Watoto wanne 'wakongwe' zaidi kuwahi kuzaliwa duniani

S

Chanzo cha picha, IS

Muda wa kusoma: Dakika 5

Familia moja nchini Marekani imeandika historia mpya katika matumizi ya teknolojia ya uzazi, baada ya kupata mtoto wa kiume, Thaddeus Daniel Pierce, anayetajwa kama "mtoto mkongwe zaidi duniani" aliyezaliwa kutoka kwa kiinitete kilichohifadhiwa kwa zaidi ya miaka 30.

Lindsey na Tim Pierce walichukua kiinitete hicho kilichogandishwa mwaka 1994 kupitia mpango wa "embryo adoption" na kukiwekwa kwenye tumbo na kuzaliwa kwa Thaddeus mnamo Julai 2025. Hii ikavunja rekodi zilizopita. Tukio hilo limeelezwa na MIT Technology Review na The Guardian kama mfano wa tukio "kama filamu ya kisayansi," ambapo kiinitete kilihifadhiwa kwa zaidi ya miaka 30 na baadaye kikawa chanzo cha maisha.

Uwezo wa kiinitete hicho kuishi katika hali ya fya na kutumika kikamilifu huonesha jinsi teknolojia ya IVF na cryopreservation zilivyofika mbali. Kabla ya Thaddeus, waliwahi pia kuwepo watoto ambao pia walikuwa na rekodi ya muda mrefu ya kiinitete na sasa tunaelewa ni kwa nini Thaddeus ameingia vikao vya historia.

Hapa chini zipo watoto watatu wa kihistoria waliowahi kushika rekodi za muda mrefu wa kugandishwa kabla ya kuzaliwa:

1. Thaddeus Daniel Pierce

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Thaddeus Daniel Pierce yeye anaongoza rekodi rasmi, kwani kiinitete chake kiligandishwa mwaka 1994, na kuzaliwa Julai 2025, hivyo kikihifadhiwa kwa zaidi ya miaka 31.

Lindsey, 35, na Tim Pierce, 34, walimpata mtoto huyu wa kiume, Thaddeus Daniel Pierce, siku ya Jumamosi juma hili. Kama angezaliwa wakati huo, sasa angekuwa na umri wa miaka 31, 'tofauti ya miaka 3 na 4 na wazazi wake wa sasa'.

Kufikia sasa hii ndiyo rekodi ya dunia inayoaminika kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari vya kimataifa kama The Guardian na MIT Technology Review. Ikivunja rekodi ya mapacha waliozaliwa mwaka 2022 kutokana na kiini tete kilichogandishwa mwaka 1992.

1. Lydia na Timothy Ridgeway – Miaka 30

S

Chanzo cha picha, National Embryo Donation Center

Rokodi ya awali ilikuwa inashikiliwa na mapacha hawa waliozaliwa 2022 kutokana na kiini tete kilichogandishwa mwaka 1992.

Mnamo Oktoba 2022, pacha Lydia Ann na Timothy Ronald Ridgeway walizaliwa Marekani kupitia kiinitete kilichogandishwa Aprili 22, 1992, karibuni miaka 30 kabla ya kuzaliwa kwao.

Mbali ya uzazi wa kawaida, viinitete hivyo vilitolewa kupitia National Embryo Donation Center (NEDC), benki ya kitaifa ya viinitete, na kupandikizwa ndani ya tumbo la mama yao Rachel Ridgeway.

Kwa mujibu wa CNN na Live Science, wazazi hao walikuwa na historia ndefu ya uzao hata tangu utoto wa baba yao mwenyewe". Lydia alizaliwa akiwa na uzito wa paundi 5.6 (takriban kilo 2.5) na Timothy alizaliwa akiwa na pauni 6.4 (kilo 2.9), wote wakiwa na afya imara kwa mujibu wa Live Science.

Tukio hili la Ridgeway lilichukua vichwa vya habari kwa muda na kuweka rekodi mpya ya muda wa kiinitete kilichogandishwa kwa miaka mingi na kufanikiwa kusababisha uzazi.

2. Molly Everette Gibson – Miaka 28

Molly Gibson alizaliwa Oktoba 26, 2020, kutokana na kiinitete kilichogandishwa Oktoba 1992, takribani miaka 28 kabla ya kuzaliwa kwake.

Mchakato ulifanyika kupitia NEDC, ambapo wazazi wake Tina na Ben Gibson walichukua kiinitete ambacho hapo awali kilitumika kusababisha kuzaliwa kwa Emma, dada yake mkubwa.

Kwa mujibu wa NBC News, kiinitete hicho kilipimwa na kuonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kuendelea kwa afya yake hata baada ya miaka 28, na kuzaliwa kwa Molly kulitangazwa kama rekodi mpya wakati huo.

Molly alizaliwa akiwa na afya nzuri na uzito wa karibu kilo 3, huku daktari akithibitisha kuwa maendeleo yake yalikuwa sawa na ya watoto wengine wa kawaida. Kufanikiwa kwa Molly kulionyesha wazi uwezo wa viinitete kuhifadhiwa miongo mingi bila kupoteza uwezo wa kuzaa.

3. Emma Wren Gibson – Miaka 24

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Mnamo Novemba 25, 2017, Emma Wren Gibson, dada mkubwa wa Molly, alizaliwa kupitia kiinitete kilichogandishwa mnamo 1992, miaka 24 kabla ya kuzaliwa kwake. Kiinitete hicho kiliwekwa katika benki ya viinitete ya NEDC kama sehemu ya mpango wa uhisani, ambapo wazazi wengine huasili viinitete vilivyotolewa kwa watu wenye shida ya kupata ujauzito.

Kwa mujibu wa The Guardian na Embryo Donation Stories, Emma alikuwa mtoto wa kwanza kuthibitishwa kuzaliwa kutoka kwenye kiinitete kilichohifadhiwa kwa kipindi cha miaka 24, tukio lililonogesha teknolojia ya IVF duniani kote katika enzi hiyo (embryodonation.org).

Mama yake, Tina Gibson, aliwaambia waandishi kwamba licha ya kiinitete kuwa na miaka mingapi, afya ya Emma ilikuwa bora na maendeleo yake kuonekana kawaida kabisa. Tukio hili lilichochea visa vya baadaye kama vile Molly na pacha wa Ridgeway kuvunja rekodi.

Jinsi teknolojia hii ya uzazi ya ajabu inavyofanya kazi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hizi ni baadhi ya vyombo vyenye baridi sana vinavyohifadhi viini tete kwa miaka na miaka
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Teknolojia ya kugandisha na kuhifadhi viinitete kwa Kiingereza embryo freezing au embryo cryopreservation ni mchakato wa kuyahifadhi mayai yaliyotungishwa au kurutubishwa na mbegu za kiume na kuhifadhiwa katika jokofu maalumu lenye baridi kali, kwa kutumia nitrojeni, hadi pale yatakapohitajika kutumika baadaye.

Mara nyingi, viinitete hivi hutungishwa kupitia teknolojia maalumu inayoitwa In Vitro Fertilization (IVF), ambapo yai la mwanamke na mbegu ya mwanaume huunganishwa maabara kisha kuhifadhiwa kama kiumbe chenye seli chache.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi wa National Embryo Donation Center (NEDC), Dkt. Jeffrey Keenan, "viinitete vinaweza kukaa salama hata kwa zaidi ya miaka 30 iwapo vitahifadhiwa katika hali ya baridi ya inayofikia nyuzi joto ya chini ama hasi -196, na bado viwe na uwezo wa kutungwa na kuleta ujauzito kamili."

Wataalamu wamebaini kwamba ubora wa kiinitete kabla ya kugandishwa ndio huchangia mafanikio makubwa ya ujauzito baadaye, hata kama miaka imepita mingi.

Licha ya kuonekana kama jambo la ajabu kwa wengi, tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa watoto wanaozaliwa kutoka kwa viinitete vilivyogandishwa hawana tofauti yoyote kiafya na wale waliotungwa kwa njia ya kawaida.

Kwa mujibu wa ripoti ya American Society for Reproductive Medicine (ASRM) na tafiti zilizochapishwa katika jarida la Fertility and Sterility, hakuna ongezeko la matatizo ya kimaumbile au ya ukuaji kwa watoto wanaotokana na viinitete vilivyohifadhiwa kwa muda mrefu. Dkt. Zaher Merhi, mtaalamu wa magonjwa ya uzazi wa IVF nchini Marekani, aliwahi kusema: "kiinitete kilichogandishwa huwa kama "kukilaza kiumbe usingizini" bila kuharibu uwezo wake wa maisha kikiamshwa, huendelea kukua kama kawaida".

Ni mafanikio haya ya teknolojia ambayo yameleta miujiza ya uzazi kwa maelfu ya familia duniani kote na sasa kuandika upya historia kupitia watoto kama Thaddeus.