'Matusi na unyanyapaa havikunizuia kusoma'

Na Dinah Gahamanyi,

BBC News Swahili

f

Chanzo cha picha, Constance Katihabwa

Constance Katihabwa, mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi (albino), ni mmoja wa wanawake watatu wenye ulemavu huo ambao wameweza kukabiliana na matusi na unyanyapaa, na kufanikiwa kufikia lengo lao la kielimu.

Nchini Burundi ni wanawake takriban watatu ambao wameweza kuhitimu chuo kikuu, akiwemo Bi Constance ambaye sasa ni mwanasheria.

Anasema safari ya kupata elimu haikuwa rahisi kutokana na jinsi wanafunzi wenzake na walimu wanavyomchukulia kutokana na kuwa na rangi ya mwili tofauti na wengine.

"Kuanzia darasa la kwanza, wanafunzi wenzangu walininyanyapaa, na ndio nikajiona kweli niko tofauti na wengine…baadhi waliponitazama walikimbia. Nilihisi uchungu sana moyoni mwangu’’, anakumbuka Bi Constance

“Unakuta kuna watu wananipiga ili waone jinsi ngozi yangu inavyokaa, , wananitemea mate na wengine hata wananidunga vitu mwilini ili waone iwapo damu yangu nyekundu au la. Nilikuwa kila mara ninarudi nyumbani nikiwa na vidonda , kuna wengine nilikuwa napigana nao’’

Watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kawaida wana asili ya ngozi dhaifu sana ambayo huharibiwa na jua pamoja na vile vile uwezo wao wa kuona mbali huathiriwa, na hii haikuwa tofauti kwa Constance.

"Nilipokuwa darasani ilinilazimu kuamka na kwenda karibu na ubao ili niweze kusoma waalimu walichoandika, unaelewa. kwamba yote hayo hayakufanya iwe rahisi kwangu kuweza kujifunza."

Alipataje msukumo kuendelea na masomo?

Maelezo ya video, Constance Katihabwa: 'Matusi na unyanyapaa havikunizuia kusoma'
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 hakuacha kusoma kwa sababu ya matatizo haya.

Constance anasema kwamba alipata nguvu ya kuendelea kutokana na sala na ushauri wa mama yake aliyemwambia mara kwa mara asikatishwe tamaa na maovu anayotendewa.

“Ilikuwa neema ya Mungu kwa sababu kulikuwa na marafiki zangu walionifundisha kusali. Kitu kingine kilichonisaidia ni mama yangu ambaye kila mara aliniambia niwe mvumilivu, nisikatishwe tamaa na maovu ninayotendewa na watu’’, aliesema.

Anasema pia kwamba alipewa msukumo wa kutia bidii zaidi katika masomo yake kutokana na kwamba wale waliokuwa wakimtusi wengi walikuwa wakipata alama za chini na ‘’baadhi ya waalimu walinielewa na kunisaidia kimasomo, hilo lilinipa nguvu ya kuendea na bidii ya kusoma’’.

Ingawa hakuna takwimu zinazopatikana katika ngazi ya taifa, mahudhurio ya shule kwa walemavu wa ngozi bado ni ya chini sana kutokana na matatizo mbalimbali, mkiwemo kuungua na jua, majeraha ya mwili, ukosefu wa kinga ya jua na kofia, na baadhi kuuawa.

w

Chanzo cha picha, Constance Katihabwa

Maelezo ya picha, Constance Katihabwa alikuwa na wakati mgumu kusoma kwa sababu ya dharau na dhuluma alizopata kutoka kwa wanafunzi wenzake na walimu.

'Walimwambia, atakuuma usiku, umemfuata kwasababu ya pesa...'

Niliolewa kihalali na mwanaume mweusi, tuliyefahamiana tangu tulipokuwa shuleni pamoja,” alisema mwanamke huyu mwenye mtoto mmoja mweusi.

“Tulianza tukiwa marafiki wa kawaida, alikuwa akinisaidia kimasomo kutokana na vile alivyokuwa akiona wanafunzi wengine wakinitendea uovu, lakini baadaye kukwa na mapenzi kati yetu, na baada ya miaka minne tukafunga ndoa kisheria kama mume na mke.”, anakumbuka Bi Constance.

Aliendelea kusema kuwa familia ya mume wake hakiyafanya maisha yake yawe rahisi kwani walikuwa wakimwambia kuwa watamzaa watoto maalbino, tawaletea albino kwenye familia, na kwamba ni sawa na ameoa mnyama huku wakimshinikiza amuache.

‘’Walimwambia, atakuuma usiku, umemfuata kwasababu ya pesa ili baadaye umuuze upatiwe pesa".

Mume wangu hakuweza kuhimili shinikizo kutoka kwa familia yake na hatimaye baada ya kuishi naye kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne alikata tamaa na kuondoka, akaniacha na mtoto wake mmoja’’.

g

Chanzo cha picha, CONSTANCE KATHIBWA

‘Wazo la kuunda shirika la Live Together as a Family’

Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, Constance Katihabwa aliamua kuunda shirika ambalo linashughulikia maendeleo ya watu wenye ulemavu wa ngozi na familia zao linaloitwa Live Together as a Family au 'Ishi Pamoja kama Familia'

Uamuzi huu anasema ulitokana na matatizo aliyopitia maishani mwake.

“Nilifikiri kwamba nifanye jambo fulani ili nisaidie. Ninaona ukosefu wa haki niliotendewa, jinsi watu walivyokuwa wakininyanyasa, na nimekuwa mikiona kwamba kuna wengine kama mimi wanaokabiliwa matatizo sawa na yangu’’ anasema.

Lengo jingine la kuanzisha shirika hilo anasema ilikuwa ni kusaidia wale wanaokabiliwa na tatizo la saratani ya ngozi, ambapo watu wengi wenye ulemavu wa ngozi hufariki kutokana na saratani.

Katika jambo lililomsikitisha sana, alisema ni kifo cha mwanamke mmoja albino ambaye kwa ugonjwa wa saratani akizikwa mara moja kabla hata família yake kumuona.

‘’Jambo hilo liliniuma, nikajiuliza mtoto wenye ulemavu wa ngozi anazaliwa katika família ambayo haimpendi, anatendewa ukatili na família, anakua katika mazingira mabaya ya kunyanyapaliwa, kiasi kwamba hata anapokufa família yake haimtaki, hana wa kumlilia, yaani anakosa hata mtu wa kusema huyu ni mtu wetu ngoja tumzike kwa heshima."anasema.

Bi Constance aliiambia BBC kuwa katika shughuli zake za kuwasaidia wenye ulemavu wa ngozi aligundua kwamba walemavu wa ngozi na familia zao kwa pamoja wanakumbwa na unyanyapaa na dhuluma.

Ananatoa wito wa kuwepo kwa mashirika yanayowasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi na família zao kwa pamoja.

Anaiomba jamii ‘’kuacha kuwatesa na kuwanyanyapaa maalbino kwani kwa kile anachosema kuwa hakuna mtu anayeomba kuzaliwa akiwa na ulemavu huo’’