Ni nini kinachochochea mashambulizi zaidi ya Urusi dhidi ya Kyiv?

Kwa watu wa Kyiv, imekuwa kama kurudi ghafla katika siku za nyuma za kutisha.

Jumatatu hii, mji mkuu wa Ukraine ulipata mashambulizi ya kwanza ya makombora ya Urusi baada ya miezi kadhaa ya hali ya kawaida.

"Roketi hizo zilipiga katikati ya mji wa Kyiv wakati wa msongamano wa watu wakati watu walipokuwa wakielekea kazini.

Moja ilipiga sio tu Shevchenko Park, lakini uwanja wake wa michezo, ambapo watoto wangu walikuwa wakicheza ," mwandishi wa BBC Abdujalil Abdurasulov aliandika kutoka mji huo.

"Hisia ya wasiwasi imerudi Kyiv. Watu hawapuuzi tena ving'ora vya uvamizi wa anga, lakini wanaenda kwenye vyumba vya chini, kama walivyofanya Februari na Machi [mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi]," aliongeza.

Mashambulizi pia yaliripotiwa katika Mtaa wa kati wa Volodymyrska, ambapo katika nyakati za kawaida kuna maduka ya kuuza zawadi na kazi za mikono, na pia katika Hifadhi ya Taras Shevchenko, mbele ambayo kuna jengo la chuo kikuu, ambalo kuna mikahawa kadhaa na uwanja wa michezo.

Kwa ujumla, zaidi ya miji kumi na mbili ya Ukraine ilipigwa wakati wa shambulio hilo ambalo liliathiri miundombinu muhimu katika mikoa 12 tofauti na kusababisha kukatika kwa umeme katika mikoa 15 ya nchi, pamoja na Lviv, Kyiv na Zaporizhia.

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 14 na wengine 97 kujeruhiwa.

Kulipiza kisasi

Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mashambulizi hayo makubwa yalikuwa ya kulipiza kisasi mlipuko kwenye daraja linalounganisha Crimea -- peninsula ya Ukraine ambayo Mossu ilinyakua kwa upande mmoja mwaka 2014 -- na eneo la Urusi.

Rais aliilaumu serikali ya Ukraine kwa kile alichokitaja kuwa ni "shambulio la kigaidi" dhidi ya miundombinu hiyo, ambayo inachukuliwa kuwa njia muhimu ya Moscow kuwaweka wanajeshi wake wanaopigana nchini Ukraine.

Evgeny Popov, Naibu kutoka chama tawala cha United Russia, alikanusha ripoti kwamba Moscow inashambulia miundombinu ya kiraia nchini Ukraine.

"Jeshi letu halishambulii, si kulipua miji au miundombinu ya kiraia. Makombora yetu yote yanalenga miundombinu ya nishati, vituo vya mawasiliano na makao makuu ya kijeshi," Popov alikiambia kipindi cha BBC 4, World at One.

Licha ya hayo, uchambuzi uliochapishwa na The New York Times unaonesha kuwa hakuna uwezekano kwamba mashambulizi hayo yatakuwa na athari yoyote kwa uwezo wa kijeshi wa Ukraine kwa vile mashambulizi yalionekana kulenga zaidi vitongoji vya makazi na miundombinu ya kiraia.

"Wakati Wizara ya Ulinzi ya Urusi na Rais Vladimir Putin walielezea mashambulio hayo kama mashambulio ya makombora ya hali ya juu yaliyokusudiwa kulemaza uwezo wa Ukraine wa kupigana vita, ilikuwa ngumu kuona jinsi baadhi ya shabaha zinavyolingana na hilo.

Wakati mitambo ya nguvu na miundombinu ya mawasiliano ilishambuliwa siku ya Jumatatu, vivyo hivyo uwanja wa michezo wa watoto na daraja maarufu la waenda kwa miguu katikati mwa Kyiv," gazeti la kila siku la Marekani liliandika.

Popov, kwa upande wake, anahakikisha kwamba uharibifu uliosababishwa na miundombinu ya kiraia - ikiwa ni pamoja na bustani ya watoto huko Kyiv - ulisababishwa na mifumo ya kupambana na makombora ya Ukraine. Lakini sababu ya mashambulizi ni haya mapya ya Putin ni nini ?

Kati ya adhabu na athari ya kutisha

Katika kueleza mashambulizi hayo ya Urusi, wataalam wanataja mambo mbalimbali kuanzia hitaji la Moscow la kuiadhibu Ukraine kwa uharibifu wa daraja la Crimea hadi kutaka kuleta athari za kutisha kwa washirika wa Magharibi wa Kyiv.

Pia wanazungumza juu ya kupitisha mkakati mpya, wa kikatili zaidi wa kijeshi ili kubadilisha mafanikio yaliyopatikana na vikosi vya Ukraine katika wiki za hivi karibuni.

"Mashambulizi haya kote nchini ni ongezeko la kimkakati, ambalo dhumuni lake kuu ni kuiadhibu Ukraine kwa kile ambacho Putin anakiita 'shambulio la kigaidi' [kwenye daraja la Crimea]," anasema Frank Gardner, mwandishi wa usalama wa BBC.

Daraja hilo lina umuhimu mkubwa ambao unapita zaidi ya manufaa yake kama njia ya usambazaji kwa askari wa Kirusi huko Crimea.

"Shambulio kwenye daraja hilo lilikuwa pigo kwa Rais Putin, kwani daraja hilo ni ishara ya kunyakua kwake rasi ya Crimea," alisema Steve Rosenberg, mhariri wa BBC wa Urusi.