FBI yafichua njama ya miaka ya 1980 ya kumuua Malkia Elizabeth II

Malkia Elizabeth II na Ronald Reagan kwenye karamu ya San Francisco mnamo 1983

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Elizabeth II alikabiliwa na tishio la mauaji wakati wa ziara ya mwaka 1983 nchini Marekani, nyaraka mpya za FBI zilizotolewa zinaonesha.

Ofisi ya Upelelezi ya Shirika hilo imetoa kasha la faili zinazohusiana na safari za marehemu Malkia kwenda Marekani, baada ya kifo chake mwaka jana.

Zinaonesha jinsi FBI, ambayo ilisaidia kulinda usalama wa Ufalme wakati wa ziara zake, walivyohofia vitisho vya IRA.

Tishio la mauaji lilitolewa kwa afisa wa polisi huko San Francisco.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, afisa mmoja ambaye alitembelea baa ya Ireland mara kwa mara huko San Francisco aliwaonya maajenti wa shirikisho kuhusu simu kutoka kwa mtu ambaye alikuwa amekutana naye kwenye ukumbi huo.

Afisa huyo alisema mwanaume huyo alimwambia kuwa alikuwa akitaka kulipiza kisasi kwa binti yake ambaye "aliuawa katika Ireland Kaskazini kwa risasi ya mpira".

Tishio hilo lilikuja tarehe 4 Februari 1983 - takribani mwezi mmoja kabla ya ziara ya Malkia Elizabeth II na mumewe Prince Philip huko California.

"Angejaribu kumdhuru Malkia Elizabeth na angefanya hivyo kwa kuangusha kitu kutoka kwaenye Daraja la Golden Gate kwenye mashua ya kifalme ( Royal Yacht Britannia) wakati inasafiri chini yake, au angejaribu kumuua Malkia Elizabeth alipotembelea Mbuga ya Kitaifa ya Yosemite," hati inasema.

Kujibu tishio hilo, Huduma ya Siri ilikuwa imepanga "kufunga njia za kupita kwenye Daraja la Golden Gate wakati mashua inakaribia". Haijulikani ni hatua gani zilichukuliwa huko Yosemite, lakini ziara hiyo iliendelea. Hakuna maelezo ya kukamatwa yaliyochapishwa na FBI.

Akiba hiyo ya kurasa 102 ilipakiwa kwenye tovuti ya Vault, tovuti ya habari ya FBI, siku ya Jumatatu, kufuatia ombi la Sheria ya Uhuru wa Habari iliyowasilishwa na vyombo vya habari vya Marekani.

 Malkia Elizabeth II na Prince Philip walizungumza na walinzi wa Hifadhi ya Kitaifa wakati wa ziara ya Yosemite

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ziara nyingi za marehemu Malkia nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na ziara ya mwaka 1983 katika Pwani ya Magharibi, zilikuja wakati wa mvutano uliokithiri wakati wa Shida huko Ireland Kaskazini.

Mnamo 1976, marehemu Malkia alikuwa katika Jiji la New York kwa sherehe za miaka mia mbili za Marekani.

Nyaraka hizo zinaonesha jinsi wito ulivyotolewa kwa rubani kwa kurusha ndege ndogo juu ya Battery Park yenye maandishi yanayosomeka "England, Get out of Ireland." ("England, ondoka Ireland.")

Nyaraka hizo zinaonesha jinsi FBI walivyokaa macho kwa kile walichokiona kuwa uwezekano halisi wa vitisho kwa marehemu Malkia.

Binamu yake wa pili Lord Mountbatten aliuawa katika shambulio la bomu la IRA kwenye pwani ya County Sligo, Jamhuri ya Ireland, mnamo 1979.

Kabla ya ziara ya binafsi ya marehemu Malkia huko Kentucky mnamo 1989, mawasiliano ya ndani ya FBI yalieleza "uwezekano wa vitisho dhidi ya Ufalme wa Uingereza upo kila wakati kutoka kwa Jeshi la Irish Republican (IRA)".

Iliendelea kuwa "Boston na New York zinaombwa kusalia macho kwa vitisho vyovyote dhidi ya Malkia Elizabeth II kwa upande wa wanachama wa IRA na mara moja wawasilishe kwa Louisville," huko Kentucky.

Marehemu Malkia, ambaye alikuwa akimiliki farasi wa mbio, anajulikana kuwa alitembelea Kentucky mara kadhaa katika maisha yake ili kufurahia mambo muhimu ya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na Kentucky Derby. (Mbio za farasi za Kimarekani)

Katika ziara ya serikali mnamo 1991, marehemu Malkia aliratibiwa kuona mchezo wa mpira wa magongo (baseball) wa Baltimore Orioles na Rais George H Bush.

FBI ilionya Huduma ya Siri kwamba "vikundi vya Ireland" vinapanga maandamano katika uwanja wa michezo na "kundi la Ireland lilikuwa limehifadhi sehemu kubwa ya tikiti za jukwaa" kwa ajili ya mchezo.

Ofisi hiyo iliiambia NBC News kunaweza kuwa na "rekodi za ziada" ambazo zipo kando na zile zilizotolewa wiki hii, lakini haikuweka ratiba ya uchapishaji wao.