimu -2023. Panafrican awards - humanity and social justice awards- 2017, Tuzo ya Malkia wa nguvu awards Tz -2017 , 6 Tuzo ya Mwanamke hodari -2023 kutoa global peace foundation Tz na Tuzo ya Message of hope awards kutoka USA -2024.
Kwa sasa anapambana kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika kama viungo mbadala kwa watu wenye ulemavu ambavyo ni bei ghali vinapatikana kwa bei rahisi nchini Tanzania, na kuweza kuwafikia walemavu kuanzia mashinani Tanzania.
Stevie Wonder

Stevie Wonder, ni mwanamuziki hodari aliyepoteza uwezo wa kuona muda mfupi baada ya kuzaliwa kwa sababu ya matatizo ya kuzaliwa kabla ya wakati.
Alisajiliwa na Motown akiwa na umri wa miaka 11, baadaye angetawazwa kama msanii mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuwa na wimbo namba 1 kwenye Billboard Hot 100. Wonder aliendelea kuwa mmoja wa wanamuziki wenye ushawishi na mafanikio makubwa katika historia, akishinda Tuzo 25 za Grammy na kutengeneza orodha ndefu ya vibao visivyopitwa na wakati.
Mafanikio yake yanatumika kama ushuhuda wa wazo kwamba ulemavu si kizuizi bali ni fursa ya mitazamo na vipaji vya kipekee kustawi.
Timothy Wanyonyi Wetangula

Chanzo cha picha, Timothy Wanyonyi /Instagram

Chanzo cha picha, Timothy Wanyonyi/Instagram
Timothy Wanyonyi Wetangula ni wakili wa Kenya na mwanasiasa mwenye ulemavu anayehudumu kama mbunge binafsi anayewakilisha Eneo bunge la Westlands jijini Nairobi.
Licha ya kutokuwa na uwezo wa kutembea somi huyu wa sheria na siasa aliyehitimu katika vyuo vikuu vya India na Kenya, amesifika kwa kazi zake mbali mbali za kimaendeleo katika jimbo la Westlands.
Huku baadhi ya wabunge wa Kenya wakilaumiwa kwa kutowhudumiwa na kuwajali raia, Bw Wanyonyi amekuwa akipongezwa na wakazi wa Westlands na Wakenya kwa ujumla kwa shughuli za maendeleo anazozifanya katka jimbo hilo, na kuwapatia fursa ya kutoa mchango wao katika shughuli za maendeleo.

Chanzo cha picha, Timothy Wanyonyi/Instagram
Baadhi ya shuguli zinazompatia sifa ni pamoja kuwa mstari wa mbele katika kudhamini na kuchagisha fedha za elimu ya watoto kutoka katika familia zenye changamoto mbali mbali za kifedha waliofaulu, na ujenzi wa barabara:
''Leo, tumefungua barabara za Kangemi Gichagi, Kangemi Marenga Hinga Drive, na Kangemi Munene Roads! Kuunganishwa kwa barabara hizi ni muhimu itaboresha maisha ya kila siku na biashara huko Kangemi na Mt View. Asante, vijana wa Kenya, kwa kuleta mabadiliko. Sauti yako ni muhimu. Wacha tuendelee kusonga mbele kwa maisha bora zaidi! Westlands Ni Kazi Tu! '', aliandika Bw Wanyonyi kwenye mtandao wake wa Facebook kuhusu ufunguzi wa barabara.
Marehemu: Stephen Hawking

Chanzo cha picha, Getty Images
Stephen alikuwa mmoja wa watu wenye akili bora zaidi wa kizazi cha sasa. Mwanasayansi huyo wa nadharia ya fizikia, ambaye alikuwa na ugonjwa wa mishipa ya fahamu (ALS), alizaliwa mnamo 1942 huko Oxford. Alikuwa na mapenzi ya mapema kwa sayansi na alianza masomo yake ya shahada katika Fizikia akiwa na umri mdogo wa miaka 17. Katika njia ya haraka ya kufikia ubora wake , maisha yake yalibadilishwa milele, akiwa na umri wa miaka 21, aligunduliwa kuwa na amyotrophic lateral sclerosis (ALS), ugonjwa wa kupooza unaokua polepole ambao uliathiri polepole usemi, misuli na harakati zake.
Licha ya mapungufu ya kimwili yaliyosababiswa na ugonjwa huo, Hawking aliendelea kuwa mwanafizikia wa kinadharia, na mwandishi maarufu duniani. Kazi yake ya msingi katika fizikia ya shimo nyeusi na asili ya ulimwengu imeacha urithi wa kudumu, kuthibitisha kwamba nguvu za akili zinaweza kuvuka vikwazo vya mwili.
Christopher Reeve

Chanzo cha picha, Getty Images
Christopher Reeve anajulikana sana kwa jukumu lake la kitabia kama Superman katika miaka ya 1970 na 1980. Maisha yake yalibadilika sana wakati ajali ya alipokuwa amepanda farasi iliyomfanya kupooza kuanzia shingoni hadi miguuni.
Licha ya changamoto za kimwili, Reeve alikua mtetezi maarufu wa utafiti wa uti wa mgongo na akaanzisha Christopher & Dana Reeve Foundation. Uthabiti wake na azimio lake la kupata tiba ya kupooza umeendelea kuhimizwa katika utafiti wa jeraha harakati za kutafuta tiba ya jeraha la uti wa mgongo.
5. Nick Vujicic

Chanzo cha picha, Getty Images
Nick Vijicic ambaye alizaliwa bila miguu na mikono nchini Australia ni mtoto wa wahamiaji wa Serbia. Hali ya Nick Vujicic inajulikana kama ugonjwa wa tetra amelia. Anasema makuzi yake nchini Australia uligubikwa na uonevu, ubaguzi, na ugumu wa maisha - hadi kufikia hatua ambapo alijaribu kujiua ili kuepuka unyanyasaji.
Njiani, Vujicic alibadilisha vizuizi vya maisha yake kuwa fursa za kuzungumza kwa motisha na kuwatia moyo watu wengine. Kupitia hotuba na vitabu vyake, Vujicic anaeneza ujumbe wa matumaini, uthabiti, na nguvu ya mtazamo chanya katika kushinda dhiki.
Aaron Fotheringham

Aaron Fotheringham, anayejulikana pia kama "Wheelz," ni mwanariadha maarufu anayetumia kiti cha magurudumu ambaye hufanya hila zilizochukuliwa kutoka kwa mchezo wa kuteleza kwenye barafu na barabara maalum.
Alizaliwa Las Vegas akiwa na ugonjwa wa uti wa mgongo, ambao ulimfanya kupooza miguu yake.
Lakini hajawahi kukata tamaa, Fotheringham kwani alimua kuishi kwa msimamo wa kuwa mtizamo chanya kuhusu kiti chake cha magurudumu, ambacho kiligeuka na kuwa kiti cha kufikia ndoto zake za maisha aliyonayo sasa.

Kwa ari na ustadi usio na kifani, amekuwa mahiri kwa kuipinduka baiskeli yake ya magurugumu juu chini kuthibitisha kwamba uwezo wa mtu haufafanuliwa na vikwazo vya kimwili. Ameshinda Mashindano manne ya Wheelchair Motocross (WCMX) na mashindano mengine.
Zaidi ya mafanikio yake ya riadha, anatetea ushirikishwaji na imani kwamba kila mtu, bila kujali uwezo, anastahili nafasi ya kutekeleza ndoto zake.
Sudha Chandran

Chanzo cha picha, Getty Images
Mcheza densi wa kitamaduni wa Kihindi mwenye kipawa, Sudha alikabiliana na hali mbaya ya maisha akiwa na umri wa miaka 16 wakati ajali ya basi iliposababisha kukatwa kwa mguu wake mmoja.
Licha ya changamoto hii kubwa, hakukatiza ndoto zake. Sudha alirudi kwenye ulimwengu wa densi akiwa na kiungo bandia, akionyesha dhamira isiyo na kifani na kujitolea kwa ufundi wake.
Kurejea kwake katika densi kuliacha alama ya uigizaji mzuri katika tamthilia ya densi "Mayuri," filamu ya wasifu inayohusu maisha yake mwenyewe.
Michael J. Fox

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa kawaida tunapofikiria ugonjwa wa Parkinson, tunafikiria ugonjwa unaoonekana tu wakati wa uzee. Hii haikuwa hivyo kwa muigizaji aliyeshinda tuzo ya Golden Globe Michael J. Fox, ambaye aligunduliwa na ugonjwa wa Parkinson alipokuwa na umri wa miaka 29 pekee.
Tukio hilo lilibadilisha mwelekeo wa maisha ya mwigizaji wa Back To The Future.
Licha ya changamoto zinazoletwa na ugonjwa huo wa neva unaoendelea, Fox amebaki kuwa muigizaji hodari na mtetezi aliyejitolea wa utafiti wa Parkinson. Wakfu wake wa Michael J. Fox umechangisha mamilioni ya fedha kwa ajili ya utafiti wa Parkinson, na kusisitiza umuhimu wa ustahimilivu na ustahimilivu wakati wa matatizo.
Marlee Matlin

Chanzo cha picha, Getty Images
Marlee Matlin alipoteza uwezo wake wa kusikia akiwa na umri wa miezi 18, lakini aliibuka kama muigizaji mwenye kipawa na wa kwanza kiziwi kushinda Tuzo ya Academy kwa jukumu lake katika "Watoto wa Mungu Mdogo." Matlin ameendelea kuvuka vizuizi katika tasnia ya burudani, akitetea uwakilishi mkubwa wa watu wenye ulemavu katika filamu na runinga.
Muniba Mazari

Chanzo cha picha, Muniba Mazari/Instagram
Muniba alilazimika kutumia kiti cha magurudumu baada ya ajali mbaya ya gari katika nchi yake ya asili ya Pakistani ambayo iliharibu vibaya uti wake wa mgongo.
Wakati wa miezi mingi ya ukarabati wake, Muniba alianza kugundua kipaji chake cha kisanii. Huchora picha za kujieleza kama njia ya huzuni yake ya kibinafsi. Mtindo wa kipekee na mzuri wa Muniba ulivutia umakini mara moja. Alikua msanii anayetafutwa sana, akifanya kazi kwa kandarasi za kibinafsi kwenye miradi mbali mbali nchini Pakistan na nje ya nchi.
Umaarufu wake ulipokua kutokana na sanaa yake ya kipekee na hadithi ya kipekee, Muniba alianza kuchukua hotuba ya kuhamasisha na harakati za kibinadamu. Amepokea tuzo nyingi za kimataifa kwa kazi yake kwa miaka mingi na ni Balozi wa Kwanza wa Nia Njema kwa UN Women kutoka taifa lake la nyumbani la Pakistan.
Bethany Hamilton

Chanzo cha picha, Bethany Hamilton/ Instagram
Mnamo 2003, Bethany alinusurika shambulio la papa ambapo alipoteza mkono wake.
Bethany hakuruhusu jeraha lake kumkasirisha. Akiwa tayari ni mtelezi mahiri, Bethany alikuwa amerejea majini ndani ya wiki tatu hadi nne baada ya shambulio hilo. Alikua bingwa na ameshiriki mashindano ya kimataifa tangu wakati huo, akishinda mataji sita ya nafasi ya kwanza na tuzo zingine kadhaa za kifahari za michezo katika kipindi cha miaka kumi na tano iliyopita.
Kando na kushindana, Bethany huendesha kozi za kuwatia watu motisha na mabadiliko ya kimaisha anazozitoa kwa kutumia uzoefu wake mwenyewe na hadithi ya kutia moyo.
Ni dhahiri kwamba mafanikio haya ya binadamu, yanaonyesha kwamba talanta, azma ya mtu, na ujasiri vinaweza kushinda kikwazo chochote. Simulizi zao zinaendelea kuhamasisha na kutoa changamoto kwa mitazamo ya jamii, na kuufanya ulimwengu kuwa mahala panapojumuisha watu wote wenye uwezo . Hawajaruhusu chochote kusimama katika njia yao. Huenda wewe na mimi tumejifunza mengi kutoka kwao.














