Mkuu wa genge la wahalifu anayeliongoza genge lake akiwa gerezani

o

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bishnoi amekuwa gerezani tangu 2015, sasa anazuiliwa mbali na jimbo lake la asili la Punjab yuko Gujarat.
    • Author, Soutik Biswas
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Siku ya Jumatatu, polisi wa Canada walitoa madai katika mkutano na waandishi wa habari kwamba maafisa wa serikali ya India walikuwa wakitumia "vikundi vya wahalifu kama kikundi cha Bishnoi" kuwalenga viongozi wa vuguvugu la pro-Khalistan, ambalo linataka kuwepo kwa nchi tofauti ya Sikh nchini India.

Hilo lilitokea saa chache baada ya nchi zote mbili kuwafukuza wanadiplomasia wakuu, huku mvutano ukiongezeka juu ya mauaji ya mwaka jana ya mtu anayetaka kujitenga wa-Sikh katika ardhi ya Canada.

Delhi iliyaita madai hayo ni "upuuzi," ikimshutumu Waziri Mkuu, Justin Trudeau kwa kuitumia jamii kubwa ya Sikh iliopo Canada kwa faida ya kisiasa.

Polisi wa Canada walimtaja Lawrence Bishnoi, mkuu wa genge mwenye umri wa miaka 31 kutoka India, ambaye sasa anafuatiliwa ndani na kimataifa.

Polisi wa India wanasema genge lake linatuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanasiasa mashuhuri jijini Mumbai mwishoni mwa juma. Watu wenye silaha walimpiga risasi Baba Siddique mwenye umri wa miaka 66 karibu na ofisi ya mwanawe.

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bishnoi ndiye mshtakiwa mkuu katika mauaji ya Sidhu Moose Wala, mwimbaji maarufu wa Kipunjabi, Oktoba 2022.

Washukiwa watatu wako kizuizini. Mtu anayeshukiwa kuwa mshirika wa Bishnoi amechapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba genge hilo ndilo linalohusika na mauaji hayo.

Bishnoi aliyekuwa mmoja wa watu wanaosakwa zaidi nchini India, yuko gerezani tangu mwaka 2015, kwa sasa yuko gerezani.

Polisi wanaamini ushawishi wake bado umeenea. Bishnoi ndiye mshtakiwa mkuu wa mauaji ya Sidhu Moose Wala, mwimbaji maarufu wa Kipunjabi aliyeuawa kwa kupigwa risasi karibu na kijiji chake Oktoba 2022.

Pia unaweza kusoma

Kumtishia Salman Khan

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polisi wa India wanahusisha genge la Bishnoi na mauaji ya Siddique (katikati); Salman Khan (kushoto) pia ametishiwa maisha
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka wa 2018, Bishnoi alipata umaarufu mkubwa kwa kumtishia nyota wa Bollywood, Salman Khan, akimshutumu kwa kuwinda swala wawili aina ya blackbuck – swala wanaoheshimika kwa jamii ya Bishnoi ya Rajasthan ambayo Lawrence anatokea.

Alipofikishwa mahakamani katika jiji la Jodhpur, aliviambia vyombo vya habari waziwazi: "Salman Khan atauawa hapa, Jodhpur... Kisha atajua kuhusu utambulisho wetu halisi." Kwa bahati mbaya, Siddique, mwanasiasa aliyeuawa, alikuwa rafiki wa karibu wa nyota huyo wa Bollywood.

Machi mwaka jana, kituo cha habari kilipeperusha mahojiano na Bishnoi kutoka ndani ya jela ya Punjab, na kusababisha mahakama kuu kuamuru uchunguzi ufanyike. Kivipi mfungwa mwenye ulinzi mkali aliweza kufanya mahojiano ya simu kutoka gerezani, bado ni kitendawili.

Wachunguzi kutoka serikali ya shirikisho wanaamini Bishnoi anaendelea kudhibiti genge lenye wanachama 700 kote Punjab, Haryana, Rajasthan na Delhi, linalojihusisha na unyang'anyi wa mali za watu mashuhuri, kusafirisha dawa za kulevya na silaha na kutekeleza mauaji.

Mshirika wake Goldy Brar, pia mshitakiwa mwenza katika mauaji ya Moose Wala, anaendesha genge hilo kutokea Canada, wanasema polisi. Bishnoi anakabiliwa na kesi zaidi ya 30, huku 19 zikisikizwa mahakamani.

"Anaendesha genge lake akiwa gerezani bila kuhitaji kuratibu kila kitu," anasema Gurmeet Chauhan, afisa mkuu katika kikosi kazi cha kupambana na magenge huko Punjab.

Historia yake

Bishnoi alizaliwa katika utajiri. Familia yake ni miongoni mwa familia tajiri katika kijiji chao huko Punjab, wanaishi katika jumba kubwa lililozungukwa na zaidi ya ekari 100 za ardhi.

Baba yake, aliyekuwa polisi wa zamani, aliacha kazi yake ili kutunza ardhi ya familia, mama yake alikuwa mfanyakazi wa nyumbani. Wanandoa hao wamezaa wana wawili Lawrence na Anmol - wote kwa sasa ni washukiwa wakuu wa mauaji ya Moose Wala.

Ramesh Bishnoi mwanafamilia, alimwambia Jupinderjit Singh, mwandishi wa habari wa gazeti la The Tribune na mwandishi wa kitabu cha Who Killed Moose Wala, kwamba Lawrence alipewa jina la afisa wa Uingereza Henry Montgomery Lawrence, mwanzilishi wa Shule ya Lawrence maarufu katika mji wa Sanawar.

Lawrence Bishnoi mwenyewe alikwenda shule, na akiendesha baiskeli yake mwenyewe akiwa tu darasa la nane na kuvaa viatu vya bei ghali - anasa ambazo hazijasikika kwa wengi. Anajulikana kwa kuwasaidia kimya kimya watoto wa eneo hilo walio na uhitaji.

ok

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Canada inadai India ilitumia "makundi ya uhalifu kama genge la Bishnoi" kuwalenga viongozi wanaounga mkono Khalistan

Akiwa na ndevu zake zilizokatwa vizuri, na kofia - mara nyingi Bishnoi huvaa mwonekano wa kawaida wa kijana. Wakati mmoja alipofikishwa mahakamani, alivalia fulana yenye picha ya Bhagat Singh, mwanamapinduzi wa India aliyeheshimika.

Katika video iliyosambazwa sana, iliyoripotiwa kurekodiwa gerezani, anasema: "Kuna hamu ya mapinduzi katika mioyo yetu. Hebu tuone adui ana nguvu kiasi gani.” Maana kamili ya maneno yake yanabaki kuwa na utata.

Kuibuka kwa Bishnoi ni tofauti na wahalifu wengine wote. "Licha ya kuwa gerezani, anaonekana kuendesha genge lake. Ni nani anayempatia vifaa au kuvifikia vyombo vya habari? Hilo asingeweza bila washirika wenye nguvu," anasema Singh.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah