Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine: Jinsi Rais Erdogan anavyouma na kupuliza kwa ndimi mbili
Huku vita vya Ukraine vikiendelea, Uturuki imetoka kuwa mshirika wa nchi za Magharibi hadi kuwa mshirika wa karibu na wa Urusi, katika kile ambacho wengi wanakielezea kuwa ni mchezo wa pande mbili.
Mwanachama wa NATO na mshirika wa jadi wa Ukraine - ambaye inamuunga mkono katika madai yake ya eneo la Crimea na Donbas- Ankara ilijiweka upande huu dhidi ya Moscow mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi mwezi Februari.
Msaada wake haukuwa wa kisiasa tu bali pia wa kijeshi: alileta ndege zisizo na rubani za Bayraktar TB2 huko Kyiv, ambazo katika miezi ya hivi karibuni zimekuwa jinamizi kwa jeshi la Urusi. Hata hivyo, haikujiunga na kambi ya Magharibi katika vikwazo vya kifedha dhidi ya Urusi, nchi ambayo hata imeimarisha ushirikiano wake katika masuala ya uchumi.
Na mapema mwezi huu, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alishangaza ulimwengu kwa kuishutumu Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kufuata sera ya "uchokozi" dhidi ya Moscow. Pia aliipongeza Urusi - akitangaza, pamoja na mambo mengine, kwamba "haipaswi kudharauliwa" - na wiki hii amepangwa kukutana na kiongozi wake, Vladimir Putin.
Erdogan pia amedai sera ya "usawa", na hivyo kuthibitisha tena jukumu lake jipya kama mpatanishi katika mzozo huo. "Anatumia kadi ya Urusi katika uhusiano wake na Marekani na Magharibi, kwa sababu anajua kwamba Uturuki ni mshirika wa thamani kwao, na pia anatumia kadi ya Magharibi katika mahusiano yake na Urusi ", anafafanua Kerim Has, mchambuzi wa kisiasa wa Kituruki.
Mkakati huu wa ndimi mbili ama wa undumilakuwili, kulingana na baadhi ya wachambuzi, kwamba unaweza kuiletea Uturuki manufaa muhimu ya kiuchumi na kisiasa.
Pesa kwa ajili ya madaraka
"Erdogan anapenda vitu viwili: nguvu na pesa," anasema Has katika mahojiano na BBC Mundo. Rais wa Uturuki, ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miongo miwili, ameshuhudia umaarufu wake ukishuka katika mwaka uliopita, unaoakisiwawa na mdororo mkubwa wa kiuchumi.
Lira ya Uturuki imeshuka hadi chini ya nusu ya thamani yake katika miezi 12 iliyopita, wakati mfumuko wa bei umepanda zaidi ya 80%.
Na mnamo Juni 2023 kuna uchaguzi wa rais, ambao unaweza kutishia kuendelea kwake baada ya zaidi ya miaka 20 ya kuwa madarakani.
"Kabla ya uchaguzi, Erdogan anahitaji usaidizi mkubwa wa kiuchumi na kifedha na uwekezaji kutoka ng'ambo," kulingana na mtaalamu huyo, ili kufufua uchumi wa nchi na kuhakikisha uchaguzi wa marudio unafanyika vizuri.
Na Urusi, kwa upande wake, inahitaji mpatanishi ili kuepuka vikwazo iwezekanavyo na kuuza bidhaa zake kwenye masoko ya dunia.
"Uturuki imeona fursa ya kuwa kituo cha kibiashara na vifaa, na pia nchi ya daraja la uhusiano wa kiuchumi wa Urusi na Magharibi," Has alisema.
Kwa mantiki hiyo, taalam huyu anaelezea kwamba "makampuni mengi ya Magharibi ambayo yaliacha soko la Urusi kwa sababu ya vyanzo yamefungua vituo vya usafirishaji huko Istanbul ili kuendelea kudumu."
Na hivyo hivyo: "Wafanyabiashara wengi wa Kirusi wanaofanya biashara na nchi za Magharibi wamehamisha vituo, vifaa na biashara hadi Uturuki." Kwa upande mwingine, anasema, "kila siku tunaona kampuni fulani ya Kituruki yakiingia katika soko la Urusi kuchukua ya nafasi ya makampuni ya Magharibi ambayo yanajiondoa."
Biashara, uwekezaji na gesi
Vita hivyo pia vimeongeza biashara baina ya nchi mbili: Mauzo ya Uturuki kwa Urusi yaliongezeka kwa 75% mwezi Julai ikilinganishwa na mwezi huo huo kwa mwaka 2021, kulingana na ofisi ya takwimu ya Uturuki (Turk Stat).
Katika mkutano wao huko Sochi (Urusi) mwanzoni mwa Agosti, Erdogan na Putin walikubaliana kupanua biashara kati yao katika eneo la nishati, usafiri, fedha, kilimo na utalii kufikia kiasi cha biashara cha dola za Marekani bilioni 100.
Kiasi hicho ni kikubw aukilinganisha na mwaka 2021 ambapo biashara ilifikia dola za Marekani milioni 33,000.
Mfano mwingine wa utitiri wa fedha wa Urusi katika uchumi wa Uturuki ni uhamisho wa dola bilioni 20 za Marekani kutoka Urusi hadi Uturuki kwa ajili ya mradi unaoendelea wa kiwanda cha nyuklia cha Akkuyu kusini mwa nchi.
Katika sekta ya nishati, Uturuki pia inaweza kuchukua fursa ya hali ya sasa ya vita. Nchi hiyo ya Mediterranean, ambayo karibu nusu ya gesi yake iaagiza kutoka Urusi, imeomba kujadili punguzo la bei, Erdogan mwenyewe alisema kabla ya mkutano wake na Putin.
Urafiki wa mashaka
Isachenko anaamini kuwa, kwa vyovyote vile, mkakati wa Uturuiki wa kucheza pande zote mbili una mipaka, haswa kwa vile Uturuki ina mizozo muhimu ya kimaslahi na Urusi katika uwanja wa siasa za kijiografia.
"Upanuzi shughuli za kijeshi za Urusi katika Bahari Nyeusi unaleta wasiwasi mkubwa wa usalama kwa Uturuki," anasema.
Na anaona kuwa, kuhusu uchumi, kipaumbele cha Uturuki ni kulinda maslahi yake ya kijiografia na kisiasa, sio tu katika Bahari Nyeusi lakini pia katika Mashariki ya Kati, Mediterania ya Mashariki, Aegean au Caucasus Kusini.
"Kwa kweli Uturuki haitaki kuwa kaka mdogo wa Urusi au kutoka nje ya NATO au kambi ya Magharibi," anasema Has.