Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waafrika nchini Lebanon: 'Kila mtu chuoni ana wasiwasi'
Farai, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 27 kutoka Zimbabwe, amekuwa akiweka vitabu vyake vya masomo ya chuo kikuu kwenye dawati lake nyumbani mjini Beirut.
Lakini wiki hii, kwenye dawati lake ameweka hati za kusafiria, na pesa taslimu.
"Nimejipanga mwenyewe ikiwa nitahitaji kuondoka haraka," anasema.
Farai, ambaye jina lake tumelibadilisha ili kulinda utambulisho wake, alirudi Lebanon mwezi Septemba kumaliza mwaka wa mwisho wa shahada yake ya uzamili katika uhandisi wa mitambo.
Likizo yake ya msimu wa kiangazi alikuwa nyumbani Harare.
Alirejea akiwa na matumaini kwamba mgogoro utapungua. Lakini tangu Hamas ilipoishambulia Israel Oktoba 7 mwaka jana, kumekuwa na mashambulizi karibu kila siku kati ya Israel na Hezbollah, kundi la kijeshi linaloungwa mkono na Iran ambalo lina makao yake nchini Lebanon.
Wiki hii kumeshuhudiwa siku mbaya zaidi za vita nchini Lebanon katika kipindi cha miaka 20. Takriban watu 120,000 wameachwa bila makao tangu Jumatatu, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Jeshi la Israel linasema linafanya mashambulizi mapya "makubwa" kusini mwa Lebanon na eneo la Beqaa, kwa lengo la kuharibu miundombinu ya Hezbollah.
Wiki iliyopita, watu 39 waliuawa na maelfu wengine kujeruhiwa wakati waombolezaji na watu waliokuwa wakitumia redio za upepo zilizotumiwa na wanachama wa Hezbollah zilipolipuka kote nchini humo.
Hezbollah inasema kuwa inashirikiana na Wapalestina. Israel inasema inataka kuwasaidia raia wake ambao wameacha makazi yao karibu na mpaka kurejea kaskazini mwa Israel.
Marekani, Uingereza, Australia, Ufaransa, Canada na India zote zimetoa ushauri rasmi kwa raia wake kuondoka Lebanon haraka iwezekanavyo.
Wanafunzi wa Kiafrika wameiambia BBC kuwa sasa wanakabiliwa na mtafaruku - ama kubaki Lebanon wakati Israel ikiendelea kushambulia au kurudi nyumbani kwao katika nchi kama Uganda, Zimbabwe na Cameroon.
Katika chuo kikuu cha Marekani cha Beirut (AUB), ambapo Farai anasoma, kuna karibu wanafunzi wa Kiafrika wa 90 kwenye mpango wa masomo.
Farai anasema kumekuwa na "hofu kubwa" miongoni mwa wanafunzi, hasa tangu mlipuko wa pager (vifaa vya mawasiliano ya ujumbe na redio za upepo (walkie-talkie).
"Hatujui nanyi aliyebeba bomu linaloweza kulipuka mfukoni mwake," anasema.
"Je, ni dereva wako wa teksi? Je, ni dereva wako wa Uber? Je, ni mtu ambaye unatembea karibu naye?"
Wasiwasi kuhusu ya chuo
Kwa kawaida siku za Farai zilikuwa na shughuli nyingi za masomo madarasani na alikuwa amezoea kuona marafiki. Sasa anasema anaondoka tu nyumbani kwenda chuo kikuu na kununua vitu muhimu.
Hivi karibuni alihifadhi chakula muhimu kama vile mkate, tambi na maji ya chupa ili kujiandaa iwapo kutakuwa na uhaba wa chakula.
"Kila mtu ana wasiwasi. Hata njia ya kuwasiliana ni tofauti," anasema.
"Tunapomaliza darasa, profesa wetu sasa anasema muwe na siku nzuri na muwe salama. Tunasema hivyo kwa sababu tunajua kinachoendelea nchini."
"Hakuna mtu aliye salama."
Chuo cha AUB kilifunga siku ya milipuko ya pager, lakini sasa kimefunguliwa tena. Lakini hakuna shughuli za kufundisha, kama vile madarasa na mitihani, zitafanyika hadi Septemba 28.
Hii ni baada ya wizara ya elimu ya Lebanon kufunga shule za umma na za kibinafsi siku ya Jumanne hadi mwishoni mwa wiki.
Wizara hiyo imesema shule za umma zitatumika kuwahifadhi watu waliohamishwa kutokana na mashambulizi ya anga kusini mwa nchi hiyo.
Mapema wiki hii chuo kikuu cha Lebanon pia kilitangaza kuwa vyuo vikuu vyake vitafungwa hadi Jumatatu tarehe 30 Septemba.
Mpango wa masomo unaofadhili wanafunzi wa Kiafrika katika chuo cha AUB umewapa wanafunzi wa kimataifa fursa ya kwenda nyumbani na kumaliza kozi yao mtandaoni.
Lakini baadhi ya wanafunzi wanasema hilo haliwezekani.
Sharon Atyang, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 27 kutoka kaskazini mwa Uganda, kwa sasa anamaliza masomo yake ya uzamili katika kitivo cha maendeleo ya jamii katika AUB.
Anasema matatizo ya ukosefu wa umeme na intaneti yatafanya kuwa vigumu kukamilisha masomo yake mtandaoni.
"Mimi pia niko kwenye mpango wa masomo nya ufadhili, na sijui kama nitasafiri nyumbani wangenirudisha hapa ikiwa hali itatulia," anasema.
Adele kutoka Cameroon, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, pia anasema kumaliza shahada yake ya kwanza ya tiba ya mionzi (radiology) nyumbani itakuwa vigumu.
"Siwezi kufanya mazoezi yangu ya kazi katika kliniki nyumbani, wakati ninahitaji kukamilisha kama sehemu ya shahada yangu," anasema.
Ikiwa kuna shambulio jingine mjini Beirut, masanduku yake yameandaliwa tayari.
"Nina kila kitu tayari kwenda."
Mpango wa ufadhili wa masomo wa Mastercard, hufadhili wanafunzi kadhaa wa Kiafrika nchini Lebanon.
Wakfu wa Mastercard Foundation umesema unafuatilia kwa karibu maendeleo na kufanya kazi na AUB kuwasaidia wanafunzi.
Msemaji wake alisema: "AUB inawasiliana mara kwa mara na wanafunzi na umetoa msaada kwa afya na wa kimaisha."
"Mtaala wa kitaaluma unabaki kuwa rahisi na makazi maalumu yameandaliwa kwa ajili ya uhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa kitaaluma kwa wanafunzi walioandikishwa. Wanafunzi wa kimataifa ambao wanataka kurudi nyumbani wanasaidiwa kufanya hivyo."
Wakati bado inawezekana kuondoka Beirut kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa, ni vigumu kupata ndege. Mashirika kadhaa ya ndege kama vile Emirates, Qatar Airways, Air France na Lufthansa yamesitisha safari zake za ndege kwenda na kutoka mjini Beirut.
'Hatuwezi kuwa makini'
Mwanafunzi mwingine, Sharon anasema kutoka chumba chake cha kulala mjini Beirut anaweza kusikia sauti za milipuko inayosababishwa na ndege za kivita za Israel zinazopaa juu ya anga la Beirut.
"Nilikuwa katika chumba cha kusoma na niliposikia sauti ya mlipuko, nilikimbia tu. Lakini sikuwa na mahali pa kukimbia. Nilijikuta nimejificha kwenye choo," anasema.
Mfadhaiko wa kusubiri shambulio lingine umemwacha "kihisia na kiakili - [haiwezekani] kufanya chochote".
Alisema wanafunzi wengi wamewaomba maprofesa wao kuongeza muda wa mwisho wa kazi.
Kati ya kujaribu kusoma na kuandika utafiti wa masomo yake, Sharon pia anajibu simu za uwongo kutoka kwa familia yake kurudi nyumbani Uganda.
"Wanadai nirudi nyumbani, wananiambia ninahitaji kuweka kipaumbele maisha yangu mbele ya wasomi."
Baadhi ya serikali za Afrika zimeanza kuwahamisha watu.
Serikali ya Kenya inawaondoa raia wake kutoka Lebanon.
Katibu Mkuu wa Masuala ya Diaspora nchini Kenya, Roseline Njogu, alithibitisha kuwa Wakenya tisa waliwasili nchini mwezi Agosti.
Aliwataka Wakenya wengine wanaotaka kuondoka kujisajili kwa ajili ya kuondolewa huko na ubalozi huo. Kwa sasa kuna takriban Wakenya 26,000 nchini Lebanon.
Mwezi uliopita, msemaji wa zamani wa serikali ya Ethiopia katika wizara ya mambo ya nje, Nebiyu Tedla, aliiambia BBC kuwa wanafuatilia kwa karibu hali hiyo na "wanaandaa mipango ya kuondoka ikiwa ni lazima".
Aliongeza kuwa kuna takriban Waethiopia 150,000 nchini Lebanon, wengi wao ni wafanyakazi wa ndani.
Baadhi ya wafanyakazi hawa wanakabiliwa na changamoto za ziada wanapofanya kazi chini ya mfumo wa kafala wa Lebanon, ambapo lazima waombe ruhusa kutoka kwa waajiri wao kuondoka.
Kwa wanafunzi kama Farai na Sharon, kutoka Lebanon inaweza kuwa rahisi kujiandaa kuondoka. Lakini wanazuiwa na tamaa yao ya kumaliza masomo yao.
Wote wawili wanasema watafanya uamuzi katika siku chache zijazo.
Sharon anasema kuwa ni vigumu sana kwa wanafunzi wa Afrika.
"Ni juu yako mwenyewe, na unapaswa kujitunza mwenyewe," anasema.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi