Vita vya Ukraine: Je nani anayeibuka mshindi?

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Vikosi vya Ukraine vimepata mafanikio ya haraka katika siku za hivi karibuni, na kuchukua tena maeneo makubwa kutoka Urusi.

Urusi inasema inajipanga upya na vikosi vyake bado vinashikilia karibu theluthi moja ya nchi.

Je mzozo umebadilikaje?

Urusi ilivamia Ukraine mnamo Februari 24, na kuuzunguka mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv. Pia ilianzisha mashambulizi kusini, mashariki na kaskazini mwa nchi.

Mapema mwezi Aprili, vikosi vya Ukraine vilitwaa tena maeneo makubwa karibu na Kyiv, baada ya Urusi kuachana na harakati zake kuelekea mji mkuu.

Tangu wakati huo Urusi imekuwa ikielekeza nguvu zake katika operesheni zake za kijeshi kusini, mashariki na kaskazini-mashariki mwa Ukraine, ikichukua maeneo makubwa.

Hata hivyo, mambo yalibadilika sana mwanzoni mwa Septemba.

Katika mashambulizi makali kaskazini-mashariki, Ukraine ilivirudisha nyuma vikosi vya Urusi. Inadai kuwa imepata tena kilomita za mraba 3,000 (maili za mraba 1,158) za eneo karibu na jiji la Kharkiv pekee.

Kwa jumla, Ukraine inasema imechukua tena zaidi ya kilomita za mraba 8,000 (maili za mraba 3,088) zilizokuwa chini ya udhibiti wa Urusi mnamo Septemba, mafanikio muhimu zaidi ya eneo tangu vita kuanza.

th

Miji ya Izyum na Kupiansk, ambayo Ukraine inasema walitwaa tena tarehe 10 Septemba, yote ilikuwa vitovu muhimu vya usambazaji wa vikosi vya Urusi. Kwa hivyo, hizi zinawakilisha faida muhimu za kimkakati.

Pia kuna mashambulizi yanayofanywa na Ukraine kuzunguka eneo la Kherson kusini mwa nchi.

Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) inasema kuwa wanajeshi wa Ukraine wamesababisha "ushindi mkubwa wa operesheni" kwa vikosi vya Urusi.

Justin Bronk wa Taasisi ya Royal United Services alisema maeneo ya Urusi huko Kharkiv yanakabiliana na "kuporomoka kabisa".

Kujiondoa kwa Urusi ilikuwa, alisema, "kwa hakika ni mabadiliko ya kushangaza zaidi ambayo tumeshuhudia kwa Urusi tangu walipoondoka Kyiv mwezi wa Aprili".

Je Urusi imejibu nini?

Urusi ilithibitisha kwamba vikosi vyake vilirudi nyuma huko Izyum na Kupiansk. Ilisema hiyo ulikuwa ni kujiondoa kimkakati ili "kujipanga upya".

Pia imesema itaendelea kulenga maeneo haya kwa mashambulizi ya kijeshi.

Jeshi la Urusi linaonekana kuwa limeacha idadi kubwa ya vifaa na risasi wakati wa kujiondoa.

Urusi bado inamiliki maeneo mangapi?

Urusi bado inashikilia takriban 20% ya Ukraine, kulingana na ISW.

Maeneo hayo kwa kiasi kikubwa yako katika eneo la mashariki la Donbas na kusini mwa Ukraine, pamoja na peninsula ya Crimea ambayo Urusi ililitwaa mwaka wa 2014.

th
Maelezo ya picha, th

Donbas ni eneo la watu wanaozungumza Kirusi na baada ya Urusi kuteka Crimea mnamo 2014, vikosi vinavyounga mkono Urusi viliteka zaidi ya theluthi moja ya eneo hilo. Iliunda jamhuri mbili zinazoitwa Jamuhuri za watu huko.

Maeneo ya magharibi mwa nchi, pamoja na Lviv, yamekumbwa na mashambulio ya makombora, lakini hakuna jaribio la vikosi vya Urusi kuchukua na kukalia ardhi hiyo.

Urusi inataka nini?

Urusi inakataa kutambua uvamizi wake kama vita, na inasema inafanya "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.

Kremlin ilisema shughuli zake zitaendelea "mpaka kazi zote zilizowekwa hapo awali" zitakapoafikiwa.

Wakati akianza uvamizi huo mwezi Februari, Rais Vladimir Putin alisema lengo lake lilikuwa "kuondoa vikosi vya kijeshi Ukraine"

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Lengo moja lilikuwa ni kuhakikisha Ukraine haijiungi na muungano wa kujihami wa Magharibi, Nato.

Madhumuni ya awali ya Urusi ilikuwa kupindua Ukraine na kuiondoa serikali yake.

Hata hivyo sasa inaonekana kuwa imepunguza matarajio yake ya kupata ardhi mashariki na kusini mwa Ukraine.

Ukraine inataka nini?

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema lengo lake kuu ni kuwafukuza wanajeshi wote wa Urusi, ili "kuchukua eneo letu lote".

Zelensky ameomba ufadhili zaidi na vifaa ili kulinda maeneo yaliyorejeshwa kutoka kwa Urusi.

Shehena za silaha za Magharibi zinatumiwa sana na vikosi vya Ukraine.

Je watu wangapi wamefariki?

Pande zote mbili zimepata hasara, ingawa hazichapishi idadi kamili.

Ukraine inadai kuwa imeua zaidi ya wanajeshi 50,000 wa Urusi, na mwishoni mwa Agosti ilisema imepoteza karibu wanajeshi 9,000 tangu kuanza kwa vita.

Urusi mara chache huweka wazi vifo vya wanajeshi wake. Hesabu yake ya hivi karibuni zaidi ya vifo ilikuwa mwezi Machi, iliposema wanajeshi 1,351 wa Urusi wamefariki tangu uvamizi huo uanze.