John Chilembwe: Mmalawi aliyejengewa sanamu Uingereza

Uwanja wa kihistoria wa Trafalgar Square katikati mwa London unatazamiwa kupata sanamu mpya siku ya Jumatano. Lakini wakati huu, sio kumbukumbu kwa mmoja wa mashujaa wa vita wa Uingereza au wafalme.

Badala yake litakuwa sanamu kubwa la mhubiri wa Kibaptisti wa Malawi na Mwafrika John Chilembwe, ambaye alipigana dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Sanamu hiyo, iliyopewa jina la Antelope, itakuwa sehemu mpya zaidi ya Nne Plinth - ambayo inachukuliwa kuwa mojawapo ya kamisheni maarufu zaidi za sanaa za umma duniani.

Tangu mwaka 2003, Plinth ya Nne imekuwa ikionesha vipande tofauti vya kazi za sanaa kila baada ya miaka miwili. Ingawa ilikusudiwa kuonyesha sanamu ya Mfalme William IV, ilibaki tupu kwa sababu ya uhaba wa pesa na sasa inaonesha sanaa ya muda, iliyochaguliwa kupitia mashauriano ya umma na kikundi cha utekelezaji.

Sanamu ya Chilembwe ya mita tano itakuwa ya kwanza ya Afrika katika Trafalgar Square. Akiwa amevalia shaba, Antelope anaweka tena picha maarufu iliyopigwa mwaka wa 1914 ya Chilembwe akiwa amesimama karibu na mmishonari Mwingereza John Chorley, nje ya kanisa lake katika kijiji cha Mbombwe kusini mwa Malawi.

Wakati wawili hao wakiwa wamesimama pamoja kwenye picha, linapokuja suala la sanamu huyo mchongaji ameongeza ubora kumaanisha kuwa sura ya Mmalawi huyo inavutia macho ya watu.

Msanii mzaliwa wa Malawi Samson Kambalu alitengeneza kipande hicho ili kumfanya Chilembwe kuwa mkubwa zaidi kuliko Chorley. Sanamu yake iko katika mita tano zaidi ya ile ya Chorley.

"Kwa kuongeza kiwango chake, msanii anamwinua Chilembwe na hadithi yake, akifichua simulizi zilizofichwa za watu wasio na uwakilishi katika historia ya Ufalme wa Uingereza barani Afrika, na kwingineko," imesema tovuti ya Meya wa London.

Ingawa mnara huo unachukua nafasi ya kwanza London, Chilembwe bado hajajulikana kwa wengi. "Watu wengi wanaweza wasijue John Chilembwe ni nani. Na hiyo ndiyo hoja nzima,'' anasema Kambalu, profesa msaidizi wa sanaa katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.

Chilembwe anajulikana sana kama mmoja wa Waafrika wa kwanza kupigana dhidi ya dhuluma za wakoloni katika Karne ya 20, akianzisha uasi dhidi ya Waingereza nchini Malawi (zamani Nyasaland) mnamo 1915.

Ingawa maasi hayo yalikuwa ya muda mfupi, matendo yake yalijirudia katika bara zima na kwingineko.

Chilembwe anachukuliwa kuwa alishawishi watu kadhaa wa ukombozi wa watu weusi, akiwemo mwanaharakati wa kisiasa wa Jamaica Marcus Garvey, na John Langalibalele Dube, rais mwanzilishi wa kile kilichokuja kuwa African National Congress (ANC) nchini Afrika Kusini.

Chilembwe alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1870, na alikulia katika Wilaya ya Chiradzulu kusini mwa Malawi.

Alikuwa mmoja wa watoto wanne, na baba yake alitoka kwa watu wa Yao na mama yake kutoka jamii ya Mang'anja.

Alipokuwa akikulia huko Chiradzulu, Chilembwe aliathiriwa sana na wamisionari wa Scotland waliokwenda Malawi kufuata nyayo za mgunduzi David Livingstone.

Hapa ndipo Chilembwe alipokutana kwa mara ya kwanza na mmisionari mwenye itikadi kali, Joseph Booth, ambaye kauli yake maarufu ilikuwa "Afrika kwa Waafrika".

Chilembwe akawa mmoja wa wafuasi wa awali wa Booth, na hatimaye wawili hao walisafiri hadi Marekani, ambako alisomea teolojia huko Virginia.

Wakati akiwa Marekani, Chilembwe alishuhudia mapambano ya Wamarekani wenye asili ya Afrika wakati wa ujenzi upya baada ya kukomeshwa kwa utumwa.

Miaka kadhaa baadaye, aliondoka Marekani akiwa na ujasiri wa kukabiliana na dhuluma za kikoloni alizoziona katika nchi yake.

Mara baada ya kurejea Malawi, Chilembwe aliyetawazwa alifanya kazi ya kuanzisha misheni huko Chiradzulu. Alijenga kanisa la matofali, shule kadhaa, na kupanda mazao ya pamba, chai na kahawa, kwa ufadhili wa kifedha kutoka Marekani.

Kupinga ukoloni

Alirejea na kuukuta upinzani unaokua kwa kasi dhidi ya utawala wa Uingereza, uliotokana na sheria mpya ambazo ziliwasukuma Wamalawi kutoka katika ardhi yao, huku wengi pia wakilazimishwa kufanya kazi kwenye mashamba yanayomilikiwa na wazungu chini ya mazingira duni.

Chilembwe alikuwa na malalamiko zaidi na wakoloni baada ya kuzuka kwa Vita vya Kwanza vya Dunia, ambapo askari wa Malawi walichukuliwa kwenda kupigana na jeshi la Wajerumani katika nchi ambayo sasa ni Tanzania. Akitangaza kutoridhika kwake, aliandika barua kwa gazeti pekee lililokuwa likitolewa wakati huo.

Inafikiriwa kwamba muda mfupi baada ya barua yake alianza kupanga uasi wake, ambao ulianza Januari 1915. Hata hivyo, jaribio la Chilembwe la kuwashambulia walowezi wa kizungu lilishindwa haraka na majeshi ya Uingereza yalikuwa kwenye tahadhari mapema.

Maasi yake yalidai majeruhi wachache tu, na jeshi la Uingereza lilitoa zawadi kwa Chilembwe na wafuasi wake.

Siku chache baadaye, aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Kiafrika alipokuwa akijaribu kuvuka katika nchi ambayo sasa ni Msumbiji.

Ingawa uasi wake haukufaulu, wanahistoria wanasema kwamba jaribio la Chilembwe lilijenga msingi wa harakati za kupigania uhuru wa Afrika.

Malawi ilipata uhuru mwaka 1964. Leo, urithi wa Chilembwe unaweza kuonekana kote Malawi. Barabara kadhaa zimepewa jina lake, huku picha yake ikionekana kwenye sarafu ya nchi hiyo, kwacha, pamoja na mihuri.

Siku ya John Chilembwe pia huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Januari.

Hata hivyo, wanahistoria wanasema kuna mjadala unaoendelea kuhusu umuhimu wake. "Kila mwaka katika Siku ya Chilembwe, magazeti na machapisho ya mtandaoni yataandika insha ili kujadili urithi wake," anasema mwanahistoria wa Malawi Muti Michael Phoya.

"Ingawa wengi wanakubali kwamba yeye ni muhimu sana katika historia ya Malawi, wengine wanasema alianzisha uasi mapema mno," aliendelea Bw Phoya. "Lakini sanamu ya Kambalu inaweza kufufua mazungumzo haya na tunaweza kuona nia mpya katika hadithi yake."

Kambalu anakubali akisema anatumai kwamba sanamu hiyo "itaanzisha mazungumzo nchini Uingereza ambayo bado yanakuja kujibu ukoloni wao wa zamani. "Sanamu yake inaleta mwangaza historia zilizosahaulika za ufalme huo, na jamii inatafuta utambuzi huo."