Francine Niyonkuru: Mtangazaji habari asiyeona anayetimiza ndoto yake
Na Dinah Gahamanyi
BBC News Swahili

Si jambo rahisi kumkuta mwandishi wa habari asiyeona katika chumba cha habari, hususan barani Afrika, lakini mwanadada Francine Niyonkuru kutoka Burundi asiye na uwezo wa kuona amebadili mtizamo huo.
Bi Francine mwenye umri wa miaka 23, ambaye amekuwa na ndoto hiyo tangu alipokuwa mtoto anaelekea kuitimiza kwani sasa anafanya mazoezi ya kazi ya utangazaji habari katika kituo kimoja cha radio na televisheni cha kibinafsi mjini Bujumbura.
''Mimi tangu nilipokuwa darasa la nne nimekuwa nikitamani sana kuwa mwandishi wa habari anayetangaza habari redioni. Nilipokua nikienda mahali nikimsikiliza mwandishi wa habari nasikia raha sana. Nilikuwa namwambia Mungu... anajalie kuwa mwandishi wa habari’’, anakumbuka.
'Safari haikuwa rahisi'

Safari ya kuisaka ndoto ya uanahabari haikuwa rahisi kutokana na ulemavu wa kutoona ambao aliupata akiwa na umri wa miaka mitatu kulingana na wazazi wake.
Alikabiliwa na changamoto si haba hasa katika maisha yake ya shule:
‘’ Nilipokuwa katika shule ya msingi ya wasioona niliyoisomea Gitega mambo yalikuwa rahisi sana, walimu walinifuatilia kwa karibu hasa katika somo la hesabu, lakini nilipoingia shule ya sekondari mambo yalikuwa magumu sana mwanzoni kwa kuwa tulisoma na wanafunzi wasio na ulemavu.’’
Kutokana na uhaba wa shule za wasioona Bi Francine alilazimika kusomea katika shule iliyokuwa na wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu, na hivyo waalimu hawakuweza kumsaidi kimasomo, kwa sababu hawakuwa na ujuzi wa kuelewa lugha ya wasioona.
''Ilikuwa vigumu sana kwangu kuendana na kasi ya mwalimu kwa sababu walimu hawakujali wenye ulemavu wa kutoona. Hasa katika somo la hisabati na masomo mengine ya sayansi nilipata shida sana. Mimi nisiyeona nikimuambia- mwalimu mbona sielewi, nieleweshe, ananiambia sioni jinsi nitakavyokusaidia. Ilibidi niwe nawauliza wanafunzi wenzangu wanisaidie baada ya somo, mpaka nikazoea, haikuwa rahisi, na kutokana na tatizo hili ilibidi nirudie darasa la kwanza’’, anasema.
Licha ya changamoto hizi, Mwanadada huyu anasema kila mara alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora darasani wanaoongoza kwa kupata alama bora na hilo lilimpatia msukumo wa kuendelea na masomo hadi kumaliza chuo kikuu.
Chama cha wanaoishi na ulemavu wa kutoona nchini Burundi kinasema takwimu rasmi za zinaonyesha kuwa 4% ya raia wa Burundi zaidi ya milioni 12 wanaishi na ulemavu.
Japo hakuna takwimu rasmi za hivi karibuni za walemavu wenye ajira, Shirika hilo linasema wanaoishi na ulemavu wa viungo hupata ajira, lakini wenye ulemavu wa kutoona na kusikia hawaajiriwi.

'Bidii na motisha ya kazi'
Mhariri katika kituo cha redio anachofanyia mazoezi ya uandishi wa habari mjini Bujumbura anasema Francine Niyonkuru aliwashangaza kwa jinsi anavyoimudu na kuipenda kazi yake, jambo lililomfanya awe na msukumo zaidi wa kumsaidia kutimiza ndoto yake.
''Tangu afike hapa Francine tulimpokea kama wanafunzi wengine na tulikua tumesikia ni mwanafunzi mwenye akili, anayependa sana utangazaji, tukasema kwa kuwa anaipenda, ni vizuri sana kwa kuwa hawezi kufanya kazi hii bila kuipenda. Ni mwanafunzi ambaye ukimwambia afanye kitu fulani anakifanya bila tatizo lolote. Ni mwanafunzi msikivu na kila mara huuliza maswali ili kuelewa zaidi kile anachokifanya. Sisi tunamsomea na akishaandika anasoma kwa mwandiko wake wa wasioona kisha anaingia studio na kusoma habari. Hatuna shaka kazi hii anaimudu’’

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya kuishi na ulemavu wa kutoona Bi Francine ameweza kufanya kazi na kuchangamana na wafanyakazi wenzake bila tatizo lolote kutokana na uchapakazi wake na hulka yake ya ucheshi.
Waandishi wa habari wa kituo cha radio na televishen anakofanyia kazi wameiambia BBC kuwa walishangazwa na uwezo wa Bi Francine kikazi na namna anavyoweza kuwatambua licha ya kuwa haoni.
‘’Francine ni mcheshi na ni mtu anayeishi vizuri na watu…Ni mchapakazi na anapenda sana kuuliza maswali kikazi ili apate kuielewa vyema. Tumezoeana na wote anatufahamu ni mtu ambaye ni rahisi kufanya naye kazi. Huwa tunamsomea habari anaandika kwa lugha ya wasioona halafu anasoma. Francine anaposoma habari leo hakuna mtu anayeweza kufikiria kuwa haoni’’, anasema Bi Arlene Rene Irahoza, mwandishi wa habari wa Burundi
‘’Alipokuja kujizoeza kazi hapa katika redio yetu ilikuwa ni mshangao mkubwa kwa watangazaji wenzake – lakini wakati tu alipoanza kufanya kazi na sisi tukashangaa kwa jinsi alivyokuwa na motisha na bidii ya kufanya kazi. Kuishi naye tunaishi vizuri, ni mtu mwenye hadithi , ni mtu anayeishi vizuri na watu wengine’’, anasema Cadou Nshimirimana, mwandishi wa habari wa redeo na televisheni anakofanyia kazi Francine.

'...akasema alaa! Kumbe huoni...aliniblock?'
Ndoto nyingine aliyonayo Bi Francine Niyonkuru ni ya kupata mchumba atakayekuwa mwenza wake na baadaye kuanza naye familia.
‘’Mimi ni mlemavu wa macho lakini viungo vingine vya mwili vinafanya kazi, kwa hiyo ningependa kuwa na mpenzi wa kiume na baadaye kuwa familia yangu’’, Francine aliiambia BBC.
‘’Nina uwezo wa kutumia simu na huwa nina ‘chat’ na watu mbali mbali nina apu ya wasioona kwenye simu yangu ya Android, ninatuma hata jumbe kwenye 'status' yangu, kwa hiyo siku nyuma katika mawasiliano’’ , aliongeza.
Hatahivyo anasema anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuanzisha mawasiliano ya kimapenzi kwasababu ya ulemavu wa kutoona alionao kwasababu ‘’wanaume wanahofia kuwa na uhusiano na msichana asiyeona’’.
‘’Nikupe hadithi ...wakati mmoja mwanaume mmoja tulikua tunawasiliana kwa njia ya ujumbe wa WhatsApp, akaniambia ananipenda, mimi pia nilimwambia ninampenda baadaye aliniomba picha yangu nikamtumia, aliposema anitumie yake nikamwambia, mimi siwezi kukuona…sina uwezo wa kuona…akasema alaa! Kumbe huoni?, baada ya hapo hakuwahi kuniandikia tena wala kuwasiliana na mimi , aliniblock…nikakosa mpenzi hivyo’’, alisema Bi Francine huku akiangua kicheko.
'Wanaume msiogope walemavu'

‘’Sijui tatizo walilinalo wanaume, mtu kama mimi naweza kufanya kazi yoyote, wanaume msiogope walemavu, ukimpenda mtu mwenye ulemavu uwe tayari kumsaidia’’, aliongeza
Mwanadada huyu anasema anawashukuru wazazi wake kwa kumpatia fursa ya kupata elimu. Hata hivyo anajiona kama mwenye bahati kwani jamii bado inawachukuliwa watu wanaoishi na ulemavu kama watu wasio na uwezo.
Ni matumaini ya Bi Francine Niyonkuru kuwa baada ya kutimiza ndoto zake atapata uwezo wa kuwasaidia watu wanaoishi na ulemavu hususan wasichana kupata elimu ili waweze kujikimu kimaisha na kupata mume wa kuanza naye familia.

















