Mtoto 'mkongwe' zaidi duniani azaliwa baada ya miaka 30

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Danai Nesta Kupemba
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Familia moja nchini Marekani imejaaliwa kupata mtoto wa kiume aliyezaliwa kutokana na kiini tete kilichogandishwa kwa zaidi ya miaka 30, na kuandikisha historia mpya duniani.
Lindsey, 35, na Tim Pierce, 34, walimpata mtoto wao wa kiume, Thaddeus Daniel Pierce, siku ya Jumamosi. Pierce aliiambia mtandao wa MIT Technology Review kwamba familia yake ilifananisha tukio hilo na " kitu kama filamu ya kisayansi ".
Inaaminika kuwa huo ndio muda mrefu zaidi ambao kiini tete kimewahi kugandishwa kabla ya mimba kutungishwa na hatimaye mtoto kuzaliwa. Rokodi ya awali inashikiliwa na pacha waliozaliwa 2022 kutokana na kiini tete kilichogandishwa mwaka 1992.
Pierce na mpenzi wake walijaribu kupata mtoto kwa miaka saba bila mafanikio kabla ya kuamua kuasili kiini tete cha Linda Archerd, 62, kilichotengenezwa kutokana yai lake na manii ya mume wake wa zamani mwaka 1994, na mimba kutungishwa kwa njia ya upandikizaji inayofahamika kwa kimombo In Vitro Fertilization (IVF).
Wakati huo, Bi Archerd alitengeza viini tete vinne. Moja ilichangia kuzaliwa kwa binti yake ambaye sasa ana umri wa miaka minne na tatu zilizobaki zikahifadhiwa.
Licha ya kutengana na mume wake, hakutaka viini tete vyao vilivyohifadhiwa kuharibiwa, kutolewa kama msaada kwa utafiti au kutolewa kwa familia isiyojulikana.
Alisema ni muhimu ahusishwe na mtoto huyo, kwani watakuwa na undugu na binti yake mkubwa.
Bi Archerd alilipa maelfu ya dola kwa mwaka kuhifadhi viini tete hivyo hadi alipopata shirika la Kikristo la kuasili kiinitete kwa jina, Nightlight Christian Adoptions, ambalo linaendesha mpango inayojulikana kama Snowflakes. Kiwango kikubwa cha mashirika hayo yanachukulia mipango yao kuwa ya kuokoa maisha.
Mpango unaotumiwa na Bi Archerd unaruhusu wafadhili kuchagua wanandoa, kumaanisha kwamba wanaweza kuzingatia misimamo yao kidini, rangi na utaifa.
Bi Archerd alipendelea wenzi wa ndoa wa kizungu na kihindi (Caucasian), Wakristo wanaoishi Marekani, kwani hakutaka wa "kutoka nje ya nchi", aliambia MIT Technology.
Hatimaye aliendana na matamanio ya Pierce na mpenzi wake.
Kliniki ya IVF ya Rejoice Fertility mjini Tennessee ambapo wanandoa hao walifanyiwa utaratibu huo, ilisema lengo lake lilikuwa kupandikiza kiini tete chochote kilichopokea, bila kujali umri au masharti.
Bi Pierce alisema yeye na mumewe hawakuwa na nia ya "kuvunja rekodi yoyote", bali "walitaka kupata mtoto tu".
Bi Archerd aliiambia MIT Technology kuwa bado hajakutana na mtoto huyo ana kwa ana, lakini tayari anahisi kuwa anafanana na binti yake.












