Kiwanda cha samaki cha Wachina kinavyoleta dhiki zaidi nchini Gambia

.

Chanzo cha picha, TOM FORD

Uwekezaji kutoka China uliokaribishwa na serikali ya Gambia unazua taharuki kwa jamii ya wavuvi wanaosema kuwa kiwanda cha samaki kinachomilikiwa na Wachina kinatatiza maisha katika ufuo wao.

"Nimekuwa nikifanya kazi hapa kwa miaka 32," anasema Buba Cary, mvuvi kutoka Gunjur akizungumza kwa lugha ya Mandinka kupitia mfasiri. "Inaleta mateso kwetu tu," anasema, akiashiria jengo jeupe.

"Kabla ya kiwanda kuja hapa kulikuwa na samaki wengi baharini. Kama unataka samaki [sasa] unahitaji kuvuka mpaka hadi Senegal au Guinea-Bissau."

Kelepha Camara, ambaye anakuja katika ufuo huu kununua samaki na kuwauza nchini, anakubali, akisema kuwa imeongeza gharama ya samaki kwa wenyeji: "Kiwanda hiki hakitusaidii."

.

Chanzo cha picha, TOM FORD

Maelezo ya picha, Wavuvi wanasema kiwanda hicho kimevuruga soko kwani kinanunua kwa wingi na kulipa bei ya chini kuliko wanunuzi wengine

Wanaume hawa wanazungumza kuhusu kituo kinachoendeshwa na Golden Lead katika kijiji cha pwani cha Gunjur, ambacho kiko karibu kilomita 45 (maili 28) kusini mwa mji mkuu, Banjul.

Kwa jumla Gambia sasa ina viwanda vitatu kati ya hivi - vingine viwili, vinavyoendeshwa na makampuni tofauti, viko karibu kilomita 10 kaskazini na kusini mwa Gunjur, ambapo mafuta ya samaki na unga wa samaki huzalishwa na kusafirishwa kwenda China, Ulaya na kwingineko.

Kwa miaka mingi tasnia ya unga wa samaki imeibua maswali kuhusu uendelevu wake.

Inatumia kiasi kikubwa cha samaki, kama vile sardinella na bonga, ambao huchangia angalau nusu ya jumla ya ulaji wa protini nchini Gambia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shirika lisilo la kiserikali la Uholanzi la Changing Markets Foundation liligundua kuwa viwanda vikubwa zaidi vya unga wa samaki vilichangia 40% ya samaki wote wa Gambia wanaovuliwa kwa mwaka mmoja.

Gambia imekuza uhusiano wa karibu na China katika miaka ya hivi karibuni. Chini ya uongozi wenye utata wa Rais wa zamani Yahya Jammeh kiwanda cha kwanza cha samaki cha China kufunguliwa kilikuwa Gunjur, baada ya kupewa mkataba wa miaka 99 mwaka 2015 mara baada ya Gambia kuvunja uhusiano na Taiwan.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba sheria ya Gambia inakataza raia wa kigeni kukodisha ardhi kwa zaidi ya miaka 26, kulingana na shirika la uangalizi wa kisiasa la Watch Gambia.

Muda mfupi baada ya Bw Jammeh kuondoka madarakani kwa kusitasita 2017 na kwenda uhamishoni baada ya miaka 22 kwenye usukani - enzi iliyofichuliwa na Tume ya Ukweli, Maridhiano na Mafidia kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ufisadi - mrithi wake alikutana na mwenzake wa Uchina na kuendeleza urafiki wao.

Mwaka huo China ilighairi $12m ($10m) ya deni la Gambia na kuwekeza $28.7m zaidi katika kilimo na uvuvi.

Hifadhi ya Wanyamapori yachafuliwa

Bado jamii ya wenyeji huko Gunjur ilikuwa tayari haijafurahishwa na jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea na Golden Lead.

Mnamo tarehe 22 Mei 2017 - karibu mwaka mmoja baada ya kiwanda cha unga wa samaki kufunguliwa - rasi katika Bolong Fenyo, hifadhi ya wanyamapori iliyo karibu, ilijaa samaki waliokufa.

Mwezi uliofuata, Shirika la Kitaifa la Mazingira liliwasilisha kesi dhidi ya Golden Lead katika mahakama ya hakimu, ikidai maji machafu kutoka kiwandani ndiyo yalisababisha uharibifu huo.

.

Chanzo cha picha, TOM FORD

Maelezo ya picha, Golden Lead hulipa $5 kwa kikapu cha samaki - chini ya kiwango cha soko

Lakini shughuli zilianza tena kwa haraka baada ya suluhu ya nje ya mahakama ya dola 25,000 kufikiwa.

Kando na suala la uchafuzi wa mazingira, kampuni hiyo ililetwa katika kesi nyingine mahakamani.

Mwezi uliopita, Bamba Banja, mtumishi mkuu wa zamani wa serikali katika wizara ya uvuvi, alipatikana na hatia ya ufisadi kwa kupokea angalau malipo matano ya $1,600 kati ya 2018 na 2020 kutoka Golden Lead.

Alikanusha kuwa alipokea fedha hizo kuruhusu meli zilizozuiliwa kwa kujihusisha na uvuvi haramu, lakini alifungwa jela miaka miwili na kuamriwa kulipa faini.

Baadhi ya jamii ya Gunjur bado wana wasiwasi kuhusu viwango kuhusu uchafuzi wa taka na wavuvi mbalimbali na wafanyakazi wa kiwanda waliambia BBC mnamo Desemba 2022 kwamba walikuwa na matatizo ya ngozi baada ya kuingia baharini karibu na kiwanda.

Lakini hakuna ushahidi wa uhakika kwamba maradhi haya ni makosa ya kiwanda.

Kwa wengi huko Gunjur ni ukosefu wa samaki unaowakasirisha - wanasema samaki wanavuliwa kupita kiasi.

Golden Lead inapata kandarasi za miezi sita na wavuvi wengi wa Senegal wanatumia boti zenye nguvu. Wavuvi wenyeji wanatumia pirogi hawawezi kushindana nao.

Kiwanda kinanunua kwa wingi, na kulipa $5 kwa kikapu - mara tatu chini ya kile kinachopatikana katika masoko ya ndani.

Baadhi ya wavuvi wanakubali hili kwa kuwa ni mauzo ya uhakika, lakini imaaana kwamba samaki wachache wanapatikana kwa watu wa Gambia ambao huuza kwa Golden Lead wanapata pesa kidogo.

Kiasi kikubwa cha samaki kinachohitajika kwa ajili ya mchakato wa kiwanda kushuhudiwa wakati samaki wanaletwa.

Boti zinapowasili kiwandani, wanaume wengi hukimbia na kushuka ufukweni wakiwa na vikapu vizito vya kilo 50 (lb 110) vichwani mwao - kila mmoja akilipwa $0.50 kwa safari moja.

Athari kubwa ni kwamba samaki wanakuwa adimu zaidi katika soko la ndani - na wanazidi kuwa ghali.

.

Chanzo cha picha, TOM FORD

Wakazi wa Gunjur pia wanalalamika kwamba Golden Lead imevunja ahadi zilizotolewa kwa jumuiya ya wavuvi.

"Waliahidi kujenga barabara kutoka kijijini hadi ufukweni na waliahidi kujenga soko la samaki kwa jamii.

Waliahidi ajira 600 hapa katika jamii," Dembo Darboe, chifu wa kijiji cha Gunjur, anayejulikana kama "alkalo" , alisema.

Hakuna kati ya haya ambayo yamefanyika, ingawa anasema kijiji hupokea malipo ya kila mwezi ya karibu $815.

"Ikilinganishwa na walichonacho, hii sio kitu," chifu alisema.

"Tunaweza kuonyesha kutokupenda kwetu. Lakini mamlaka yapo mikononi mwa serikali."

Kulingana na mfanyakazi katika kiwanda hicho, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, ni raia 40 pekee wa Gambia wanaoajiriwa katika kiwanda cha Gunjur's Golden Lead, ambapo hali ni mbaya na malipo hayaridhishi ya takriban $60 kwa mwezi, wanalipwa pesa taslimu.

"Wanakata pesa kutoka kwa mshahara wangu kwa ushuru wa mapato na hifadhi ya jamii. Sina hata akaunti ya hifadhi ya jamii au nambari," alisema.